JUMLA ya visima 9 kati ya 10 vya maji safi na salama vimechimbwa Wilayani Lindi na Wizara ya maji kupitia kwa wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (Ruwasa)Wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa programu ya uchimbaji visima 900 kwa nchi nzima.
Programu hiyo inalenga kuhakikisha zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa maeneo ya vijijini wanapata huduma ya maji safi na kutimiza adhma ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Lindi Mhandisi Athanas Lume Patrick amesema visima hivyo vinavyogharimukiasi cha shilingi Milioni 600 ,visima 4 vimechimbwa jimbo la mchinga vitakavyohudumia wakazi 2604 huku visima 5 ambayo vimechimbwa kwa halmashauri ya Mtama vitawahudumia takribani wakazi 4709 na hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kutoka 76 hadi 82.4
Ametaja maeneo ambayo vimechimbwa kuwa ni pamoja na Dimba,Ruchemi,Kitongoji cha Runyu,Makangala,Kitongoji cha Likonde kwa upande wa jimbo la Mchinga wakati jimbo la Mtama vikichimbwa katika maeneo ya Vijiji vya Utimbe, Madingo ,Milamba,Litingi na Kitongoji cha Mbindo (Nahukahuka A).
Baadhi ya wananchi kutoka katika kijiji cha Dimba kata ya Kilolambwani akiwemo Saidi Abdalah,mwenyekiti wa Kijiji hicho na Desteria Joseph Chilumba wamelalamikia kutembea umbali mrefu kufuata hudua ya maji kwenye vyanzo vya asili ambavyo wamedai wanashirikiana na wanyama kama Tumbili na kwamba uchimbaji wa visima hivyo unakwenda kuondoa adha hiyo.
Akizungumza Januari 21 wakati wa ziara maalum ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva ametoa wiki 2 kwa wakala huo kukamilisha ujenzi wa miundombinu kama vioski katika visima ambavyo ujenzi wake unaendelea ili wananchi wa maeneo ambayo hawakufikiwa na miradi mikubwa waanze kupata huduma ya maji safi,salama na yenye kuwatosheleza.
Amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 12.79 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 13 ikiwemo miradi 5 ya uchimbaji wa visima kwa Jimbo la Mtama na Bilioni 5.71 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 17 ndani yake ya uchimbaji wa visima.
“Kutokana na uhitaji mkubwa wa maji,visima vinachimbwa ili wananchi warahisishiwe kupata huduma, nawaomba sana Ruwasa nitakaporudi tena nikute maji Mwamwamwa!”.Alisema Mwanziva.