NYOTA mpya wa Namungo, Issa Abushehe ‘Messi’, amesema kitendo cha kujiunga na kikosi hicho anaamini itakuwa njia nzuri kwake ya kumrejesha katika ubora wake, huku akiweka wazi sababu kubwa za kuamini hivyo ni uwepo wa kocha, Juma Mgunda.
Winga huyo amejiunga na kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, baada ya kuvunja mkataba wake wa miezi sita uliobaki na KVZ ya Zanzibar, aliyojiunga nayo msimu huu kufuatia kuachana na Biashara United ya Mara inayoshiriki Ligi ya Championship.
“Wengi wao wanatamani kumuona yule Messi waliyekuwa wanamfahamu tangu mwanzoni, kwangu ni changamoto ya kuhakikisha naingia kwanza na kuanzia hapo itakuwa ni njia nzuri ya kunirudisha tena katika hali ya kujiamini zaidi.”
Abushehe alisema kitendo cha kufanya kazi na Mgunda kinamfanya kuamini atarudi katika makali yake ya mwanzoni kutokana na ushirikiano wao mzuri aliokuwa naye, tangu akikichezea kikosi cha ‘Wagosi wa Kaya’, Coastal Union.
“Kwanza ni zaidi ya kocha kwa maana ni mzazi, hata ujio wangu hapa yeye ndio sababu kubwa.”
“Bado nina kipaji kikubwa na ninaweza kuisaidia Namungo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, nipo tayari hapa kwa changamoto mpya.”
Nyota huyo aliwahi kufanya kazi na Mgunda wakati akiwa Coastal Union na kuonyesha kiwango kizuri kilichompa nafasi ya kujiunga na Al Mokawloon Al Arab inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, aliyojiunga nayo Septemba 19, 2022 hadi Julai 20, 2023.