Lissu aendelea na Mnyika katibu mkuu, awateua Dk Nshala, Lema kamati kuu

Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu, ameanza kusuka safu za uongozi ndani ya chama hicho kwa kupendekeza majina ya Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu wawili, Bara na Zanzibar.

Lissu ameunda safu ya viongozi hao wa sekretarieti wakiongozwa na Katibu Mkuu, John Mnyika, anayeendelea kushika wadhifa huo.

Akimpendekeza Mnyika mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho jioni ya leo, Jumatano, Januari 22, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Lissu amewasilisha jina la Mnyika na manaibu wake kwa uthibitisho.

Ukumbi ukiwa umetulia, Lissu ametamka:”Amekulia kwenye chama, kijana wa chama kwelikweli, ameshika dhamana kubwa kwenye chama, ameshika dhamana kwenye Bunge. Sitawaleteeni ‘surprise’.”

“Ni mmoja wa wafanyakazi waadilifu sana wa chama chetu, na kama kulikuwa na uhitaji wa uthibitisho wa uwajibikaji wake ni John Mnyika. Sasa nawaleteeni John John Mnyika kuwa Katibu Mkuu wa chama chetu,” amesema Lissu huku ukumbi ukilipuka kwa shangwe.

Baada ya kutaja jina la Mnyika, aliuliza kama wanamthibitisha, ambapo wajumbe wote walinyoosha mikono kuonyesha ridhaa yao. Wajumbe mbalimbali walikwenda kumpa pongezi Mnyika, ambaye alianza kutumikia nafasi hiyo mwaka 2019.

Kisha, Lissu amemtaja Katibu wa Kanda ya Unguja Zanzibar, Wakili Ali Ibrahim Juma, kuwa Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar, akichukua nafasi ya Salum Mwalimu, huku Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Aman Golungwa, akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu – Bara, akichukua nafasi ya Benson Kigaila.

Juma na Golungwa walithibitishwa na Baraza Kuu kushika nafasi hizo.

Katika hatua nyingine, Lissu ametumia mamlaka yake ya kikatiba kuwateua wajumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, ambao pia walithibitishwa na Baraza hilo.

Waliochaguliwa ni Godbless Lema-  aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Rose Mayembe – aliyekuwa Mwenyekiti wa chama Mkoa wa Njombe na Dk Rugemeleza Nshalla – aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambaye ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama.

“Huyu Rose amepitishwa katika misukosuko mingi. Ndiye sababu Mkoa wa Njombe usifanye uchaguzi hadi sasa ili asiwe kiongozi. Haya ndiyo makovu tunayosema yanapaswa kutibiwa, na mtakubaliana nami anafaa kuwa mjumbe wa kamatiKuu,” amesema Lissu.

Pia, amemteua Salima Kasanzu, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza:

“Wakati wa usaili wa wagombea wa Bawacha (Baraza la Wanawake), baadhi ya wajumbe walihoji jina lake kuwepo kwenye orodha, lakini fomu yake haikuwepo. Tukafanya manuva fulani ambayo siwezi kuyasema hapa, akaitwa. Naye anafaa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu yetu.”

Mjumbe wa mwisho aliyeteuliwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Pemba, Hafidh Ali Saleh.

“Kuanzia leo, hawa watano ni wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chetu. Ninawaomba muwape maua yao. Karibuni sana katika kamati kuu,” amesema Lissu.

Baada ya kumaliza kuzungumza, alimkaribisha Salum Mwalimu, ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa miaka kumi, na mwaka 2020 alikuwa mgombea mwenza wa Lissu katika uchaguzi mkuu.

Mwalimu ametoa shukrani zake na kuwaomba radhi wote aliowakosea, huku akieleza uzoefu wake katika nafasi hiyo:

“Miaka kumi haikuwa miepesi hata kidogo. Kuacha suti na tai na kuvaa gwanda; kuacha kupanda ndege na kupanga magari na pikipiki. Miaka kumi ya Naibu Katibu Mkuu imenifundisha uvumilivu na ustahimilivu.”

Mwalimu amebainisha kwamba alishamweleza Mnyika mwaka 2021 kuwa hiyo itakuwa awamu yake ya mwisho katika nafasi hiyo, akisisitiza kuwa dhamana hiyo si ndogo.

“Leo inaweza kuwa siku ngumu kwangu, kama ilivyokuwa siku ngumu miaka kumi nyuma katika ukumbi huu, Septemba 2014, nilipokabidhiwa nafasi hii. Ninawashukuru kwa kunivumilia. Kama kuna mtu yeyote niliyemkosea, naomba radhi,” amesema Mwalimu.

Related Posts