Kumekucha! Yanga kubomoa kamati ya mashindano

BAADA tu ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, vigogo wa Yanga waliitana haraka na kufanya tathmini ya kile ambacho kimewakwamisha na kupitia kikao hicho yapo waliyoyabaini na kuna maamuzi walichukua, ikiwamo kuigusa kamati ya mashindano ya klabu hiyo.

Kwanza kwa pamoja walikubaliana kwamba timu yao ilistahili kupata ushindi dhidi ya MC Alger ya Algeria katika mechi ya mwisho ya makundi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wikiendi iliyopita ambayo iliwakwamisha kumaliza nafasi ya pili kwa Kundi A na kuvuka kwenda robo fainali.

Pili waligundua utaratibu wa wachezaji kufanya mazoezi wakitokea nyumbani na kisha kukutana siku chache kabla ya mechi unawapa uhuru uliopitiliza ambao unaleta athari hasi kwa timu.

Kutokana na hilo, klabu hiyo imepanga kufanya mambo mawili ambayo inaamini yatakuwa suluhisho kwa siku za usoni.

Jambo la kwanza ambalo imeamua kulifanya ni kufanya maboresho ya kamati ya mashindano na kuna baadhi ya watu itawapunguza na wengine kuongezwa ili kuipa nguvu zaidi.

“Ni maboresho ya kawaida ambayo yamekuwa yakifanyika mara kadhaa pindi msimu unapomalizika au pale na uongozi unaona kuna sehemu inayumba hivyo wala sio jambo la ajabu au la kushangaza kwa vile lengo ni timu ifanye vizuri,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga.

Timu hiyo pia imeamua kurudisha utaratibu wa kambi kwa wachezaji wake ambayo itaanza rasmi leo huko Avic Town Kigamboni.

“Wachezaji wataingia kambini kesho (leo) na itakuwa endelevu tofauti na zamani na walikuwa wakitokea nyumbani na kisha kukutana siku chache kabla ya mechi,” kilisema chanzo hicho.

Related Posts