Uamuzi wa Chadema: Wasira ahoji amri za Lissu, wachambuzi wapongeza

Dar es Salaam. Wakati Freeman Mbowe akihitimisha uongozi wake ndani ya Chadema kwa kuacha maagizo mawili ikiwemo kuundwa tume ya ukweli na upatanishi ili kutibu makovu yatokanayo na uchaguzi, mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu amemuunga mkono akisema itakwenda kuangazia chaguzi zote kuanzia ngazi ya chini.

Lissu ambaye sasa ndiyo mwenyekiti amekwenda mbali zaidi akisema tume ya ukweli na upatanishi iliyopendekezwa na Mbowe itakayoundwa itakwenda kushughulikia makovu yaliyotokana na chaguzi mbalimbali zilizofanyika ndani ya chama hicho. 

Mbali na hilo, Lissu anayekuwa mwenyekiti wa nne wa Chadema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992 amebainisha mambo ambayo utawala wake utayasimamia ikiwemo ukweli na uwazi pasi na kuyumba. Wenyeviti wengine ni Edwin Mtei na Bob Makani.

Kushusha madaraka na mgawanyo wa fedha kutoka makao makuu kwenda ngazi za chini kama kanda, mikoa na wilaya itakuwa kipaumbele chake.

Pia, mabadiliko ya katiba ya chama ili kuweka ukomo wa uongozi kwa ngazi zote zikiwamo za  udiwani na ubunge wa viti maalumu ili kuweka ulinganifu wa wanawake wengi kushiriki.

Miamba hiyo ya siasa za upinzani wamesema hayo leo Jumatano, Januari 22, 2025 mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mbali ya Lissu, Makamu mwenyekiti bara ameshinda John Heche kwa kura 577 sawa na asilimia 57 dhidi ya washindani wake wawili, Matharo Gegul alipata kura 49 asilimia 5 na Ezekia Wenje kura 372, sawa asilimia 37.

Nafasi ya Makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar ameshinda Said Mzee Said ambaye amepata kura 625 sawa na asilimia 89 ya kura 706, huku halali zikiwa 700 na sita zimeharibika.

Lissu mwenyewe amemshinda Mbowe kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5 ya kura zote 996. Mbowe amepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku Charles Odero akipata kura moja. Kura tatu zimeharibika.

Matokeo hayo yameibua shangwe na mijadala maeneo mbalimbali kubwa ikipongezwa Chadema kwa kuonesha demokrasia ya kweli kwa miamba miwili kuchuana na kuhitimisha uchaguzi uliokuwa huru na wa uwazi.

Mara baada ya kura kumalizwa kuhesabiwa asubuhi ya leo na kuonesha Lissu ameshinda, Mbowe alitumia ukurasa wake wa kijamii wa X kumpongeza kwa ushindi huo.

“Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa mkutano mkuu wa chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mheshimiwa Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu.”

Baadaye akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu kuwashukuru na kuwaaga, Mbowe ametoa maagizo mawili kwa uongozi mpya chini ya Lissu kuponya majeraha ya uchaguzi na kuilinda katiba ya chama.

Mbowe ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Chadema atakuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu amesema: “Tumemaliza uchaguzi huu, lakini uchaguzi huu umeacha majeraha mengi kwa chama chetu, ushauri wangu kwa viongozi wetu kakiponyeni chama chetu.”

“Mimi niliahidi ningeshinda ningeunda tume ya ukweli na maridhiano, watu wakazungumze yaliyojiri kwenye uchaguzi huu, watu walipokoseana, walipokosana, walipokosa maadili, walipokibagaza chama chetu, wakasameheane wapeane mikono ili chama chetu kiwe na nguvu zaidi,” amesema.

Amesema: “Kama mnaniheshimu kama mtu niliyekifanyia kazi chama hiki, nawaagiza haraka kaundeni tume ya ukweli na upatanishi, mkatibu majeraha ili muweze kujenga umoja.”

“Ushindi wowote ni ushindi wa chama, asitoke mmoja wetu akaleta kiburi cha uchaguzi. Oneni ulazima wa kutibu majeraha ya mchakato wa uchaguzi.”

Mbowe pia, amewaasa viongozi wapya kuilinda katiba ya chama badala kuendesha chama kwa mapenzi yao.

“Tembeeni kwenye katiba ya chama, msitembee kwenye mapenzi yenu, tembeeni kwenye katiba. Pale mnapoona katiba ina upungufu, shirikisheni wenzenu.”

Akizungumzia mnyukano uliokuwepo katika uchaguzi huo, Mbowe amesema kuna watu walimshauri ajitoe lakini aliwakatalia.

“Wakati mnyukano umekolea wapo walioniambia toka, nikawaambia nitafia kwenye demokrasia. Naondoka nikiwa na fahari kwa demokrasia niliyoijenga kwa miaka 30,” amesema.

Amesema katika mazungumzo yake mbalimbali aliahidi uchaguzi huo utakuwa huru, wazi na wa kidemokrasia jambo ambalo kila mmoja ndani na nje ya Chadema na Tanzania wameshuhudia hilo.

Mbowe ameishukuru familia yake kwa kumvumilia kwa muda wote aliokuwa kiongozi wa Chadema.

“Baada ya matokeo, wa kwanza kunipigia simu alikuwa binti yangu, halafu akaja mama yake wakasema nirudi nyumbani wakanipikie supu, nikampa akaongea na Lissu. Sisi ni rafiki wa familia,” amesema.

Amesema kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara, amepata likizo ya wafanyabiashara: “Nakwenda kutafuta mafekechee.”

Lissu alipata wasaa wa kuzungumza na wajumbe wa mkutano huo mara mbili. Wakati akimkaribisha Mbowe na baadaye kufunga mkutano mkuu huo. Katika maelezo yake amesema hatokuwa na ndimi mbili kwenye utumishi wake.

“Tumelipata tulilokuwa tukilitafuta, sasa tufanye kazi na kazi inaanza leo. Kuanzia leo, kesho na siku zinazofuata tunafanya kazi ya kuhakikisha tunajenga chama chetu.”

Amesema kilichotokea katika chama hicho (uchaguzi) ni jambo la historia katika siasa za chama hicho na nchi kwa jumla.

Lissu amesema uchaguzi huo umeacha maumivu makubwa: “Lakini hatutalipiza kisasi mimi si mtu wa visasi. Tutawaponya wale wote walioumizwa na uchaguzi huu ambao tunasema ni wa kihistoria. Tuliingiza taratibu ambazo si za kikatiba, hivyo kama tunataka kuwa salama tutarudi kuwaambia wanachama wetu kwamba hili halitajirudia.”

Katika hotuba hiyo, Lissu amesema moja ya kazi watakayoanza nayo kwa sasa ni kuangazia rufaa zilizokatwa na watia nia wa ujumbe wa kamati kuu, ambao kamati kuu iliwaengua kwa sababu mbalimbali.

“Tutaanza na maumivu ya chinja chinja ya wagombea, tutasikiliza rufaa zao kama zina hoja tutawarudisha. Kila mwenye haki ya kugombea uongozi ni lazima apate nafasi hiyo.

Lazima tuhakikishe watu wote wanatendewa haki, hatuwezi kudai haki kwa CCM wakati sisi wenyewe ndani hatutendeani haki,” amesema.

Huku akishangiliwa, Lissu amesema: “Kila mwanamke katika chama hiki anayetaka kuwa diwani au mbunge wa kuchaguliwa au viti maalumu ni lazima wapate haki sawa.

“Namna bora ya kufanya hilo, tutaweka ukomo wa viti maalumu hata ikitulazimu kufanya mabadiliko ya katiba na kanuni. Tutaweka pia ukomo wa uongozi wa chama, mimi sitaki kuja kuhutubiwa kwamba nimekaa kwenye uongozi kwa muda mrefu hili litaanza na mimi,” amesema.

Aidha, Lissu katika hotuba yake amesema kwenye uongozi wake hatokuwa na ndimi mbili na kwamba endapo sheria za uchaguzi hazitabadilishwa basi hakuna kufanyika uchaguzi.

Jambo jingine ambalo utawala wake utalifanya ni kurejesha madaraka ngazi ya chini kutoka makao makuu ikiwamo fedha zinazopatikana kuzishusha huko ili kuleta ufanisi na kama hazitokuwapo basi wataelezwa.

Kuhusu maridhiano na CCM amesema wanakubaliana nayo, lakini yenye mwelekeo chanya na kama hakuna katiba hakuna uchaguzi.

Aidha Lissu amesema Mbowe amewezesha kufanyika kwa kitu kikubwa ambacho hakijawahi kufanyika tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992.

”Tumefanya uchaguzi ambao hatujawahi kuufanya katika historia yetu kama chama. Tumeweka viwango vya juu kwa vyama vingine. Sasa chama chochote kama kinatuweza wafikie hicho kiwango, tumefanya uchaguzi wa kihistoria, huru na haukuwa na mizengwe.

“Mivutano ilikuwepo lakini hakukuwa na mizengwe, ulikuwa uchaguzi huru, kila mwenye haki ya kupiga kura alipiga kura na ilihesabiwa na kuhesabika. Matokeo ambayo tumepata yametokana na kura halali.”

Kuhusu maridhiano, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira amesema chama hicho kiko tayari kuzungumza na chama chochote.

“Mimi nilisema tuko tayari kwa maridhiano, lakini sina dawa ya kukwama kwa maridhiano. Kwa hiyo kama Chadema watakuja na mambo mahususi, tutazungumza,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu kukwama kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya CCM na  Chadema, Wasira amesema kuna mambo waliyoleta likiwemo la mabadiliko ya Katiba ambayo ni ya muda mrefu.

“Chadema walikuja na mambo 11, lakini katika awamu ya kwanza ya mazungumzo kulikuwa na mambo sita na manne yalikubaliwa,” amesema.

Ametaja suala la Katiba akisema walishindwa kuafikiana kwa sababu linahitaji muda mrefu.

“Mabadiliko ya Katiba ni jambo nyeti, huwezi kulimaliza kwa siku moja. Leo ni Januari, Bunge linaisha Juni na litakuwa ni Bunge la bajeti, huo muda wa kujadili katiba utatoka wapi?

“Dunia hii kuna mambo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu,” amesema.

Ametaja pia suala la wabunge 19 waliofukuzwa Chadema, akisema lilishindikana kwa sababu suala lao lilikuwa mahakamani.

Hata hivyo, amesema yapo yaliyofanikiwa likiwamo la kufunguliwa kwa wanachama wa Chadema waliokuwa na kesi za kisiasa na kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara.

“Chadema wamefanya mikutano ya hadhara nchi nzima,” amesema.

Wakati Lissu akisisitiza kuwa katika uongozi wake wataweka azimio la kutaka mageuzi ya uchaguzi maarufu “No reforms no election”, Wasira amekosoa kauli mbiu hiyo akisema ni amri.

“Hiyo ni amri sio mapendekezo, sasa utakujaje kwenye mazungumzo na amri? Nilisema kwenye mkutano mkuu wa CCM kwamba, tuko tayari kwa maridhiano na tutazungumza na wadau wote zikiwamo asasi za kiraia, vyama vya siasa na mashirika ya dini, ili tupate amani tufanye maendeleo,” amesema.

Akijadili suala hilo, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Revocatus Buyobe amesema, pamoja na misimamo mikali ya Lissu, hajaonyesha kukataa mazungumzo.

“Lissu na Mbowe wanatofautiana, lakini Lissu hajasema hataki mazungumzo. Kwa kuwa Makamu mwenyekiti wa CCM, Wasira amesema ataanza na mazungumzo, basi watakubaliana,” amesema.

Akiuzungumzia uchaguzi wa Chadema, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka amesema umeakisi jina la chama hicho.

“Kwa muda mrefu Mbowe amekuwa hapati upinzani mkali, lakini safari hii amepata upinzani na hiyo ndio demokrasia na ni somo kwa vyama vingine,” amesema.

Kuhusu kuponya majeraha, Seka amesema japo Mbowe ameshindwa, lakini kwa asilimia 48 alizopata bado ana wafuasi wengi.

“Lissu ana kazi kubwa ya kuvunja makundi kwa kuwashirikisha katika uongozi. Tunatarajia kuona Mbowe atapewa nafasi zaidi ya kushiriki katika chama,” amesema.

Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba amesema Chadema wameonyesha ukomavu wa siasa kwa kurejesha mshikamano baada ya uchaguzi.

“Awali tuliona malumbano yaliyotishia kupasua chama, lakini wamemaliza vizuri,” amesema.

Kuhusu ukomo wa madaraka unaozungumzwa na Lissu, Dk Bisimba amesema ni muhimu kwa taasisi.

“Ukomo wa madaraka una uzuri wake kwa sababu unaleta mawazo mapya katika taasisi na kunakuwa na uendelevu,” amesema.

Mwanazuoni maarufu nchini, Profesa Abdallah Saffari amesema ulikuwa huru, haki na uwazi tofauti na chaguzi nyingine za vyama vya siasa, akimtaka Mbowe kukubaliana na kilichotokea na awasaidie viongozi wapya.

“Kiukweli awasaidie hawa, maana yeye ni mzoefu pia, hasa katika kutafuta Katiba mpya,” amesema Profesa Saffari ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara.

Awali, Heche amesema majukumu waliyopata ni makubwa hawana budi kuungwa mkono katika kuendeleza mapambano ya chama hicho.

 “Mbowe ameweka standards ambazo hazijawahi kuonekana kwenye chama kingine, Chadema ni chama pekee ambacho watu wake wanaweza kubadilishana madaraka kwa njia za kidemokrasia.

“Chadema ni chama, tutakilinda na tunawahidi kukiendeleza, hakuna kulala hadi kieleweke,” amesema.

Heche amempongeza Mnyika kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kusimamia uchaguzi huo pamoja na sekretarieti yake.

“Nimshukuru sana ndugu yangu John Mnyika, ni mtu mwadilifu na msafi sana, nilivyomfahamu tangu siku ya kwanza hadi sasa hajawahi kubadilika. Fikiria kwa presha ile amefanya kazi na mwenyekiti (Mbowe) kwa miaka yote hiyo lakini amesimamia uchaguzi ukiwa amenyooka. Hakutaka kuona aibu na kupindisha mambo,” amesema.

Related Posts