Dar es Salaam. Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza amechambua ushindi wa Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kushindwa kwa Freeman Mbowe.
Mbowe amekuwa mwenyekiti wa Chadema kwa miaka 21. Baada ya kushindwa katika uchaguzi uliomalizika asubuhi ya jana Jumatano, Januari 22, 2025 alikubali matokeo. Lissu na Makamu wake bara, John Heche wanaanza safari wanayoiita ya mabadiliko.
Lissu anaingia madarakani sawia na Donald Trump ambaye Jumatatu ya Januari 21, 2025 aliapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani.
Upande mwingine, Stephen Wasira, mwanasiasa mkongwe ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anachaguliwa na mkutano mkuu wa chama hicho kuwa Makamu Mwenyekiti Bara. Uchaguzi huo uliofanyika Januari 18, 2025 jijini Dodoma.
Katikati ya yote hayo, Askofu Bagonza anaandika tafakuri kuchambua na anachokiona juu ya viongozi hao akinasibisha na aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ambaye alifariki dunia Septemba 6, 2019. Mugabe aliliongoza Taifa hilo kwa miongo mitatu hadi alipoondolewa madarakani kwa njia ya Mapinduzi ya kijeshi Novemba 2017.
Tafakuri hiyo ya Askofu Bagonza ameipa kichwa cha habari ‘Mbowe siyo Mugabe na Tundu Lissu siyo Trump.’ Soma andiko lenyewe lilivyo.
Naandika kupongeza. Sina pole za kutoa.
Nawapongeza Mwenyekiti Tundu Lissu na makamu wake, mtani wangu John Heche. Hata mimi siamini kama mmeshinda lakini sina pa kukata rufaa. Mwaka huu nina bahati sana. Makamu wote wa vyama vikubwa ni watani wangu: Wasira na Heche. Kuna nini hapa? Najiteua kuwa mpatanishi siku wakigombana.
Nampongeza Mbowe. Ameshinda kuliko alivyoshindwa. Ametufundisha sote. Kukubali matokeo hutokana na mchakato uliojaa uhuru, uwazi na haki. Tuzo ya MO Ibrahim inamhusu lakini iwe na bahasha nzito, siyo kupewa ubao tu.
Nampongeza Frank Mwakajoka na John Mnyika kwa kusimamia vizuri uchaguzi usiku kucha. Hakuna kazi mbaya kama kusimamia uchaguzi. Muulizeni Mzee Damian Lubuva! Baada ya pongezi, nibwabwaje haya:
1. Mbowe siyo Mugabe kwa sababu Mugabe hakuwahi kushinda wala kushindwa uchaguzi. Daima aliamua apate kura ngapi.
2. Mbowe siyo Mugabe wala wale wote waliowahi kukaa madarakani muda mrefu.
– Nilikuwapo wakati wa JKN; kama angegombea 1985, angeshinda.
– Nilikuwapo mwishoni mwa Mzee Ruksa (Hayati Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi), Hayati Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Hayati John Magufuli (JPM) (Atake Asitake), na hata sasa nipo na Mama, Chifu Hangaya. Wote hawa wangegombea baada ya vipindi vyao kwisha, bado wangeshinda! Mbowe ameshindwa na amekubali matokeo. Yeye ni zaidi ya “Bwawa Darasa” la siasa hapa nchini.
2. Mbowe si Mugabe. Jamani! si rahisi kumshinda aliye kitini. Mjinga mmoja wa chama kingine kaniandikia, “Mwamba kaamua tu kumlegezea mropokaji; angeamua kubaki wangemfanya nini?”
Nami nikamjibu, “waulize waliowahi kuamua kubaki. Kutoka kujadiliwa na baraza la mawaziri hadi kutojadiliwa na baraza la madiwani!” Huko si kuanguka ni kuporomoka. Mbowe kathibitisha umwamba wake.
3. Tundu Lissu siyo Trump. Wanafanana ukali wa maneno si ujinga wa kisiasa. Wote walipigwa risasi, zikawaongezea kura zao. Wapinzani wa Lissu ndani ya CDM wakapuuza risasi zake na kumuongezea huruma. Lissu ni hukumu isiyo na rufaa kwa watawala wanaotumia risasi badala ya hoja. Rudisheni risasi mfukoni, nendeni shule mjifunze hoja. Wamarekani walitumia risasi, sasa wanaongozwa na “kichaa mstaarabu”.
4. Tundu Lissu siyo Trump. Kwa Trump mihimili inajitegemea na ina nguvu. Hapa kwetu, mihimili inamtegemea Lisu aiseemee na kuisimanga. Mmemsahau Spika Makinda? “Mwanangu Lissu, hebu tusaidie tuondoke hapo jamani”. Natamani Dk Ackson Tulia atulie mbele ya Spika mstaafu Anna Makinda apate twisheni ya kufanya kazi na Lisu.
5. Tundu Lissu na Freeman wameelewana. Wapambe wao wamenuniana. Tatizo lilikuwa moja. Tundu Lisu aliwamudu na kuwaendesha wapambe; Mwamba wapambe walimumudu na kumwendesha. Wote wawili ni somo kwetu: Wapambe wanaweza kukuambia wakati gani kuingia uwanjani (Lissu), lakini hawawezi kukuambia wakati gani utoke uwanjani (Mwamba).
6. Mbowe amefuta makosa yake yooote ya miaka 21 kwa kubonyesha kitufe kimoja tu: Kukubali matokeo. Lissu kachukua mkopo mkuuubwa wenye riba kubwa wakati kazungukwa na vibaka. Atamudu kurejesha mkopo huu? Neno kwa Mbowe: Ukistaafu, ustaafu. Neno kwa Lissu: Mahaba ya kutongozea na kuolea ni tofauti na mahaba ya kuishi katika ndoa.
8. Wanachadema na Watanzania: Msiyemtaka kaja. Mliyemtaka kaja. Tuna taifa la kutunza na kustawisha. Mambo yetu hayako sawa. Walio madarakani wananung’unika. Walio nje wananungunika. Wageni wananungunika. Wawekezaji wananungunika. Tusifanye maridhiano ili hii hali iendelee. Turidhiane kuondoa hali hii. Watawala wa zamu, msipuuze watu kulala sakafuni mlimani City. Kuna kitu ndani yao.
9. Wako wenye mashaka na Lissu. Nami nimo. Tulio na mashaka tuna bahati moja: Hatuhitaji kumharibia Tundu Lissu. Yeye ana uwezo mkubwa wa kujiharibia. Tumuombee.
10. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa CCM kumaliza mkutano wake na CDM kuhitimisha uchaguzi wa ndani, taifa linaweza kuwa tayari limempata rais, chama tawala na chama kikuu cha upinzani. Penye CCM waweza kuweka CDM na penye CDM waweza kuweka CCM bila kuathiri maana ya nisemacho.
Haki inaunganisha, dhuluma inaligawa taifa. Salaam nyingi kutoka barafu za milima ya Ufaransa na Ujerumani.