Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imesimamisha uamuzi wa kesi inayomkabili mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbroad Slaa, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, iliyopangwa kutolewa kesho pamoja na mwenendo wa wote wa kesi hiyo.
Hatua hiyo inatokana na mashauri mawili tofauti aliyoyafungua Dk Slaa mahakamani hapo kupitia mawakili wake kutokana na kutoridhishwa na namna Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki anayesikiliza kesi hiyo inayomkabili, jinsi anavyoiendesha.
Dk Slaa amefungua mashauri hayo ya maombi Mahakama Kuu kufuatia uamuzi wa Hakimu Nyaki kuridhia mapendekezo ya upande wa mashtaka katika kesi hiyo kuwa usikilizwaji wa maombi yao ( upande wa mashtaka) kupinga Dk Slaa kupewa dhamana yasikilizwe baada ya uamuzi wa pingamizi la Dk Slaa kuhusiana na uhalali kesi hiyo.
Hivyo, kupitia kwa mawakili wake amefungua mashauri mawili ya maombi Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura.
Katika shauri la kwanza, shauri la maombi ya jinai namba 1637/2025, Dk Slaa anapinga uamuzi wa Hakimu Nyaki kutokumpa dhamana kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya Jamhuri ya kupinga dhamana yake.
Katika hati ya dharura iliyothibitishwa na Wakili Hekima Mwasipu, anaeleza kuwa, kwa mtizamo wake usikilizwaji na uamuzi wa shauri hilo inahitaji uharaka mno kwa masilahi ya haki ya mteja wao.
Amefafanua kuwa, mteja wao wamemuweka mahabusu ya Gereza la Keko bila sababu halali kwa mashtaka yanayodhaminika na kwamba mteja wao ni mgonjwa.
Amesema kuendelea kumuweka mahabusu kunamnyima haki ya kupata matibabu, hivyo kuyaweka maisha yake hatarini kubwa.
Katika hati ya maombi anaiomba Mahakama iitishe kwa mwenendo wa shauri la maombi madogo yaliyowasilishwa na Jamhuri katika Mahakama ya Kisutu, maombi namba 1015/2025 ya kupinga dhamana ya Dk Slaa kwa ukaguzi na marejeo.
Pia, anaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa Hakimu Nyaki hastahili kuendelea na kesi hiyo, kwamba amewekwa katika mahabusu ya Gereza la Keko kwa amri ya Mahakama isivyo halali.
Vilevile anaiomba Mahakama itamke kuwa, mwenendo wote wa shauri hilo tangu siku ya kwanza mpaka ulipoishia umegubikwa na nia ovu, uzembe na upendeleo unaothiri haki ya uhuru wa mteja wao moja kwa moja.
Kisha anaiomba Mahakama hiyo itoe maelekezo kwa Hakimu Nyaki kuwa, maombi ya mshtakiwa yeyote kuhusiana na uhuru wake yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanagusa haki ya msingi ya kwenda popote na haki ya kufanya kazi.
Shauri la pili, shauri la maombi ya jinai namba 1688/2025, Dk Slaa anahoji uhalali wa hati ya mashtaka katika kesi ya msingi inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu, shauri linaloungwa mkono na kiapo cha binti yake, Emiliana Wilbroad Slaa.
Katika shauri hilo, Dk Slaa anaiomba Mahakama iitishe kumbukumbu (mwenendo) wa kesi ya msingi namba 993/2025 inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu kujiridhisha na usahihi, uhalali utaratibu wa hoja zozote au amri iliyorekodiwa au kutolewa na Mahakama hiyo mwenendo huo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya dharura Wakili Madeleka anaeleza kuwa wao ameshtakiwa kwa mashtaka yasiyokuwa na msingi na kama hayataamuriwa kwa wakati, ataendelea kuathirika kwa kukosa uhuru isivyo halali kwa kiasi kisichoweza kufidiwa.
Naye binti yake, Emiliana, ameeleza kuwa mwombaji (Dk Slaa ) anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Kisutu wakati upelelezi wa kesi hiyo ukiwa haujakamilika na kwamba anaendelea kupitia hasara ya kukosa uhuru wake kwa kiwango kisichoweza kufidiwa.
Mashauri hayo yote yametanwa leo mbele ya Jaji Anold Kirekiano na upande wa wajibu maombi ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa na kuomba siku sita kuwasilisha kiapo kinzani.
Maombi hayo yamepingwa na jopo la mawakili wa Dk Slaa, likiongozwa na Madeleka, akisaidiana na Mwasipu na Edson Kilatu, kuwa siku sita nyingi kulingana na asili ya maombi kwa kuwa mteja wao ambaye ni mgonjwa anaendelea kuteseka mahabusu.
Jaji Kirekiano katika uamuzi wake amewataka wajibu maombi kuwasilisha kiapo kinzani kwa mashauri yote mawili kesho, Alhamisi Januari 23, 2025 saa tatu, huku akipanga kusikiliza shauri la maombi yanayohusiana na dhamana ya Dk Slaa, kesho saa 8:00 mchana.
“Ninaelekeza pia mwombaji (Dk Slaa) kesho wakati wa kusikiliza shauri lake awepo. Shauri litasikilizwa saa 8:00 mchana na shauri la Kisutu litasimama kama ilivyo utaratibu maana pia tutaita mwenendo wake japo kwa kidijitali,” amesema Jaji Kirekiano.
Kwa maana hiyo hata uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na mawakili wa Dk Slaa wakipinga uhalali wa kesi hiyo kufunguliwa ambao Mahakama ya Kisutu ilikuwa imepanga kutoa kesho Alhamisi, Januari 23, 2025, nao hautasomwa tena.
Kuhusiana na shauri la uhalali wa hati ya mashtaka, Jaji Kirekiano amesema litasikilizwa keshokutwa, Ijumaa Januari 24, 2025.
Dk Slaa alipandishwa kizimbani mahakamani hapo, Januari 10, 2025 na kusomewa shtaka moja la kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa X zamani Twitter, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, Dk Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk Slaa anadaiwa siku hiyo ya tukio kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka: “Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya,…na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia, anadaiwa aliandika katika akaunti maneno yalisomeka: “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe.”
Baada ya kusomewa shtaka hilo, upande wa mashtaka ulieleza kuwa, upelelezi haujakamilika lakini waendesha mashtaka wakasema wamewasilisha maombi ya kupinga dhamana yake.
Hata hivyo, siku hiyo jopo la mawakili wa Dk Slaa nalo likaibua pingamizi dhidi ya uhalali wa kesi hiyo wakidai ni batili na haipaswi kuwepo mahakamani kwa kuwa imefunguliwa kinyume na masharti ya sheria.
Wanadai kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 131A (1) na (4), shtaka linalomkabili mteja wao ni miongoni mwa mashtaka ambayo hayapaswi kufunguliwa mahakamani kabla upelelezi haujakamilika.
Upande wa mashtaka ulipinga hoja hiyo wakidai kuwa shtaka hilo kwa tafsiri yake liko katika kundi la mashtaka yanayoweza kufunguliwa mahakamani hata kabla upelelezi haujakamilika.
Mahakama ilielekeza kusikilizwa maombi ya Jamhuri pamoja na pingamizi la Dk Slaa Januari 17, 2025.
Siku hiyo baada ya kusikiliza pingamizi hilo na Mahakama ikapanga kulitolea uamuzi Januari 23, 2025, huku waendesha mashtaka wakitoa hoja ya kuahirisha usikilizwaji wa shauri la maombi ya kupinga dhamana kusubiri kwanza uamuzi wa Mahakama kuhusiana na pingamizi la Dk Slaa.
Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa Dk Slaa wakitaka na maombi hayo yasikilizwe siku hiyo hiyo kama walivyokuwa wameshakubaliana ili kuokoa muda.
Hata hivyo, Hakimu Nyaki alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka akaamua kuwa maombi ya Jamhuri kupinga dhamana yatasikilizwa baada ya kutoa uamuzi wa pingamizi la Dk Slaa kuhusu uhalali wa kesi hiyo, uamuzi ambao ndio umemfanya Dk Slaa kwenda Mahakama Kuu.