Unguja. Wakati baadhi ya wananchi na wafanyabiashara kisiwani hapa wakilalamikia katikakatika ya umeme, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaib Hassan Kaduara, amesema inasababishwa na ongezeko la watumiaji na wawekezaji nchini.
Hata hivyo, amesema Serikali inatarajia kuleta msongo mpya wa umeme wenye megawati 220 kutoka Tanzania Bara mapema mwaka huu.
“Unaotumika sasa una megawati 132, umezidiwa kwa sababu watumiaji wa huduma za nishati wameongezeka, hasa wawekezaji. Hivyo, transfoma nyingi zinazidiwa na hata njia za kusambaza umeme huo pia zimezidiwa, ndiyo maana hali hii inatokea,” amesema Waziri Kaduara.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano, Januari 22, 2025, Waziri Kaduara amesema Serikali pia inaliongezea nguvu za kifedha Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) ili lifanye maboresho ya miundombinu ya umeme yote iliyochakaa.
“Kile kijumba ambacho kimefanyiwa harusi kikawa kinamtosha baba na mama, kwa sasa kimeshapata watoto wengi. Hakitoshi tena, ndiyo maana Serikali inaelekea kuboresha miundombinu ya umeme kwa sababu wananchi tumeshaongezeka,” amesema Kaduara.
Hivyo, amewaomba wananchi wa Zanzibar wawe wavumilivu katika kipindi hiki kifupi ambacho Zeco linashughulikia tatizo hilo, hususan wa Mkoa wa Kaskazini ambako kuna shida zaidi.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 22, 2025, baadhi ya wananchi wameeleza kukerwa na tabia ya kukatika kwa umeme mara kwa mara bila taarifa, hali inayosababisha uharibifu wa bidhaa zao za biashara zikiwamo samaki, juisi na matunda.
“Ni vizuri basi wangekuwa wanatupa taarifa kabla hawajaukata ili tujipange tunahifadhi vipi bidhaa zetu. Hii ni biashara, ni mtaji. Zikiharibika tumeua biashara,” amesema Habiba Salum, mkazi wa Mahonda.
Amesema awali shirika lilikuwa linatoa taarifa kabla ya kukata umeme, lakini siku hizi hali hiyo haipo; umeme unakatika bila mpangilio.
“Sisi hapa hatuna siku maalumu ya kuzimiwa umeme; ni kila siku, hususan nyakati za usiku. Kwa kweli tunaumia na joto. Shirika litoe taarifa,” amesema Habiba.
Naye Fatma Said Juma, mkazi wa Mangapwani, amesema tatizo hilo linachangia ongezeko la vitendo vya uhalifu, ikiwemo wizi, kwa sababu giza linawapa wahalifu fursa ya kujificha.
“Inapofika usiku na umeme umekatika, huwezi kulala vizuri. Akili yako inawaza kuwa kuna mtu anaweza kukuvamia. Hali hii inatuweka kwenye hofu kubwa,” amesema.
Kwa upande mwingine, Khatabi Khamis, mkazi wa Mangapwani, amesema: “Mimi nafanya biashara ya samaki. Wanapobaki, lazima niweke kwenye jokofu, lakini hali hii ya umeme kukatikakatika inaleta hasara. Mara nyingi samaki wanaharibika.”
Naye Abdallah Rajabu, mkazi wa Mfenesini, ameelezea changamoto ya kukatika kwa umeme inawaathiri zaidi wafanyabiashara wadogo, ambao bidhaa zao haziwezi kuhifadhiwa bila umeme.
Ametoa wito kwa Shirika la Umeme kurudisha utaratibu wa kutoa taarifa mapema pindi wanapolazimika kukata umeme, ili kuwasaidia kujipanga.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) ilitangaza mabadiliko ya umeme, ambapo sababu kubwa ilitajwa kuwa ni ongezeko la mahitaji, kama ilivyoombwa na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).