Medo amvalisha mabomu Mpole | Mwanaspoti

KOCHA wa Kagera Sugar, Melis Medo ameonyesha imani kubwa kwa mshambuliaji mpya, George Mpole, akisema  ana uwezo wa kufanya mambo makubwa na kuwa msaada katika juhudi zao za kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka Ligi Kuu Bara.

Medo ameliambia Mwanaspoti kwamba Mpole atakuwa silaha muhimu katika timu hiyo hasa katika duru la pili la Ligi Kuu Bara ambapo Kagera Sugar inakutana na changamoto kubwa ya kupigania kubaki kwenye ligi.

Mpole ambaye amejiunga na Kagera Sugar akitokea Pamba Jiji katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15 ni mchezaji mwenye rekodi nzuri akiwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2021/22 baada ya kufunga mabao 17 akimzidi Fiston Mayele aliyekuwa Yanga aliyeyetupia 16.

Medo alisema anaamini uzoefu wa Mpole utaongeza nguvu katika timu yake ambayo inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11.

“George Mpole ni mshambuliaji ambaye ana uzoefu mkubwa na amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara. Ana uwezo wa kuleta madhara makubwa katika maeneo muhimu uwanjani. Hii ni silaha muhimu kwa timu yetu kwani tunahitaji mchezaji ambaye anaweza kuleta ubunifu mbele na kumalizia nafasi za kufunga,” alisema.

Kocha huyo aliongeza kwamba Mpole ni mchezaji ambaye ametua kwao kwenye kipindi muhimu.

“Tunahitaji wachezaji kama yeye ambao hawana hofu wanapambana hadi dakika ya mwisho na wanajua jinsi ya kutumia nafasi. Huu ndio ubora tunaohitaji ili kujinasua katika nafasi tuliyopo sasa,” alisisitiza.

Mbali na Mpole, Kagera Sugar pia imetambulisha nyota mwingine katika dirisha lililofungwa la usajili ambaye ni kipa Ahmed Feruzi aliyejiunga kwa mkopo akitokea Simba, na Medo anaamini kuwa kuongezwa kwa kipa huyo kutaimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Related Posts