ZFDA yaondoa sokoni vidonge vya PED Zinc kwa kukosa sifa

Unguja. Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA), imeondoa sokoni dawa aina ya PED Zinc (Zinc Sulphate Dispersible Tablet) toleo namba 2203002.

Dawa hiyo inatengenezwa na kiwanda cha Beta Healthcare International Ltd cha Nairobi, Kenya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 21, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA, Dk Burhan Othman Simai, imeleza toleo hilo limelalamikiwa na vituo vya afya kuwa vidonge vyake vinatoa ukungu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, toleo hilo limezalishwa Machi mosi, 2022, na tarehe ya mwisho ya matumizi yake ilikuwa Februari 28, 2025.

“ZFDA ilifanya ufuatiliaji kufuatia malalamiko hayo, ikiwemo kuchukua sampuli na kuzifanyia uchunguzi wa kimaabara, ambapo majibu yalionyesha kuwa toleo hilo lilifeli vipimo na hivyo kusababisha kutofaa kutumika kwa matumizi ya binadamu,” amesema.

Amewataka wananchi kutambua dawa za toleo hilo na kuepuka kuzitumia, na wale ambao walikwisha kuwa na dawa za toleo hilo wazirejeshe kwenye vituo vya afya au maduka ya dawa walikozipata.

Pia, amewataka wataalamu wa afya kuzitambua dawa za toleo hilo, kuacha kuzitoa kwa wagonjwa, kuzitenga na kuzirejesha kwa msambazaji aliyewazambazia.

Jambo lingine, ZFDA pia imewataka waingizaji, wasambazaji, na wauzaji wa jumla na rejareja walio na dawa hizo kusitisha usambazaji wake na kuziuza, badala yake kuzitenga na kuziwasilisha ZFDA kwa ajili ya kuziteketeza.

“ZFDA inaomba wataalamu wa afya na wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu bidhaa za dawa zenye viashiria vya ubora duni au madhara yanayosababishwa na utumiaji wa bidhaa za dawa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati na kwa ajili ya manufaa ya umma,” imeeleza taarifa hiyo.

Akieleza namna hatua wanazochukua kabla ya kuchukua hatua hizo, Mkurugenzi Msaidizi wa ZFDA, Yussuf Ali, amesema wanafuatilia bidhaa sokoni (TMS) wanapopata malalamiko kutoka watumiaji au wauzaji. Wanaweza kukusanya sampuli ya dawa hizo na kuzipeleka maabara.

“Uchunguzi wa maabara ndio unatuambia kama dawa ina shida, ikiwa imekaa muda mrefu na haina sifa tena, au imebadilika rangi au imesababisha shida kwa watumiaji,” amesema Yussuf.

Mei 2024, ZFDA pia iliondoa sokoni zaidi ya makopo 1,000 ya maziwa aina ya Infacare na kupiga marufuku uingizaji, uuzaji, na usambazaji wa maziwa hayo kutokana na kuwepo kwa maandishi kwenye bidhaa hiyo yanayokataza kuuzwa nchini.

Hata hivyo, wakala huyo ulisema kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanafanya udanganyifu kwa kuchuna maandishi hayo na kubandika stika juu yake au kubadilisha mifuniko halisi na kuza bidhaa hiyo, jambo ambalo ni kosa kisheria.

ZFDA ilisitisha matumizi ya maziwa hayo kutokana na kutokukidhi matakwa ya sheria na vigezo vya bidhaa za chakula, kusajiliwa, na kutothibitishwa kwa ubora na usalama na wakala wa dawa.

Katika ukaguzi uliofanywa kipindi hicho, walifanikiwa kutoa sokoni zaidi ya makopo 1,000 ya maziwa hayo yakiwa na maandishi yanayosomeka ‘Not for Sale in Tanzania’ (Yasiuzwe Tanzania).

Related Posts