KIUNGO Nassor Kapama amezua maswali baada ya kuonekana akijifua na Fountain Gate kisha ghafla kurudi chaka lake la zamani wa Kagera Sugar iliyomtambulisha juzi, lakini Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Thabit Kandoro afunguka sababu iliyomrudisha.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba ni miongoni mwa wachezaji wakongwe wa klabu hiyo, lakini katika kipindi cha dirisha dogo alionekana na Fountain Gate akifanya mazoezi.
Mwanaspoti linafahamu, kiungo huyo alishabeba virago vyake na kutimkia Fountain, huku kocha wa kikosi hicho Mellis Meddo akitoa ruhusa ya kuondoka kwake.
“Kocha alishaona kuondoka kwake hakuwezi kuleta madhara kwenye hesabu zake ndio maana akabariki kuondoka kwa Kapama lakini mabosi wamegoma,” taarifa ya awali kutoka ndani ya timu hiyo.
Baada ya taarifa hiyo Mwanaspoti iliamua kuutafuta uongozi wa Kagersa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Thabit Kandoro alisema wameona umuhimu wa kiungo huyo bado unahitajika ndio maana wamemrudisha.
“Kama viongozi wa klabu tumeona umuhimu wa kiungo huyo mzoefu, ambaye anaweza kuziba maeneo mengi katika kikosi hiki ndio maana tumesitisha safari ya kuondoka kwake,” alisema Kandoro.
Kapama bado ana mkataba na Kagera ambao utamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akiwa na rekodi ya kuwa mchezaji bora katika mechi dhidi ya Yanga.