TRA YAZINDUA MFUMO WA TANCIS ULIOBORESHWA NA TOVUTI MPYA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Tovuti mpya na mfumo wa TANCIS ulioboreshwa utakaosaidia kurahisisha uondoshaji wa shehena Bandarini, katika Viwanja vya Ndege pamoja na mipakani.

Akizindua mfumo huo leo Januari 20, 2025 Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi ya TRA Mussa Uledi amesema mfumo wa TANCIS utapunguza kuonana kwa watu baina ya TRA na Walipakodi ambapo shughuli zote zitafanyika mtandaoni huku Tovuti mpya nayo ikirahisisha upatikanaji wa taarifa.

Uledi amesema mfumo wa TANCIS ulioboreshwa utasaidia kuongeza mapato ya TRA kwa upande wa Forodha kutokana na shughuli zote za ukadiriaji wa Kodi utafanywa na mfumo kwa usawa.

Amesema mfumo huo umeunganishwa na mifumo 36 ya taasisi nyingine na kuzitaka taasisi zilizounganishwa na mfumo huo kuhakikisha mifumo hiyo inasomana kiutendaji.

Amebainisha kuwa kumekuwa na changamoto kadhaa na malalamiko ya wadau kupitia utolewaji huduma kwa kuonana hivyo uwepo wa mfumo utafanya watu wasionane na kuzifanya Bandari za Tanzania na vituo vya Mipakani viwe bora katika kutoa huduma kwenye ukanda huu na hili litachagizwa na mfumo wa TANCIS.

Mapema, akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi, Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda amesem mfumo wa TANCIS ulioboreshwa unakwenda kujibu matakwa ya watumiaji wa mfumo huo na kuboresha utendaji kazi wa TRA kwa upande wa Forodha.

Mwenda amesema mfumo huo utasaidia sana kupunguza muda wa kufuatilia mizigo inayoingizwa nchini kutoka sehemu mbalimbali maana mfanyabiashara ataweza kuzifikia taasisi nyingi kwa wakati mmoja kwa kutumia mfumo bila kutoka Ofisini kwake na kuwafuata.

Amesema mfumo wa TANCIS utaleta usawa katika kulipa Kodi ambapo kila mmoja ataweza kujua anapaswa kulipa kiasi gani kwa kutumia mfumo jambo ambalo litaongeza ukusanyaji wa Kodi.

Ameongeza kuwa, mfumo wa TANCIS umegharimu zaidi ya Sh. Bilioni 100 katika ujenzi wake lakini faida zake ni kubwa sana kuliko gharama iliyotumika maana utaleta mapinduzi ya kiutendaji.

Kuhusu Tovuti mpya ya TRA Mwenda amesema Walipakodi wataweza kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na TRA na kupatiwa majibu kwa mambo watakayouliza.

Naye, Richard Kayombo ni Mkurugenzi Mkuu Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kwa Umma wa TRA amesema Tovuti mpya ya TRA iliyozinduliwa leo  imeboreshwa na kubeba vitu vingi tofauti na awali

ambapo imeunganishwa na Taasisi nyingine za Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa.

Kwa upande wake Kamishna wa Forodha, Juma Hassan Bakari amesema, mfumo wa TANCIS ulioboreshwa uliozinduliwa leo utarahisisha uondoshaji wa mizigo Bandarini na katika Viwanja vya Ndege huku ukileta mapinduzi ya kiutendaji ndani ya Forodha.

Wadau wa utumiaji wa mfumo wa TANCIS wakiongozwa na Rais wa Chama Cha Mawakala wa Forodha Edward Urio amesema washirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa mfumo huo ambao ulikuwa ndiyo kilio chao cha muda mrefu, sasa utawarahisishia ufanyaji wa kazi zao.

Related Posts