Simba yapasua mtu 11-0, Mnunka arejea na mbili

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Simba Queens leo jioni wameichakaza Mlandizi Queens kwa mabao 11-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Jentrix Shikangwa alifunga mabao manne, Asha Djafar alitupia hat-trick, Aisha Mnunka aliweka kambani mawili wakati Precious Christopher na Ruth Ingosi kila moja alifunga mara moja.

Huu ni mchezo wa pili timu hizo zimekutana baada ya ule wa mzungukio wa kwanza ambao Simba iliondoka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni.

Kivutio kikubwa kwenye mchezo huo kilikuwa mshambuliaji wa Simba, Mnunka ambaye alionyesha kiwango bora kwenye mchezo wake wa kwanza tangu arejee katika timu hiyo ambayo aliikacha bila ya kuaga katika mazingira ya kutatanisha.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita aliibuka kinara wa ufungaji alipotupia mabao 21, alikuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitano, alipoondoka klabuni kiutata huku ripoti zikidai kuna klabu ilimtorosha kwa nia ya kumsajili, licha ya kwamba alikuwa bado ana mkataba na Simba kabla ya kurejea baada ya vikao vya mwafaka katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka (TFF).

Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kusalia kileleni na pointi 28 huku JKT Queens ikiwa nafasi ya pili na pointi 23 na Mashujaa ikisalia nafasi ya tatu na pointi 18.

Ukiachana na matokeo hayo kuna vita ya wafungaji kwa Shikangwa ambaye ana mabao 14 kwenye mechi 10 nyuma ya Stumai Abdallah wa JKT mwenye nayo 10 na wote wakifunga hat-trick kwenye mchezo wa duru la pili.

Related Posts