Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emanuel Tutuba amesema noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na yeye, toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari mosi, 2025.
Tutuba amesema hayo leo Jumatano, Januari 22, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akimkabidhi Dk Mwigulu noti za Sh10,000, Sh5,000, Sh2,000 na Sh1,000
kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Mheshimiwa waziri, ninayofuraha kukujulisha zoezi (kazi) letu la uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali,” amesema Tutuba.
Amesema noti hizo zitatumika sambamba na noti zilizopo hivi sasa.
Amesema noti hizo zina mwonekano wa zinazotumika hivi sasa zilizotolewa mwaka 2010, ikiwamo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Awali, noti hizo zilizokuwa na saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango na saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Profesa Florens Luoga, zimebadilishwa na kuwekwa saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Emmanuel Tutuba.
Dk Mwigulu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Tutuba kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi.