NIKWAMBIE MAMA: Polisi wetu walionaswa kwa rushwa ni kama tone

Siku moja Rais mstaafu wa awamu ya pili, marehemu mzee Ali Hassan Mwinyi alipokuwa akizungumza na wananchi kuhusu janga la Ukimwi, alijikuta akitamka kwa huzuni kubwa: “Jamani gonjwa hili limekaa kwenye sehemu mbaya…” Binafsi nilimwelewa kuwa gonjwa limekaa kwenye eneo lisiloweza kukwepeka na kiumbe hai. Mfano hewa yote ingegeuka sumu, ni wazi hakuna kiumbe ambaye angenusurika.

Kauli hii naiona kwenye rushwa. Mdudu rushwa anaonekana kukaa sehemu mbaya kama Ukimwi. Ametega kwenye mahitaji makuu ambayo kila mwananchi ni lazima ayapate. Binadamu hawezi kuishi bila afya, haki na ulinzi na usalama wa maisha yake. Sekta zinazosimamia tunu hizo zina nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu. Lakini sekta hizi ndizo zinazotajwa kuwa vinara wa kudai na kupokea rushwa kutoka kwa wahitaji.

Mtu anapopambania mahitaji yake muhimu kama afya na haki, anakuwa radhi kupoteza chochote anachomiliki. Anapata utayari wa kupoteza gari, nyumba, shamba au vito ili mradi apate kile anachokithamini zaidi ya hivyo. Lakini kwa upande wa pili, wale ambao wangempatia haki yake wanatumia nafasi hiyo kumnyang’anya kila alichonacho. Rushwa haichukuliwi kwa shida, bali tamaa.

Tamaa haina kikomo, anayepata kumi leo atatamani mia kesho. Tumefikia mahala ambapo vinara wa mlungula wanachukulia kuwa ni haki yao kudai na kupewa rushwa. Hali hii inawalazimisha raia wema kujiingiza wenyewe kwenye mfumo, kwani wanatambua hawawezi kuhudumiwa vinginevyo. Watafanyaje wakati watu wa mamlaka wanadai? Wakati mwingine inawapasa kuziogopa mamlaka, kwani ndizo zilizokamatia mpini.

Mapambano dhidi ya rushwa yalianza tangu kuumbwa kwa dunia. Kila jamii inazo aina zake za rushwa. Na kwa kuwa kila ugonjwa haukosi dawa, ndivyo kila jamii inavyotafuta namna ya kupambana nayo. Lakini kwa kuwa rushwa ni haramu inayotendwa gizani, wala rushwa huwa makini sana. Mhalifu huwa makini sana na macho ya haki. Kwa hiyo wamekuwa wakihama kuukwepa mwanga kila ulipowasogelea.

Wakati fulani vita ilikuwa kubwa ikawalazimisha waumini wa rushwa kubuni njia tofauti za kukwepa macho ya Serikali. Kwanza dereva aliyekamatwa na kosa aliamriwa kumnunulia askari gazeti la siku hiyo.

Kwenye moja ya kurasa za gazeti ndimo ulifutikwa mlungula. Waliposhtukiwa askari sasa wakawatumia mafundi viatu na viduka vya Mangi kama mawakala wao. Dereva aliyepigwa mkono alijua apeleke wapi shilingi elfu tano mpaka kumi kulingana na kosa lake.

Lakini wakati huu rushwa imegeuzwa kuwa haki. Ile video iliyowanasa askari wa usalama barabarani inathibitisha maneno yangu. Wamenaswa wakipokea rushwa kutoka kwa madereva wa daladala bila woga wala tahadhari. Tena basi walikuwa wakihama kutoka basi moja hadi lingine bila kuogopa abiria waliokuwa wakiwatazama. Hiki ni kiwango cha juu zaidi cha uhalalishaji wa rushwa hapa nchini.

Hii ni sehemu moja tu ambayo bila shaka sio mbali kutoka katikati ya mji wa Dar es Salaam. Hujasogea nje ya mji au kule mkoani, wala hujafika huko maporini kwenye mabasi na malori ya safari ndefu. Sasa kama katikati ya mji askari wanawanga mchana kweupe kama vile, je, hali ikoje huko maporini usiku wa manane? Waswahili husema; “Akuwangiaye mchana usiku atakunyonga”.

Hawa askari wametuonesha jeuri kubwa sana. Kwa akili ya kawaida tunajiuliza ni mtu gani anayeweza kuhatarisha kazi yake kwa kiwango kile? Yaani hata woga kwamba bosi anaweza kupita ghafla na kumkuta kwenye harakati zile za kuchangisha!

Au hata kuogopa kusemewa na wabaya wake kwamba ameonekana akifanya ukafiri barabarani? Hakika askari hawa wanafaa kukabiliana na gaidi aliyefungasha mabomu.

Kujiamini kwao kunatutia shaka kwamba baadhi ya wakubwa wao wanaufahamu mchezo. Katika miaka ya tisini na kuendelea, iliwahi kuzuka kashfa ya askari wa doria kupangiwa kurudisha fedha kwa wakubwa wao. Viwango vilikuwa tofauti kulingana na vyombo walivyopewa; aidha pikipiki au gari (gofu).

Kashfa hii ilifuata baada ya ile ya askari kuhonga ili wapangiwe usalama barabarani kwenye maokoto ya fasta.

Maneno yote haya yamekuwa yakizungumzwa kwa muda mrefu. Ni wajibu wa Jeshi letu kuyafuta vichwani mwa wananchi na kuwaaminisha vinginevyo, lakini mara nyingi wananchi hawakupata majibu waliyoyategemea kila mara walipokuwa na maswali juu ya chombo hiki nyeti.

Wengi bado wana shaka pale Jeshi la Polisi linapohusishwa na tuhuma, kisha Jeshi lenyewe likaamua kujichunguza.

Uzuri wa mitandao ya kijamii ni kutumika na watu wanaodhaniwa kuwa hawana akili, wenye akili finyu na wenye akili mbovu. Laiti Polisi wenyewe ndio wangeanza kuipata video ile usingeliiona kamwe.

Wangezingatia mambo mengi kama walinzi wa haki za binadamu na wasimamizi wa itifaki. Mpango wa kulisafisha Jeshi hilo ungewaongoza kutafutana na kumalizana kimyakimya. Lakini jioni hatua chache kutoka hapo makusanyo yangeendelea.

Kwenye tukio hili tunategemea Serikali kuja na jambo kubwa zaidi. Vinginevyo tutakuwa tunawahamasisha walinzi wetu wageuke wahalifu.

Mlinzi wa haki za raia akiamua kuzisigina anakuwa hatari zaidi ya mhalifu nguli. Kama mjini rushwa inachukuliwa vile mchana kweupe, basi itachukuliwa kwa mitutu usiku huko maporini.

Related Posts