Dar es Salaam. Mwanasiasa maarufu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, ameshinda nafasi ya Makamu mwenyekiti wa chama hicho baada ya kupata kura 577 sawa na asilimia 57 na kumbwaga mshindani wake, Ezekia Wenje aliyepata kura 372 sawa na asilimia 37.
Heche amechukua nafasi ya Tundu Lissu aliyoingoza kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2019.
Lissu amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chadema akimshinda Freeman Mbowe
Kuanzia mwaka 2019, Heche alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wakati Lissu akiwa Makamu Mwenyekiti Bara.
Alizaliwa Julai 14, 1981. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Bulima, kisha kujiunga na Shule ya Sekondari ya Musoma Alliance ambapo alihitimu kidato cha nne mwaka 1997.
Baada ya hapo, alijiunga na Bunda Teachers’ Training College na kupata diploma ya ualimu mwaka 2004. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (St. Augustine University of Tanzania) na kuhitimu shahada ya ualimu mwaka 2006.
Katika ulingo wa siasa, Heche alichaguliwa kuwa mbunge wa Tarime Vijijini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 34. Alihudumu katika Bunge la 11 la Tanzania kuanzia Oktoba 29, 2015 hadi 2020.
Katika kipindi cha utumishi wake bungeni, Heche alijitokeza kwa kuwasilisha maswali 34 na michango 26 katika vikao vya Bunge.
Baada ya kumalizika kwa muhula wake bungeni, Heche aliibuka tena katika siasa za chama chake. Januari 2025, alitangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara katika mkutano mkuu wa chama hicho. Hii inaonyesha kuendelea kwake na kujitolea katika kuimarisha chama na kuleta mabadiliko katika siasa za Tanzania.
Januari 5, 2024, Heche alitangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti bara katika uchaguzi wa ndani wa chama uliofanyika Januari 21, 2025.
Hatua hiyo ya Heche ya kuwasilisha fomu yake ya kugombea na kuthibitisha hadharani kumuunga mkono kiongozi wa chama, Lissu, iliongeza chachu ya uchaguzi, huku Wenje, anayegombea nafasi ya makamu mwenyekiti bara, akimuunga mkono Freeman Mbowe.
Hadi hatua yake ya kugombea nafasi hiyo, Heche alikuwa mwanachama wa Kamati Kuu ya Chadema tangu mwaka 2011, alihudumu kama Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha), alikuwa Diwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na pia alihudumu kama mbunge wa Tarime Vijijini kutoka 2015 hadi 2020.
“Nilichukua hatua ya kugombea baada ya kutafakari kwa makini na baada ya wanachama wengi kunihimiza kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti,” alisema Heche alipokutana na wanahabari mjini Mwanza.
“Nataka kuongoza chama hiki kuelekea katika malengo yake ya msingi: kushinda uchaguzi, kuondoa CCM (Chama cha Mapinduzi) madarakani, na kutumia rasilimali za nchi yetu kwa mabadiliko ya watu wetu.”
“Tuna lengo la kupeleka chama hiki madarakani, kuchimba madini yetu, na kuhakikisha vijana wetu wanapata ustawi na maisha bora. Tunataka kutoa huduma bora za afya kwa watu wetu, na hilo linawezekana.”
Baadhi ya waliochukua fomu za kugombea ni Naftal Daniel, mwanachama wa muda mrefu wa Chadema ambaye amewahi kugombea ubunge wa Kwela mwaka 2015 na 2020. Naftal pia aliwahi kufanya kazi kama Ofisa Utawala wa Bavicha chini ya Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu, Deogratius Munisi.
John Pambalu, mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Bavicha ambaye alikuwa Diwani wa Butimba, Mwanza kutoka 2015 hadi 2020, aliamua kugombea ngazi ya Taifa baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Mwenyekiti wa Chadema kwa Kanda ya Victoria.
Twaha Mwaipaya, Katibu wa Uenezi wa Bavicha aliyemaliza muda wake, naye alijitokeza katika mbio hizo. Twaha ni kiongozi mashuhuri ndani ya Chadema na alikuwa mfungwa wa kisiasa mwaka 2020 baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya miezi mitatu bila kufunguliwa mashtaka.
Dorcas Fransis, mwanachama wa Chadema na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bavicha Queens, naye alijiingiza katika mbio hizo.
Patrick Ole Sosopi, mwanachama wa Chadema ambaye awali alikuwa Mwenyekiti Msaidizi wa Bavicha na aligombea nafasi ya ubunge wa Isimani mwaka 2015, pia alishiriki.
Wengine waliochukua fomu za kugombea ni Grace Kiwelu, Sina Said Manzi, Pasquina Ferdinand Lucas, William Mungai, Jenerali Kaduma, Frank Mwakajoka, Mwandishi Michael Mwangasa na Sina Said Manzi.
Hata hivyo, katika kinyang’anyiro hicho, Heche ameibuka kama mshindi kwa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa chama huku Lissu akishinda kiti cha mwenyekiti wa chama hicho kilichokuwa kinashikiliwa na Mbowe.