Dar es Salaam. Kada wa Chadema, Godbless Lema ameeleza sababu za kumtetea Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu katika kuwania uenyekiti wa chama hicho, akisema lengo lake ni kuhakikisha matakwa ya wananchi yanashinda.
Lema amesema hayo leo Jumatano Januari 22 nje ya ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kuhesabiwa kura za mwenyekiti, huku Lissu akiibuka mshindi.
Tayari Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameshatuma ujumbe katika X akimpongeza Lissu kwa ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lema aliyekuwa akishangiliwa na wafuasi wake, amesema uchaguzi huo ni fundisho.
“Ni ngumu sana mimi kuachana na Mbowe, ni tendo gumu la kisiasa, Mbowe ni kaka yangu lakini niliona Lissu anafaa zaidi kwa sasa, kwa hiyo nilipata wakati mgumu sana.
“Unaona umati wote huu, unamtaka Lissu. Naamini yeye sio malaika, lakini akifanya kazi na kamati kuu ana ujasiri wa kutosha.
“Nilitaka Lissu ashinde, nilitaka John Heche ashinde, ndio maana niliacha likizo yangu ya mapumziko nikaja hapa kuweka mguu chini,” amesema.
Amesema baada ya Lissu kumteua kuwa msimamizi wa kura zake alisikia minong’ono kuwa atamhujumu.
“Nimeona kwenye mitandao wakisema, ooh, imekuwaje mheshimiwa Tundu Lissu amemchagua Lema, haoni kuwa ni ndugu wa mwenyekiti, mimi sio wa hivyo kabisa, mini kabila langu ni Mtanzania.
“Lissu anajua integrity yangu, Mbowe anajua integrity yangu, wanajua nikipewa jambo naweza kusimamia,” amesema.
Hata hivyo, amesema uchaguzi huo umekuwa fundisho kwa vyama vingine kwa kufuata misingi ya demokrasia.
“Kwanza umeona uchaguzi ulivyoendeshwa, hakukuwa na hujuma yoyote, umeona katibu mkuu alivyosimama kwenye procedure, umeona watu walivyohakikiwa, sisemi kwamba hakukuwa na kasoro, lakini uchaguzi ujao utakuwa mzuri zaidi,” amesema.
Amesema wasiwasi wa wajumbe ulitokana na ushindani mkali uliokuwepo.
“Nafikiri uchaguzi umewafundisha vyama vingine kwamba tunaposema tunataka uchaguzi huru na wa haki maana yake nini, hata msajili wa vyama vya siasa ameona,” amesema.
Kampeni meneja wa Lissu, Gerva Lyenda amesema kitendo cha Freeman Mbowe kutuma ujumbe wa kumpongeza Lissu kwenye mtandao wa X ni ishara ya kumaliza makundi kwenye chama.
“Watu wanauliza mbona ametuma ujumbe mapema, mimi nasema mwenyekiti Mbowe ana nia njema na chama.
“Japo matokeo rasmi bado lakini kwa kura hizo zinaonyesha kila mmoja ana kundi kubwa, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kudhibiti kundi lake, kwa hiyo Freeman kutuma ujumbe maana yake analipooza kundi lake,” amesema.
Timu Mbowe watoweka ukumbini
Wakati wafuasi wa Lissu wakiwa na furaha ukumbini hapo, baadhi ya wanachama waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe walitoweka ukumbini hapo.
Hali hiyo imejitokeza wakati wa mchakato wa kura za marudio za Makamu mwenyekiti wa Zanzibar.
Matokeo ya jumla ya uchaguzi wa Chadema, yametangazwa huku Tundu Lissu akiibuka kidedea.
Katika nafasi hiyo ya mwenyekiti wa Chadema Taifa, wapiga kura waliojisajili walikuwa 1,014 huku kura zikizopigwa zikiwa 999, kura halali 996 na zilizoharibika tatu.
“Odero Odero kapata kura moja sawa na asilimia 0.1, Freeman Mbowe amepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku Lissu akipata kura 513 sawa na asilimia 51.5,” amesema Profesa Raymond Mushi mwenyekiti wa uchaguzi.
Nafasi ya Makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar ameshinda Said Mzee Said ambaye amepata kura 625 sawa na asilimia 89 kati ya kuwa 706, halali zikiwa 700 na zilizobaribika sita.
Kwa upande wa makamu mwenyekiti bara, idadi ya wapiga kura ni 1,014 kura zilizopigwa ni 1,005, halali zikiwa 998 na zilizoharibika saba.
Hivyo, Matharo Gegul alipata kura 49 asilimia 5, Ezekia Wenje (kura 372, sawa na asilimia 37 na John Heche kura 577 sawa na asilimia 57. Hivyo Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara ameshinda Heche.
Uchaguzi huo umesimamiwa na wazee wanane akiwamo Profesa Mushi na Katibu akiwa Dk Azaveli Lwaitama. Wengine ni Ruth Mollel, Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo na Azumuli Kasupa.