VIDEO: Lissu atoa kauli dhidi ya Mbowe

Dar es Salaam. Baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa takribani siku mbili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amemshukuru mtangulizi wake, Freeman Mbowe na kueleza walichofanya kitaacha historia kwenye siasa za Tanzania.

Lissu aliyepata nafasi ya kuzungumza baada ya matokeo kutangazwa leo Jumatano, Januari 22, 2025, amesema Mbowe amewezesha kufanyika kwa kitu kikubwa ambacho hakijawahi kufanyika tangu kuanzishwa kwa chama hicho.


Kauli ya Lissu dhidi ya Mbowe

”Tumefanya uchaguzi ambao hatujawahi kuufanya katika historia yetu kama chama. Tumeweka viwango vya juu kwa vyama vingine. Sasa chama chochote kama kinatuweza wafikie hicho kiwango, tumefanya uchaguzi wa kihistoria, huru na haukuwa na mizengwe.

“Mivutano ilikuwepo lakini hakukuwa na mizengwe, ulikuwa uchaguzi huru, kila mwenye haki ya kupiga kura alipiga kura na ilihesabiwa na kuhesabika. Matokeo ambayo tumepata yametokana na kura halali.”

Kuhusu hatua ya Mbowe kukubali matokeo hata kabla ya kutangazwa Lissu amesema ni kitendo cha heshima kukubali matokeo na kuruhusu uchaguzi huo uwe huru na uliozingatia misingi ya kidemokrasia.

“Tumefanya uchaguzi uliofuatiliwa na Watanzania ndani na nje ya Tanzania. Sasa mwenyekiti, wapigakura wametamka na wewe umekubali kauli ya wapigakura, tunakushukuru sana,” amesema Lissu huku akishangiliwa.


Lissu mwenyekiti mpya Chadema

“Mwenyekiti wetu ameongoza chama kwa miaka mingi na kuwa kiongozi aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi katika historia ya chama. Alichukua chama kikiwa na wabunge watano, amekipeleka hadi kikawa chama kikuu cha upinzani, akakifanya chama kilichounda kambi rasmi ya upinzani na chama kikubwa cha siasa katika historia ya nchi hii.”

Lissu amemshukuru Mbowe kwa kazi kubwa aliyoifanya na hakuna miongoni mwao anayeweza kuibeza akisisitiza histora ya nchi itaandikwa juu ya demokrasia, jina la Mbowe litaandikwa kwa wino wa dhahabu.

Mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu wakati akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho leo Jumatano Januari 22, 2025.

Kabla ya matokeo kutangazwa rasmi na mwenyekiti wa uchaguzi, Profesa Raymond Mushi, Mbowe alitumia ukurasa wake wa X kuwapongeza Lissu na timu nzima iliyoshinda uchaguzi huo.

“Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa mkutano mkuu wa chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22, Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu,” ameandika Mbowe.

Freeman Mbowe na Tundu Lissu wakijadili jambo baada ya kurudi ndani ya ukumbi wa Mlimani City leo Januari 22, 2025. 

Katika nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, wapigakura waliojisajili walikuwa 1,014 huku kura zilizopigiwa ni 999, halali zikiwa 996 na tatu zimeharibika.

“Odero Odero kapata kura moja sawa na asilimia 0.1, Freeman Mbowe amepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku Lissu akipata kura 513 sawa na asilimia 51.5,” amesema  Profesa Raymond Mushi mwenyekiti wa uchaguzi.

Nafasi ya Makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar ameshinda Said Mzee Said ambaye amepata kura 625 sawa na asilimia 89 ya kura 706 huku halali zikiwa 700  na sita zimeharibika.

Katika upande wa Makamu mwenyekiti bara idadi ya wapigakura ni 1, 014 zilizopigwa ni 1,005, halali zikiwa 998 na saba zimeharibika.

Matharo Gegul alipata kura 49 asilimia 5, Ezekia Wenje (kura 372, sawa asilimia 37) na John Heche kura 577 sawa na asilimia 57. Hivyo Makamu mwenyekiti wa Chadema bara ameshinda Heche.

Uchaguzi huo umesimamiwa na wazee wanane akiwamo Profesa Mushi na Katibu akiwa Dk Azaveli Lwaitama. Wengine ni Ruth Mollel, Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo na Azumuli Kasupa.

Related Posts