Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kusitisha misaada ya maendeleo nje ya Marekani kwa siku 90, pamoja na azma ya kujitoa kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), umeikuta Tanzania ikiwa imejitayarisha kwa changamoto hizo.
Trump, ambaye Jumatatu wiki hii ameapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, alisaini amri za kiutendaji takriban 78, ikiwemo hatua ya Marekani kujitoa WHO na kusimamisha misaada ya maendeleo nje ya Marekani kwa muda wa siku 90.
Aidha, misaada ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) imeathirika, huku taarifa zikidai kuwa baadhi ya wafanyakazi wake ambao ni raia wa Marekani wanaweza kurejeshwa nyumbani.
Kwa muda mrefu, misaada kutoka USAID na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) imekuwa na mchango mkubwa katika sekta za afya, elimu, na maendeleo nchini Tanzania.
Kwa mwaka 2023 pekee, USAID ilitoa zaidi ya dola milioni 400 kwa ajili ya kuimarisha sekta mbalimbali nchini.
Licha ya uamuzi wa Trump, Tanzania tayari imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuelekea kujitegemea katika miradi ya afya, hususan katika mapambano dhidi ya janga la Ukimwi.
Hatua hizo zilijidhihirisha kupitia uzinduzi wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NMSF V) uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Desemba mosi, 2022, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mkoani Lindi.
Katika hotuba yake, Rais Samia aliwataka viongozi wa sekta mbalimbali, wakiwemo mawaziri 15 waliokuwa wamehudhuria, kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo.
Nchi ilifikia hatua hiyo wakati wafadhili wakianza kupunguza mchango wao, huku asilimia 94 ya afua za Ukimwi nchini zikitegemea wahisani.
Serikali ya Tanzania kupitia sheria iliyopitishwa mwaka 2015, iliunda Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF), ambao umekuwa ukichangiwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali.
Kwa mujibu wa ripoti ya makusanyo ya fedha kwenye mfuko wa ATF kwa mwaka 2021-2023, makusanyo yameongezeka kutoka Sh1.06 bilioni mwaka 2021 hadi Sh2.04 bilioni mwaka 2023.
Hata hivyo, changamoto ya kutosha kwa fedha bado ni kikwazo kwa utekelezaji kamili wa miradi mbalimbali ya afya.
Akizungumza leo Jumatano Januari 22, 2025, na Mwananchi kwa simu kuzungumzia namna Serikali ilivyojipanga kufuatia uamuzi wa Trump na iwapo suala hilo litakuwa na athari kwa huduma za afya hasa kwa dawa za miradi misonge, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, aliyekuwa kwenye kikao amesema;
“Suala hili linaangaliwa lakini tunasubiri kupata taarifa kamili.” amesema waziri huyo akiahidi kutoa ufafanuzi zaidi akimaliza kikao.
Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi, amesema kutokana na uamuzi Rais huyo wa Marekani, changamoto hasa itakuwa kwenye mahitaji ya lazima hasa ugharamiaji wa afya katika baadhi ya dawa na matibabu ya miradi misonge.
“Zaidi ya asilimia 90 ya rasilimali zinazotokana na Ukimwi na VVU zinatoka nje, Pepfar inachangia asilimia 40 na kuna mashirika mengine yanachangia ikiwemo WHO, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) na Global Fund, na huku kote Marekani inaweka fedha nyingi, kwa hiyo unaona tutakavyoyumba,” amesema.
Hata hivyo, Dk Lilian amesema Tanzania inapaswa kujiandaa vilivyo, ingawaje ilishaanza kuweka mikakati mbalimbali, ina uwezo wa kuchangia asilimia sita pekee kupitia Bajeti ya Wizara ya Afya na Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF).
Amesema kuna huduma zitakwenda kuathirika moja kwa moja kutokana na sera za sasa za Marekani ikiwamo miradi ya utoaji mimba salama na uzazi wa mpango.
“Sheria husema kama unapokea fedha unatakiwa kufanya hiki na kile na nini hutakiwi kufanya. Kwa sera za sasa za Marekani, kuna baadhi ya mambo itabidi tuache kuyafanya, hivyo tutafanya kulingana na matakwa yao na si uhitaji wa jamii,” amesema Dk Lilian.
Hata hivyo, ametoa angalizo kuwa kuna makundi yanayosaidiwa kujikinga, hivyo sera za sasa zitayatenga na kama hakutakuwa na fedha za kuyatazama makundi hayo, huenda maambukizi ya VVU yakaongezeka nchini.
Kwa upande wake, mshauri na mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati, amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuwekeza katika rasilimali za ndani ili kujitegemea.
“Dawa na matibabu ya VVU tunategemea sana misaada kutoka Marekani. Kuyumba kwa msaada huu kunapaswa kuwa chachu ya sisi kama nchi kujitegemea zaidi katika afya na elimu.
“Mfuko wa ATF ni muhimu sana, lakini hatujautumia ipasavyo. Ni wakati sasa kuweka mkazo katika mfuko huu na kushawishi mataifa mengine kama China kuchangia zaidi,” amesema Dk Osati.
Naye Veronica Lyimo kutoka Jukwaa la Wanawake Wanaoishi na VVU, amesema hoja ya Trump inalenga kuzitaka nchi zinazotegemea misaada kujenga mifumo endelevu ya kujitegemea.
Tanzania tayari imepiga hatua kupitia mkakati wa kuhakikisha uendelevu katika masuala ya Ukimwi na afya kwa ujumla.
Miradi ya Marekani nchini
Mpaka mwaka 2025, miradi ya USAID Tanzania inahusisha sekta za kilimo, demokrasia, haki za binadamu, ukuaji wa uchumi, elimu, mazingira, jinsia, vijana, na afya.
Kwa mwaka 2023 pekee, USAID ilitoa zaidi ya dola milioni 400 za Mrekani (Sh993.2 bilioni) kusaidia sekta hizo.
Hata hivyo, uamuzi wa Marekani kujitoa WHO na kusimamisha misaada unasisitiza hitaji la Tanzania kuimarisha rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa takwimu, mwathirika wa VVU anayepokea dawa za kufubaza makali ya ugonjwa hutumia dawa zenye thamani ya dola 58.20 kwa mwezi.
Kwa idadi ya waathirika zaidi ya milioni 1.5 nchini, gharama za dawa pekee ni zaidi ya Sh204 bilioni kwa mwezi mmoja.
Hali hii inadhihirisha umuhimu wa Tanzania kujipanga kikamilifu ili kukidhi mahitaji ya afya ya wananchi wake.