WINGA wa Simba, Mzambia Joshua Mutale amepewa nafasi nyingine ya kuonyesha kile kilichopo miguuni mwake, baada ya mabosi wa klabu hiyo kuamua kumbakisha katika dirisha dogo tofauti na mipango iliyokuwapo awali ya kumchomoa kikosini.
Kwa sasa nyota huyo wa zamani wa Power Dynamos ana kibarua cha kusalia kikosini humo ama kujiondoa kwa kile atakachokionyesha duru la pili la Ligi Kuu Bara inayorejea tena mapema mwezi ujao.
Ipo hivi. Inaelezwa kipindi cha dirisha dogo la usajili, mabosi wa Simba walikaa kikao kuchambua uwezo wa kila mchezaji kujua nani akatwe na nani aongezwe kikosini, ilipofika zamu ya Joshua Mutale yakafanyika maamuzi ya kumpa nafasi ya pili, licha ya baadhi ya wajumbe kutaka achomolewe kikosini.
Taarifa za ndani kutoka Simba zinasema wakati anasajiliwa Mutale walitarajia angefanya makubwa na Kocha Fadlu Davids alimpa nafasi ya kucheza, lakini bado hakuonyesha kiwango kikubwa, ikiwamo kushindwa kufunga bao lolote wala kuasisti hadi sasa Ligi Kuu na hata michuano ya Kimataifa, kitu kilichowafanya wajumbe kutaka atemwe iletwe mashine ya maana.
Hata hivyo, baadhi ya vigogo inadaiwa walimkingia kifua ikizingatiwa umri alionao na kuwa kwake majeruhi mara kadhaa mbali na kutua kwa Ellie Mpanzu ikielezwa inaweza kuwa chachu ya kumfanya aongeze juhudi ili kujihakikishia namba kikosini.
“Amepewa nafasi ya pili kwa sababu alipata majeraha ya hapa na pale, hivyo maamuzi ya kusalia Simba ama kuondoka yapo mikononi mwake mwenyewe,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Simba inaposajili mchezaji mgeni inakuwa na matarajio ya kuja kuongeza chachu kikosini, ndiyo maana katika kikao kulijadiliwa mambo mengi na dirisha lijalo mtayaona mabadiliko kadha.”
Tangu Mutale ajiunge na Simba msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Power Dynamos ya Zambia, Ligi Kuu amecheza mechi 10 kwa dakika 438, hajafunga bao wala kutoa asisti.