Adaiwa kuchomwa mshale chanzo mgogoro wa ardhi

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mtu mmoja kati ya wanane wanaodaiwa kumshambulia na kumpiga mshale Mussa Ngasa (40), mkazi wa Kijiji cha Nhobola kilichopo Kata ya Tagala wilayani Kishapu, wakigombea ardhi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 22, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na tukio hilo.

“Hata sisi taarifa hiyo tumeipokea jana asubuhi saa 3. Ngasa alijeruhiwa kwa kuchomwa mshale ubavuni na mkono wa kulia, na tayari tunamshikilia mtu mmoja (jina tunalihifadhi kwa sababu ya upelelezi) huku tukiwatafuta wengine wanane,” amesema Kamanda Magomi.

Amesema taarifa za awali zinadai chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi, lakini upelelezi bado unaendelea sambamba na kuwasaka watuhumiwa wengine.

Awali, akizungumza na Mwananchi, majeruhi Ngasa alieleza chanzo cha mgogoro huo hadi kufikia hatua ya kujeruhiwa kwa mshale na watu hao.

“Siku ya Jumatatu (Januari 20, 2025), nilikuwa natoka shambani saa 12 jioni, nikaona watu 8 ambao tuna mgogoro nao wa maeneo. Wakanishambulia kwa mshale.

“Lakini maeneo hayo nilikabidhiwa na mkuu wa wilaya baada ya kesi kupelekwa mahakamani na kushinda, lakini hawa watu bado wananiwinda kuniua. Mgogoro huu una muda mrefu, kama miaka mitano sasa,” amesema Ngasa.

Aidha, majeruhi huyo amesema kuwa hiyo ni mara ya nne anashambuliwa na watu hao. Mara ya kwanza walimpiga kwa panga kichwani mpaka akalazwa hospitalini.

“Hii ni mara ya nne sasa nashambuliwa, na huwa wananijeruhi halafu wanakimbia kijijini hapa. Lakini nashukuru madaktari wa hapa wananihudumia vizuri, na sasa naendelea vizuri,” amesema Ngasa.

Daktari wa kitengo cha upasuaji wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Matinde Doto, amesema majeruhi huyo anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.

“Tulimpokea Musa Ngasa akiwa katika hali mbaya jana. Alikuwa anavuja damu nyingi sana na kipande cha mshale kilikuwa kimeingia ndani hadi kwenye ini. Tulimfanyia upasuaji na kukitoa, na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri; anaweza hata kuzungumza,” amesema Dk Matinde.

Dada yake Ngasa, Magreth Ngasa, amesema ndugu yake alijeruhiwa Jumatatu na watu hao, huku akieleza kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu.

“Nilipata taarifa saa 10 usiku kuwa kaka amechomwa mshale na amepelekwa hospitali. Ila mgogoro huu naujua, haujaanza leo; ni wa muda, na hawa watu huwa wanamjeruhi mara kwa mara sababu ya eneo ambalo ni la kwake. Kesi ilishaenda mahakamani, ikaamuliwa akabidhiwe eneo hilo kwa sababu ni mmiliki halali,” amesema Magreth.

Related Posts