Aliyetakiwa Yanga atua Sauzi | Mwanaspoti

UNAMKUMBUKA yule straika mwili jumba, Makabi Lilepo aliyekuwa akiwindwa na Yanga tangu msimu uliopita ili kuja kuziba nafasi ya Fiston Mayele? Unaambiwa jamaa huyo aliyekuwa enzi hizo Al Hilal ya Sudan ametua Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini akitokea Valenciennes ya Ufaransa.

Lilepo alikuwa akitakiwa na Yanga iliyokuwa chini ya Kocha Nasreddine Nabi ambaye kwa sasa yupo Kaizer na ndiye aliyependekeza mshambuliaji huyo asajiliwe kuisaidia timu hiyo inayopambana kurejesha heshima katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).

Mwaka 2023, viongozi wa Yanga, wakiongozwa na Injia Hersi Said, walifanya mazungumzo na wakala wa Lilepo wakimuhitaji mchezaji huyo, lakini walishindwa kufikia makubaliano baada ya mchezaji huyo kupokea ofa kubwa kutoka Ufaransa.

Baada ya Yanga kugonga mwamba katika harakati zao za kumchukua, Lilepo alijiunga na Valenciennes ya Ufaransa ambayo msimu uliopita ilishuka daraja kutoka Ligue 2 na sasa inapambana isishuke tena daraja ikishiriki Ligi Daraja la Tatu Ufaransa.

Lilepo, ambaye mkataba wake na Valenciennes ulikuwa unamalizika Juni 30, 2026, alikuwa hana nafasi ya kutosha kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu huu wa 2024/25 akishiriki michezo tisa tu na ametoa asisti moja, lakini hakufunga bao lolote.

Kabla ya kufanya makubwa akiwa na Al Hilal, Lilepo alianzia maisha yake ya soka katika akademi ya AS Vita Club, baadae akaichezea FC Renaissance nayo ya nchini DR Congo kabla ya Florent Ibengé kumvuta kwa miamba hiyo ya soka la Sudan. Pia aliwahi kuitumikia Mbabane Swallows ya Eswatini kwa mkopo.

Ndani ya Kaizer Chiefs, Lilepo anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Mkongomani mwenzake, Christian Saile Basombili ambaye msimu huu amecheza mechi sita za ligi bila ya kufunga wala kutoa asisti.

Related Posts