Liang na Chupaza kortini kwa madai ya kukutwa na kobe 104

Dar es Salaam. Raia wa China, Liang Zhou Liang (37) na Happyphania Chupaza (31) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la kukutwa kobe 104, kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na kobe hao 104 wenye thamani ya Sh 18 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Alhamisi Januari 23, 2025 na wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swallo.

Wakili Mafuru amedai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumo namba 2072/2025.

Hata hivyo, kabla kusomewa shtaka hilo, Hakimu Swallo aliwaambia washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote Mahakamani hapo kwa kuwa Mahakaka ya Kisutu haina Mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Baada ya kutoa maelezo hayo, washtakiwa hao walisomewa shtaka lao.

Mafuru alidai washtakiwa wanadaiwa kukutwa na nyara za Serikali isivyohalali kinyume na kifungu 86(1) na (2)b cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2022 ikisomwa kwa pamoja na Aya ya 14 ya jedwali la kwanza na kifungu 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akiwasomea shtaka lao, wakili Mafuru alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa lao, Januari 16, 2025 eneo la Mwanzo Mgumu, Samangila, wilaya ya Kigamboni.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na kobe 104 wenye thamani ya dola za marekani USD 7280 ambazo ni sawa na Sh18, 022,950 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao waliomba dhamana na hakimu Swallo alitoa masharti matano ya dhamana dhidi ya washtakiwa hao.

Moja alitaka kila mshtakiwa kuwasilisha fedha taslimu au mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 4.5milioni.

Pia, kila mshtakiwa anatakiwa awe na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoa Serikali za Mitaa au kama ni mwajiriwa, basi awe na barua ya utambulisho.

Sharti ya tatu, wadhamini hao wanatakiwa wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida) au kitambulisho cha Mpiga Kura.

Sharti ya nne, washtakiwa wanatakiwa kuwasilisha mahakamani hapo hati zao za kusafiria.

Vilevile, washtakiwa hao hawatakiwi kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.

Hata hivyo washtakiwa hao walifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa kwa dhamana.

Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 kwa kutajwa.

Related Posts