Moshi/Nairobi. Mahakama ya jijini Nairobi, imeamuru kijana John Wambua (29), anayedaiwa kukutwa akiwa amebeba begi lenye vipande vya mwili wa mkewe, aendelee kushikiliwa na polisi kwa siku 21 ili waweze kukamilisha upelelezi.
Wambua alikamatwa na polisi wa doria saa 11 alfajiri ya Januari 21, 2025 katika Mtaa wa Huruma jijini Nairobi, akiwa amebeba begi mgongoni baada ya maofisa hao kumshuku anasafirisha bidhaa haramu na ndipo walipobaini mwili huo.
Amri hiyo imetolewa Januari 22, 2025 na Hakimu Gilbert Shikwe kufuatia ombi la Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) nchini Kenya kuwawezesha makachero kukamilisha upelelezi ikiwamo kuchukua maelezo ya mashahidi muhimu wa tukio hilo.
Nyaraka za mahakama zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa na makachero, Wambua anadaiwa kukiri kumuua mkewe aliyefahamika kwa jina la Fridah Munani (19) baada ya kumkuta mkewe na mwanamme mwingine.
Awali, taarifa iliyotolewa na DCI kupitia kurasa zake za X (zamani Twitter) na Facebook, ilieleza kuwa wakati polisi wakikamilisha jukumu lao la doria karibu na Kelly Towers, walimsimamisha mshukiwa huyo akiwa na begi mgongoni.
Wakiwa na imani pengine alikuwa akisafirisha kitu ambacho si halali, walipekua begi alilokuwa amebeba na kwa mshtuko, walikuta amebeba vipande vya mwanamke na katika mahojiano alidai ni vya mkewe, Fridah Munani (19).
Taarifa hiyo ambayo imenukuliwa pia na vyombo vya Habari vya Kenya na mashirika ya Habari ya kimataifa, ilidai kuwa Wambua aliwaongoza maofisa wa Polisi hadi nyumbani kwake na chini ya kitanda walikuta pia kichwa cha Fridah.
Halikadhalika maofisa hao walidai kufanikiwa kupata kisu ambacho ndio silaha iliyotumika kumchinja mwanamke huyo pamoja na nguo za marehemu zikiwa na damu na kwamba baadhi ya sehemu za mwili wa marehemu hazijapatikana.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza BBC, Kenya inatajwa kuwa na matukio mengi ya mauaji ya wanawake ambapo kati ya Agosti na Oktoba 2024 pekee, wanawake 97 waliuawa kikatili na hiyo ni kwa mujibu wa Polisi Kenya.