‘Tumemaliza kazi, tumebakiza kushindana na vyama vingine’

Unguja. Mgombea mteule wa urais wa Zanzibar wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wamemaliza uchaguzi wa chama wakiwa salama, hivyo kazi iliyobaki ni kujipanga  kushindana na viongozi wengine kutoka vyama vingine.

Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, amewataka wananchi kujiandikisha kupigakura na kujitokeza kwa wingi  katika uchaguzi mkuu kupiga kura.

Amezungumza hayo katika hafla ya mapokezi ya mgombea mteule wa urais wa CCM Zanzibar akitokea Dodoma baada ya kumaliza mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 18 na 19  na kuwapitisha Dk Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu.

“Ndugu zangu kwenye chama kazi tumemaliza, sasa kazi iliyobaki ni kujipanga kwenda kushindana na viongozi kutoka vyama vingine,” amesema.

Katika kulifanikisha hilo, Dk Mwinyi amewataka wafuasi hao na wananchi kwa jumla kujitokeza kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ambalo kwa awamu ya pili na mwisho itaanza Februari mosi na kumalizika Machi 17, mwaka huu.

“Niwaombe tujitokeze kujiandikisha kwa wingi, lakini wanaCCM huwa tuna tabia tunaweza kujiandikisha kwa wingi lakini hatujitokezi kupiga kura, sasa niwaombe tujitokeze pia kupiga kura itakapofika Oktoba ili tuwashinde kwa kishindo,” amesema.

Amewashukuru wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Halmashuri Kuu ya CCM Taifa waliompigia kura na kumthibitisha yeye na Rais Samia kuwa wagombea urais kwa kipindi kingine.

“Kuna watu wanaweza kujiuliza kwa nini tumepitishwa mapema hivi tofauti na kawaida, lakini jibu ni kwamba wajumbe wameridhika namna tulivyotekeleza Ilani,” amesema Mwinyi.

Mzee wa chama hicho aliyepata fursa ya kusalimia katika hafla hiyo, Baraka Shamte amesema lipo kundi linataka fomu za kugombea lakini mkutano mkuu ulikuwa na jukumu la kumaliza kazi.

“Tunapongeza kamati kuu na mkutano mkuu, walifanya uamuzi sahihi, wenzetu wanalalamika huko lakini hii haijawahi kutokea katika chama chetu,” amesema.

Amesema CCM hakijawahi wala haiwezi kushindwa huku akiwataka viongozi hao kutoa elimu kwa vijana ili wasiharibu kura siku ikifika kwa kuandika mambo ambayo yatakuwa hayafai.

Dk Mwinyi alipokewa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume saa 8:30 mchana kisha akaondoka na msafara wake kwa mwendo wa taratibu hadi makao makuu ya ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.

Wakati akitoka uwanja wa ndege, barabara ilifungwa na kuruhusu msafara wake, akiwa katika gari la wazi lenye rangi ya kijani, njiani alikuwa akiwasalimia na kuwapungia mikono wananchi waliokuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara kumlaki.

Baada ya kufika ofisi za chama Kisiwandui, Dk Mwinyi alizuru kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, akasaini kitabu kisha akasalimiana na wazee.

Baada ya kumaliza shughuli hizo aliondoka na kuelekea Mnara wa Kisonge ilipoandaliwa sehemu maalumu kwa ajili ya burudani na kuzungumza na wananchi.

Related Posts