SIKU chache baada ya maboresho ya ratiba, kocha mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Mexime amekiri mwezi ujao wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea ni dume kwelikweli kutokana na bandika bandua ya mechi huku akiweka wazi kuwa wataendelea walipoishia.
Mchezo wa mwisho Dodoma Jiji kabla ya ligi kusimama kupisha Mapinduzi Cup 2025 na fainali za CHAN 2024 zilizoahirishwa hadi Agosti, timu hiyo iliishinda mabao 3-1 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Jamhuri na sasa itaanza ngwe ya mwisho pia nyumbani dhidi ya Pamba Jiji siku ya Februari 5.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mexime alisema wana mechi sita ndani ya mwezi mmoja zote ni ngumu kutokana na kila timu kupambana kuto kuangusha pointi katika mzunguko wa lala salama hivyo ana kazi ngumu ya kufanya kuhakikisha timu yake inakusanya pointi zote ili kuibakisha timu Ligi Kuu.
“Februari ni mwezi dume kweli kweli ukizingatia wachezaji walikuwa mapumzikoni nafanya kazi kuwajenga kiushindani ikiwa ni pamoja na kujenga utimamu wa mwili.”
“Hakuna mchezo rahisi nyumbani wala ugenini, tunatakiwa kujipanga kiushindani na kumuheshimu mpinzani wetu bila kujali ubora tulionao, natarajia mwendelezo mzuri na wachezaji tuliowaongeza kikosini watakuwa na chachu kutokana na uzoefu walionao.”
Mexime alisema usajili uliofanywa kwa timu yake umeendana na mahitaji na anatarajia pia kukutana na maingizo mapya kutoka kwa wapinzani wake hivyo kujiandaa vizuri ndio kutakakompa matokeo mazuri na kumuhakikishia nafasi ya kucheza ligi msimu ujao akisisitiza kila timu ina nafasi kutegemea na namna itakavyochanga karata zake vizuri.
Mechi sita za Dodoma Jiji ndani ya Februari ni dhidi ya Pamba Jiji, itakuwa ugenini dhidi ya Namungo na Simba kisha itarudi nyumbani kuzipokea Tanzania Prisons na Fountain Gate, kisha kufunga mwezi ugenini dhidi ya Tabora United mechi itakayopigwa Februari 28 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.