‘Miamala kidijitali ni njia salama’

Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Wateja wa Rejareja kutoka Benki ya Absa, Ndabu Swere amesema malipo ya kidijitali ni njia inayowezesha kufanya miamala kwa usalama zaidi.

Amesema walipoanzisha huduma ya miamala kwa njia ya kidijitali, asilimia 70 pekee ya wateja wao ndiyo walikuwa wanatumia huduma hiyo, kwa sasa watumiaji wa huduma hiyo wamefikia asilimia 90.

Amesema hayo leo Jumatano Januari 22, 2025 wakati wa hafla ya kumkabidhi zawadi ya gari mshindi wa tatu wa shindano la ‘spend and win’ Amalia Shio aliyeshinda kwa kufanya miamala mingi ya kidijitali.

“Kama mnavyojua, huduma za kibenki zipo za namna tofauti, unaweza kufanya huduma ndani ya tawi la benki na unaweza kutumia miamala ya kidijitali, kwa sasa huduma ya kidijitali imefanikiwa zaidi, jambo linaloashiria kufanikiwa kwa kampeni ya Serikali katika kuhamasisha matumizi ya miamala kidijitali na kukuza kiuchumi,” amesema.

 Amesema wanahakikisha, wanatimiza azma ya Serikali katika kufikisha huduma mpaka sehemu zisizokuwa na tawi la benki.

“Kupitia huduma ya kidijitali malipo yatafanyika bila vikwazo vyovyote na wakati wowote,”ameeleza Swere.

Aidha, mshindi wa tatu wa shindano hilo, Shio amesema huduma ya miamala kidijitali hapa nchini imeendelea kukua na kumwezesha kutumia huduma hiyo akiwa nje ya nchi.

“Matumizi ya miamala kidigitali, inatuondoa katika wasiwasi wa kiusalama, hasa unapokuwa na pesa mkononi, hata kwa upande wa makato, yako chini zaidi unapofanya miamala hiyo, ukiwa nje ya nchi,” amesema.

Related Posts