Kwa heri Chadema ya Mbowe siasa, karibu Lissu

Mashambulizi ya jicho kwa jicho na kuvuana nguo. Vita ya maneno na mabadilishano ya ahadi kuhusu kesho ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kilikuwa kipindi pevu cha mnyukano, hatimaye tamati imefikiwa na mwanzo mpya umezaliwa.

Tundu Lissu ndiye Mwenyekiti wa Chadema na Freeman Mbowe, anavaa cheo kipya, mwenyekiti mstaafu.

Tamthiliya, vioja na ngebe za uchaguzi, sasa mwisho. Hiki ni kipindi ndugu wawili pacha; “Yaliyopita si ndwele” na “tugange yajayo”, huitwa kuponya majeraha ya kampeni.

Ushindi wa Lissu ambao umetokana na kura asilimia 51.5 za wajumbe wote na kushindwa kwa Mbowe aliyevuna asilimia 48.3, kumetengeneza viulizo vingi kuhusu hatima ya Chadema.

 Chama kitakuwa na uelekeo gani bila Mbowe? Lissu atajenga ‘shepu’ ipi ya kisiasa Chadema?

Wakati wa mkutano mkuu na hata Baraza Kuu Chadema, ungewaona Lissu na Mbowe, wakitabasamu kama watu wenye kupendana.

Hali halisi ni kuwa nyuso zao, hata maneno waliyotamka kwenye mkusanyiko, ni mbali kabisa na kitovu cha ukweli. Tayari kuna chuki, swali ni je, itamalizwaje?

Chuki haiishii tu kwa Mbowe na Lissu, bali pia timu zao. Lissu hana chaguo zaidi ya kuongoza chama ambacho sehemu kubwa ya safu ya uongozi inampinga. Ushauri, Lissu asome kitabu “Team of Rivals; The Political Genius of Abraham Lincoln,”kilichoandikwa na mwanahistoria Doris Goodwin.

Kitabu hicho, kinaeleza kinagaubaga jinsi Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alivyoweza kufanya kazi kwa mafanikio na watu waliokuwa mahasimu wake kwenye uchaguzi.

Pengine Lissu akajifunza. Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, sehemu kubwa ya maarifa yake ya kiuongozi, yalijengwa na kitabu hicho.

Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, jina lake linakuja haraka wakati wowote unapotafakari aina ya mahasimu ambao Lissu atatakiwa kufanya nao kazi. Je, itawezekana au zinakuja zama za kukamiana na kufukuzana?

Ukifuatilia hoja za Lissu, hatua kwa hatua, vilevile watu waliokuwa wakimuunga mkono katika mbio zake za kuwania uenyekiti, jina la Wenje limesikika mara nyingi kama ndiye chanzo kikuu cha mtifuano Chadema. Ukiweka maneno kwenye chujio la ukweli, unapata jibu kwamba Lissu na Wenje walikuwa timu moja, wakageukana.

Lissu alipata kusema kuwa hakuwa na mpango wa kugombea uenyekiti dhidi ya Mbowe, isipokuwa alifanya hivyo baada ya kuona alitakiwa kushindana na Wenje kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

Lissu amekuwa akimpa tuhuma nzito Wenje kuwa ni dalali, anayefanikisha viongozi wa Chadema kuhongwa fedha.

Wenje, ameshindwa kwenye kinyang’anyiro cha umakamu mwenyekiti dhidi ya John Heche. Pamoja na hivyo, cheo chake cha uenyekiti wa Kanda ya Victoria, kinampa hadhi ya ujumbe wa Kamati Kuu Chadema, ambayo Lissu ataiongoza. Wasiwasi ni mkubwa jinsi watakavyochukuana na kufanya kazi.

Kipindi cha kampeni, mwanachama mwandamizi wa Chadema, Godbless Lema alisimama na Lissu. Lema alisema, kama Chadema ingekuwa inaongozwa kwa misingi madhubuti, Wenje hakutakiwa kuwa mwanachama wa Chadema. Je, baada ya ushindi wa Lissu, usalama wa Wenje kwenye chama upo kiasi gani?

Kamati Kuu ya chama cha siasa, kwa kawaida ndiyo chombo kinachoundwa na viongozi wa daraja la juu. Katika vyama vya Kikomunisti Kamati Kuu huitwa Politburo au Political Bureau. Chadema chini ya Lissu, tabaka la juu la viongozi wanaounda Politburo.

Wajumbe wengi wa Politburo ya Chadema, walikuwa na Mbowe. Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi “Sugu”, Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi, Dickson Matata, Mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Devotha Minja, hao kutaja wachache, wote ni timu ya Mbowe.

Katika salamu zake kwa Mkutano Mkuu Chadema, Mbowe aliwataka viongozi wapya kutibu majeraha ya uchaguzi. Lissu ameahidi kutekeleza hilo.

Uchambuzi wa awali ulikuwa wazi, kwamba Mbowe alikuwa akiungwa mkono na sehemu kubwa ya safu ya uongozi.

Upepo uliokuwa unavuma nje ya chama kusindikiza jina la Lissu, uliwazidi nguvu viongozi wote. Wanaharakati na watumia mitandao kwa wingi wao, walisema wanamtaka Lissu. Mwanzoni, ilionekana wana-Chadema, hususan wapigakura wa mkutano mkuu walikuwa na Mbowe.

Kilichomkuta Mbowe, kisiasa, ni matokeo ya nadharia inayoitwa “bandwagon Effect” – “athari ya mkumbo”.

Tangu Lissu alipotangaza nia ya kuwania uenyekiti Chadema, aligeuka bandwagon. Ikawa fasheni kumuunga mkono. Waliompinga wakaitwa machawa, yaani watu wanaojipendekeza.

Mitandaoni, Lissu akiwa bandwagon, Mbowe alikumbwa na matokeo ya nadharia ya “underdog effect” – “Athari ya mgombea dhaifu.” Waliojilipua kumtetea Mbowe, walikuwa wapweke mitandaoni. Viongozi wa Chadema walishindwa kulisoma hilo na kulifanyia kazi haraka.

Kampeni ikapigwa mitandaoni, kwamba Mbowe akichaguliwa Chadema ingekufa. Wajumbe wengi, hata kama walikuwa wakimuunga mkono Mbowe, lakini hofu ya chama chao kufa wasingeibeba kiholela. Wanaharakati na mitandao imeamua mshindi. Wajumbe wa Mkutano Mkuu Chadema na wanachama wengi, waliendeshwa na wakaendesheka.

Timu ya Mbowe inaamini Lissu hana uwezo wa kuongoza chama, ila ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa. Watakutana kwenye vikao vya Politburo, mnyukano utakuwaje ikiwa hawaungani mkono wala kuaminiana?

Mbowe, ameongoza Chadema kwa miaka 21. Amekuwa akifanya siasa katika majira tofauti. Kuongoza maandamano na vuguvugu mbalimbali zilizogharimu uhuru wake mara nyingi. Maisha ya mahabusu hadi kuhukumiwa kifungo jela au faini. Pamoja na hivyo, siku zote, mlango wa maridhiano ulipofunguliwa, Mbowe aliukimbilia.

Inawezekana Mbowe anapenda maridhiano kwa sababu anajua athari za vurugu. Alisema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu: “Amani ni kitu adhimu sana. Kama umepitia vita, oparesheni na mapigano, unahitaji amani.”

Mbowe amekuwa mwenyekiti Chadema, kipindi vijana watatu waliuawa kwenye maandamano Arusha mwaka 2011.

Mbowe aliongoza maandamano Dar es Salaam, Februari 16, 2018, ikawa sababu ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, kuuawa kwa risasi.

Mbowe akiwa mwenyekiti wa  Chadema, chama hicho kilifanya maandamano yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa, Iringa, ambayo ni sababu ya kifo cha mwandishi wa habari, Daud Mwangosi, Septemba Pili, 2012. Ongeza matukio mengine mengi. Inawezekana Mbowe anajua athari, ndiyo maana huchagua maridhiano.

Upepo mkali uliovuma kumsindikiza Lissu kwenye kiti cha mwenyekiti Chadema, unaharamisha maridhiano.

Hivyo, Chadema mpya chini ya Lissu, inatarajiwa kutembea na falsafa ya jino kwa jino au ngangari na ngunguri, ambazo hazikuwahi kukisaidia Chama cha Wananchi (Cuf), wakati kikiwa kinaongoza upinzani Tanzania.

Mbowe alikuwa na sifa kubwa ya kusuka mikakati, ambayo imewezesha chama kufika kilipo. Timu Mbowe, ambao ni sehemu ya viongozi waliopo Kamati Kuu, wanaamini Lissu siyo mtu wa mikakati, kwa hiyo chama kitapoteza nguvu haraka.

Mbowe alikuwa mwenye kujitolea rasilimali zake binafsi kujenga chama. Hata Mkutano Mkuu Chadema na Baraza Kuu, ambayo bajeti yake inatajwa kufika Sh600 milioni, zimetoka kwa Mbowe, wakati Lissu mchango wa Sh30 milioni hakufanikisha.

Uendeshaji wa chama cha siasa unahitaji mtandao wa kifedha. Timu ya Mbowe inaamini Lissu hana mtandao wa kifedha. Wanasema kuwa mkutano mkuu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2025, utakuwa aibu, kwani chama hakitapata fedha za kuugharamia na Mbowe atakuwa pembeni  akiimba wimbo.

Ushiriki wa Chadema Uchaguzi Mkuu 2025, unatazamwa kwa macho tofauti. Timu inayomuunga mkono Mbowe inaamini Lissu atakata pumzi mapema, kuanzia kutafuta fedha za kampeni hadi kuunda mtandao wa wagombea ubunge, madiwani.

Kubwa ni fedha. Afrika, historia inaonesha kuwa upepo hutengeneza mkumbo (bandwagon).

Lissu, jinsi anavyoungwa mkono na wanaharakati, endapo atasimamishwa mwenyewe kuwa mgombea urais, anaweza kusababisha ushindani mkubwa dhidi ya CCM.

Kinaitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, uchaguzi wa viongozi wake mwaka 2024 na 2025, umethibitisha kuwa chama hicho kweli ni cha kidemokrasia.

Mwisho wa Mbowe haukupaswa kuwa wa angusho la uchaguzi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.

Hata hivyo, kuondoka kwake kunampambanua kuwa kiongozi aliyeweka misingi ya kidemokrasia na kuiheshimu.

Uchaguzi wa viongozi Chadema umekuwa huru, haki, wazi na wenye kuaminika. Kila mtu anaisifu Chadema.  Sifa hizo kwa wino uliokoza, ziende kwa Mbowe.

Mwaka 2004, Mbowe alipoingia ofisini kama mwenyekiti, chama kilikuwa na jengo dogo la makao makuu, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Saalam.

Sasa hivi, Chadema wana jengo kubwa Mikocheni, Dar es Salaam. Ukijumlisha na mtandao wa chama ulionea nchi nzima, kazi kubwa aliyoifanya kuvumbua vipaji vya viongozi na kuwakuza, heshima ya Mbowe kisiasa ni ya kudumu.

Related Posts