Unguja. Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaibu Ibrahim Mohammed, amesema ipo haja Serikali kuendelea kubuni mbinu za kuwajengea uwezo vijana, wajitambue, kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Amesema hayo wakati akifungua kongamano la vijana leo Jumatano, Januari 22, 2025, katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana Bweleo, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini na Magharibi, Zanzibar.
Amesema kongamano hilo ni muhimu katika kuwapa moyo wa kujitolea na uzalendo vijana, hasa katika kipindi hiki cha kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ipo pamoja na wadau wa masuala ya vijana, ikiwemo kupatia mafunzo ya uongozi ili wawe wazalendo wa kujenga nchi yao na viongozi wa hapo baadaye,” amesema.
Hivyo, amewaomba wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na wizara hiyo ili kuwaendeleza na kuwawezesha vijana katika nyanja mbalimbali kama vile za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na Kilimo Hai na Masuala ya Kijamii (PPIZ), Ikram Ramadhan Soraga, amesema wapo mstari wa mbele kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya kujitolea na uongozi.
Amesema makongamano kama hayo ni muhimu kwa vijana kwani yatasaidia kujielewa, kuwajengea uwezo, na kujiajiri na kuajiriwa.
Naye Faiza Nassor Said, Mratibu wa Zan Change Makers, amesema lengo la mradi huo ni kuwakusanya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar na nje ya nchi kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujiongoza na kuelewa jinsi ya kuishi na watu wengine.
“Lazima vijana wajitambue, wapewe miongozo namna wanavyoweza kujiongoza na stadi za maisha ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika harakati za maisha,” amesema.
Nao baadhi ya vijana waliopewa mafunzo hayo wamesema yatawasaidia kujipambanua na kutambua mambo yanayotakiwa kufanywa kwa ajili ya mustakabali wao na Taifa kwa ujumla.
Khadija Omar ni mmoja wa vijana hao, amesema yapo mengi wataondoka nayo na kwenda kuyafanyia kazi katika maisha ya kawaida huku wakijenga mikakati ya kuinuana katika kutembea njia ya pamoja.
“Vijana ni nguvu ya Taifa. Lazima tuwe na mipango na mikakati kuhakikisha tunainuana na kuliinua taifa letu, lakini haya hayawezi kufanyika ikiwa hakuna mipango na mbinu za kufika huko,” amesema.
Mafunzo hayo ya siku nne ya kuwajengea uwezo vijana kutoka Tanzania Bara, Ghana na wenyeji Zanzibar, yameandaliwa na Taasisi ya Zan Change Makers chini ya ufadhili wa mashirika mbalimbali.