Aliyemuua mwenzake wakigombea maji, ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Shinyanga imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Nkwabi Joseph, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mwanakijiji mwenzake, Tungu Sabuni.

Katika hukumu ya Januari 22, 2025 aliyoitoa Jaji Lutengano Mwakahesya na nakala yake kupatikana katika tovuti ya Mahakama, Nkwabi amepewa adhabu hiyo baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.

Nkwabi alishitakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 25, 2023 katika kijiji cha Tinden Hulu, Wilaya na Mkoa wa Shinyanga.

Ilidaiwa kuwa marehemu alikuwa amechimba dimbwi la maji kando ya mto wa eneo hilo alilokuwa akitumia kunyweshea mifugo yake na wakati wa ukame huwakataza wanakijiji wenzake kuchota maji hayo.

Ilielezwa na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa huyo alikuwa na bustani na alihitaji maji kwa ajili ya kumwagilia na siku hiyo ya tukio akiwa amebeba panga na makopo ya plastiki, alikwenda kuchota maji kwenye bwawa la marehemu.

Ilidaiwa marehemu aliyekuwa akilinda bwawa hilo alimkabili mshitakiwa na kutomruhusu kuchota maji, jambo hilo lilimkasirisha mshitakiwa huyo na kwa hasira zake alimkata marehemu kwa panga alilokuwa ameshika.

Ilidaiwa kuwa alimkata sehemu kadhaa za mwili wake ikiwemo kichwani huku mmoja wa watoto wa marehemu waliokuwa jirani na malisho ya ng’ombe walishuhudia tukio hilo, wakapiga kelele na kuwahi eneo la tukio na kumkamata Nkwabi.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane, vielelezo sita huku mshtakiwa akiwa shahidi pekee wa utetezi.

Shahidi wa pili ambaye ni mtoto wa marehemu, Mayunga Pastory, alidai siku ya tukio akiwa anachunga kwenye mashamba ya mpunga alimuona mshtakiwa ambaye alimfahamu tangu utotoni akiwa amebeba panga na baadhi ya makopo ya kubebea maji.

Alidai kumuona mshtakiwa akiwa anazonana na marehemu karibu na dimbwi la maji la marehemu, ndipo mshtakiwa huyo alimshambulia marehemu kwa panga na kudai yeye na kaka yake walipiga kelele kuomba msaada na kufanikisha kukamatwa Nkwabi.

Alidai kuwa katika eneo la tukio walimkuta marehemu akivuja damu nyingi kichwani na mkononi.

Shahidi wa kwanza PF. 21937 Inspekta Charles Luzambya kutoka Kituo cha Polisi Didia, alidai siku ya tukio watu watatu walifika ofisini kwake mmoja akiwa na shati lililolowa damu (mshitakiwa) na mwingine alikuwa amebeba panga lililokuwa na damu.

Shahidi wa tatu, Kajala Nangi, alidai siku ya tukio aliombwa kubeba abiria na alipofika eneo la tukio alikuta shati la mshtakiwa likiwa limelowa damu, hivyo kumpeleka mshitakiwa kituo cha polisi.

Shahidi wa nne, Masali Sabuni ambaye pia ni mtoto wa marehemu, alidai Oktoba 25, 2023 alipigiwa simu na shahidi wa pili akimjulisha kuhusu kushambuliwa kwa baba yao, na alipofika eneo la tukio marehemu alikuwa na majeraha kichwani, mkononi na mguuni.

Alidai marehemu alimweleza kuwa alivamiwa na mshtakiwa na kwa wakati huo mshitakiwa alikuwa amekamatwa na wanakijiji na alikuwa amelala pembeni na panga mkononi na kusisitiza kuwa mshitakiwa aliwahi kugombana na marehemu kuhusu matumizi ya bwawa la maji.

Shahidi wa tano ambaye alikuwa ni mwenyekiti  wa kijiji cha Kitendan’hulu, Philipo Shimba, alidai siku ya tukio alipokea simu kutoka kwa shahidi wa nne na alipofika eneo la tukio alikuta mshitakiwa akiwa amefungwa mikono huku marehemu akiwa na majeraha mengi.

Alidai alimwambia shahidi wa nne ampeleke mwathirika hospitalini huku akimpeleka mshitakiwa polisi.

Daktari kutoka Zahanati ya Didia, Kapime Thomas ambaye alikuwa shahidi wa sita katika kesi hiyo alidai Oktoba 25, 2023, saa  sita mchana, aliombwa kwenda katika Kituo cha Afya cha Bugisi kufanya uchunguzi wa maiti.

Alidai marehemu alikuwa na majeraha matano, sehemu ya nyuma ya kichwa, kwenye kiganja cha mkono wa kushoto huku vidole vya kati vikining’inia, majeraha mengine yalikuwa kwenye mkono wa juu wa kushoto na mguu wa kushoto na kifo hicho kilisababishwa na kuvuja damu nyingi.

Shahidi wa nane, H.8896 Koplo Stanslaus, alidai Oktoba 25, 2023 yeye na polisi wenzake walipewa maelekezo ya kwenda Didia kwenye tukio la mauaji na walipofika aliagizwa kumhoji mshtakiwa na kudai mshtakiwa alikiri kumuua marehemu.

Baada ya Mahakama kumkuta mshitakiwa huyo akiwa na kesi ya kujibu kwa mujibu wa kifungu cha 293(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, alipewa nafasi ya kujitetea ambapo alichagua kutoa ushahidi kwa kiapo.

Alidai siku ya tukio asubuhi, alikwenda kumwagilia bustani yake iliyopo pembezoni mwa mto Ishegenya na kuwa akiwa na mitungi mitatu ya maji, alielekea kwenye bwawa la maji lililochimbwa na marehemu mjomba wake, Hamisi.

Alidai alikuwa pia na panga alilokuwa amekusudia kutumia kupasua kuni baada ya kumaliza kumwagilia bustani yake na kuwa alipofika bustanini kwake alikwenda kwenye bwawa na kwa mbali aliona watu wanne wakija kwa upande wake.

Alidai mmoja wao alikuwa ni marehemu akiwa amebeba kombeo, wa pili akiwa Willy Tungu, wa tatu akiwa Mayunga Tungu aliyekuwa na panga na wa nne akiwa Pius Masali.

Alidai walipofika walianza kurusha mawe kwa kutumia kombeo, hivyo na yeye alilazimika kutumia kopo moja kama ngao ya mawe aliyorushiwa na walipofika kwake walimvamia kimwili na kumfanya aanze kujitetea.

Alidai alitupa kopo aliyokuwa akiitumia kama ngao na kutoa panga lake lililofungwa kwenye baiskeli yake na alitumia panga kujitetea na kudai chanzo cha shambulio hilo ni wavamizi hao kudai kuwa alikuwa akichota maji kwenye bwawa lao.

Alieleza kuwa madai ambayo yalikuwa ya uongo kwa sababu bwawa hilo lilikuwapo tangu mwaka 2003 na kila mtu kijijini alijua lilichimbwa na marehemu mjomba wake.

Mshitakiwa huyo alidai  alijitetea na kuwazidi nguvu washambuliaji wake ambao nao walitawanyika, hata  hivyo, marehemu alijaribu kumpiga na chuma lakini aliikamata kwa mkono wa kushoto na kuishika, mkono wake wa kulia kulikuwa na panga lake na kuwa waliokimbia walirudi kumsaidia marehemu.

Alidai alimpiga marehemu kwa kutumia ubapa wa panga lake na marehemu akaanguka chini na kuwa mmoja wa washambuliaji hao aliporusha jiwe ambalo lilimpiga na kumfanya aanguke na kupoteza fahamu.

Alidai alipopata fahamu aligundua kuwa alikuwa na jeraha la pili usoni, upande wa kulia wa uso wake, huku jeraha la pili lilikuwa upande wa kushoto wa uso wake ambalo lilikuwa linavuja damu iliyomwagikia panga lake.

Mshtakiwa huyo alieleza mahakama kuwa wakati huo alikuwa amedhoofika sana kwa sababu alikuwa amevuja damu nyingi, ambapo alimuona marehemu akiwa pembeni yake, kifua wazi huku kukiwa na umati wa watu, akikana kumkata marehemu kwa panga.

Alidai Mwenyekiti huyo alimnyima fursa ya kuosha damu usoni na fulana yake ilikuwa imelowa damu na kupanda naye pikipiki kumpeleka kituo cha polisi Didia kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Shinyanga.

Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mwakahesya alichambua ushahidi huo na kumtia hatiani mshtakiwa kosa la mauaji ya mwanakijiji mwenzake na kusisitiza kifo cha marehemu hakikuwa cha kawaida.

Jaji alisema kuwa ni jambo lisiloeleweka kwamba mshitakiwa alipokuwa akilinda maisha yake dhidi ya washambuliaji wengi, alikuwa na akili ya kutumia tu ubapa wa panga kujitetea huku marehemu akikutwa na majeraha yanayoendana na aina ya silaha iliyotumiwa na mtuhumiwa.

“Katika kesi hii mtuhumiwa alitumia panga ambalo ni silaha hatari na mbaya, mbili katika shambulio hilo alisababisha majeraha mengi nyuma ya kichwa cha marehemu, sehemu ya juu ya mkono wake wa kushoto, mguu wa kushoto na kidole cha shahada na cha kati cha mkono wa kushoto vilikatwa na karibu kujitenga nayo.

“Hii inaonesha kuwa nguvu iliyotumiwa na mshtakiwa ilikuwa nyingi na vipigo vilikuwa vingi vikiwemo vitano vya kisogoni,vipigo hivyo pia vilielekezwa kwa sehemu zilizo hatarini za mwili,” alisema Jaji Mwakahesya.

Alisema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi yake kwa kiwango kinachohitajika na sheria, pasipo shaka yoyote na kumkuta Nkwabi na hatia ya kosa la mauaji na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Related Posts