Kocha ASEC aichambua Simba, afichua siri nzito

WAKATI mashabiki wa Simba wakisubiria kwa hamu droo ya mechi za robo fainali za Kombe la Shirikisho Afrika ili kujua timu yao itapangwa na nani kuitafuta nusu fainali, timu hiyo imeonekana kuwa tishio.

Simba iliyofuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuongoza kundi A, inaweza kupangwa kucheza na timu mojawapo kati ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, Stallenbosch (Afrika Kusini) na Al Masry (Misri) zilizomaliza nafasi ya pili katika makundi ya B, C na D.

Kocha wa Asec Mimosas, Julien Chevalier ameichambua Simba kutokana na alivyoiona huku akifichua kwamba kati ya timu ambazo hatamani kukutana nayo robo fainali basi ni hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti Chevalier, amesema sababu kubwa ya kutotamani kabisa kukutana na Simba katika hatua hiyo ni kutokana na kuufahamu mziki wa Mnyama kila wanapokutana hasa kwa mechi za Kwa Mkapa.

Rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimewahi kukutana mara sita katika michuano tofauti ya CAF, ikiwamo mara mbili katika Kombe la Shirikisho na nne za Ligi ya Mabingwa, huku kila moja ikishinda mara mbili na nyingine mbili kumalizika kwa sare, mechi zote sita zikiwa ni za hatua ya makundi.

Safari hii kuna uwezekano wa kukutana tena katika Kombe la Shirikisho, lakini ni hatua ya robo fainali na Kocha Julie alisema moja kati ya kitu ambacho hakitamani hatua inayofuata ni kukutana na wapinzani wao hao.

“Simba ni timu kubwa nimeiona msimu huu, pia nimewahi kucheza nayo, haina utani kabisa katika michuano ya kimataifa. Ina kikosi hatari wala siyo cha kukibeza ukikutana nacho ni lazima ujipange vilivyo kwani ukicheza vibaya atakupiga ugenini na nyumbani,” alisema Julie na kuongeza.

“Kilichoongezeka msimu huu kwa Simba ni mastaa wakali wanaokifanya kikosi hicho kuwa kipana zaidi, pia kocha wake ni mpya na falsafa zake ni kubwa.”

Alisema  kati ya timu tatu kati ya nne zilizoongoza makundi ya michuano ya msimu huu, ikiwamo watetezi, Zamalek na RS Berkane pamoja Simba, anaona ni heri akutane na timu hizo nyingine na sio Mnyama kwani wanaujua mziki wake Kwa Mkapa, pia ni timu yenye uzoefu na mechi kubwa za maamuzi.

“Kuna Zamalek na Berkane, kwangu mimi bora timu moja kati ya hizi na siyo Simba, tumewahi kucheza nao kwa Mkapa, tunajua walivyo.”

Hata hivyo, licha ya kauli hizo bado Simba haipaswi kubweteka kwani Asec ambayo imekuwa ikizalisha mastaa kadhaa wakubwa imekuwa na matokeo mazuri ikiwa nyumbani dhidi ya Simba, kwa kutopoteza na mara ya mwisho msimu uliopita ilitoka suluhu, baada ya awali kutoka sare ya 1-1 Kwa Mkapa.

Katika mechi mbili za nyumbani Asec imeifunga Simba kwa 3-0 na 4-3, wakati ilipoteza ugenini mbele ya Mnyama kwa wa 3-1 na 1-0 ikiwa ni wastani mzuri wa mabao kwani imevuna mabao tisa dhidi ya saba katika mechi hizo sita zilizochezwa 2003, 2022, 2023 na 2024.

Huu ni msimu wa sita kati ya saba Simba inafanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF ikiwa ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano kwa sasa.

Simba ambayo imebaki kuwa timu pekee kwenye michuano ya Caf ikiiwakilisha Tanzania msimu huu, hatua ya makundi imefanikiwa kushinda mechi zote tatu za nyumbani ilizocheza Kwa Mkapa, huku ugenini ikishinda moja, sare moja na kupoteza moja ikimaliza na pointi 13 juu ya CS Constantine ya Algeria iliyokuwa na 12.

Related Posts