Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, imeiagiza Serikali kuingia makubalino na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) maarufu Selian, ili ianze kupeleka ruzuku ikiwemo kuwapatia wahudumu wa afya vifaa tiba pamoja na dawa.
Maagizo hayo yametolewa leo Alhamisi, Januari 23, 2025 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Dk Elibariki Kingu wakati kamati hiyo ya Bunge ilipokutana na uongozi wa hospitali hiyo jijini Arusha.
Kwa muda mrefu ombi kwa Serikali kuwa na ubia na Hospitali ya Kanisa la KKKT ya Selian, lilikuwa na lengo la kuiokoa, kulinda ajira pamoja na kuongeza wigo wa huduma wakati wa mashindano ya Afcon na huduma za utalii.
Dk Kingu amesema katika kikao hicho wamepokea hoja kuhusu na mwenendo wa hospitali hiyo na kamati baada ya kuwa imepitia maoni waliyoyatoa na yale ya wajumbe, imeazimia hayo.
“Kamati inaiagiza Serikali kufanya haraka kuingia makubalino kati ya serikali na hospitali ili ianze kupeleka ruzuku ikiwemo kuwapatia wahudumu wa afya vifaa tiba pamoja na dawa, ikizingatiwa hospitali hiyo imekuwa kama nembo ya mkoa wa Arusha.
“Tumeona kwenye takwimu inapokea asilimia 85 ya wagonjwa wanaotibiwa kupitia mfuko wetu wa bima ya afya ya NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya),” amesema Dk Kingu.
Amesema Serikali inatakiwa kutekeleza hilo kabla Bunge la bajeti halijaanza, kamati ipatiwe taarifa ya hatua za utekelezaji wa kusaini makubaliano kati yake na kanisa na kamati ipate ripoti mapema.
Dk Kingu amesema pia kamati inashauri wasimamizi wa hospitali ambao ni kanisa, mifumo iliyofungwa kwenye Hospitali ya KCMC iliyoweza kudhibiti ubadhirifu na upotevu wa fedha na kuiwezesha kuwa na mapato ya Sh2.5 bilioni kwa mwezi, ifungwe pia Serian.
“Mifumo ya afya ikafungwe ambayo haitaruhusu mtu kupokea fedha taslimu, tunataka mifumo ya hospitali iwe ya kidijitali ni maelekezo ya kamati, tuna wajibu wa kusimamia kuona ufanisi na katika sehemu ambayo Serikali inafikiria kuwa na ubia,” amesema na kuongeza;
“Waziri wewe ni shahidi hospitali yetu inakusanya Sh2.5 bilioni kila mwezi kwa sababu wamefunga mifumo. Kwanini KCMC ifanye vizuri na Serian isifanye vizuri? Tunaagiza mifumo ya afya ikaimarishwe ili kuhakikisha mapato ya hospitali yanaokolewa.”
Pamoja na hayo kamati ilitoa maelekezo kwa NHIF wakutane na Serian kuangalia uwezekano wa kuwakopesha vifaa tiba na mashine ya uchunguzi wa magonjwa ya MRI.
“Tunaomba haraka tupate majibu kabla ya Bunge la mwezi wa tatu, tuone kwamba usitishwaji wa ile mashine binafsi, serikali iangalie namna ya kuwasaidia hospitali hii iweze kukopeshwa mashine ya CT Scan na vifaa vingine muhimu ili kuweza kuleta ufanisi wa hospitali,” amesema.
Pamoja na hayo Kamati ya Bunge iliielekeza serikali kuhakikisha watumishi wote ambao watapelekwa katika hospitali ya Serian wawe na weledi, uwezo na uzoefu wa kutosha ikizingatiwa mji wa Arusha ni wa kitalii na unakwenda kupokea mashindano ya Afcon yatakayofanyika mwaka 2027.
“Kwa mujibu wa uwekezaji mkubwa uliofanywa na kanisa kwa majengo na mindombinu hatuoni haja kwa serikali kwenda kujenga hospitali nyingine ya kanda, tunaweza tukawezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na miundombinu kuhakikisha hospitali hii inakuwa mbadala kama ilivyo KCMC, Bugando na hospitali zingine za rufaa,” amesema Kingu.