Mawakili walivyorushiana mpira, Dk Slaa kuendelea kusota mahabusu

Dar es Salaam. Wakati mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbrod Slaa akiendelea kusota mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi ya jinai, mawakili wanaomtetea na mawakili wa Serikali wamerushiana mpira kila upande ukiutuhumu kuwa chanzo cha mwanasiasa huyo kupelekwa mahabusu na kuchelewesha kuamua hatima ya dhamana yake.

Mawakili hao wamerushiana mpira huo, leo Alhamisi, Januari 23, 2025, wakati wa usikilizwaji wa shauri la mapitio alilolifungua Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kuhusiana na hatima ya dhamana yake hiyo.

Dk Slaa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar e Salaam, akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka linalomkabili, Januari 10, 2025 akidaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tangu siku hiyo amekuwa akihifadhiwa katika mahabusu ya Gereza la Keko amabako mpaka leo amekaa kwa siku 13, akisubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa shauri la maombi ya Jamhuri ya kupinga kupewa dhamana.

Hata hivyo, kupitia jopo la mawakili wake amefungua mashauri mawili ya maombi ya Jinai Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, moja kuhusiana na hatima ya dhamana yake na lingine akihoji uhalali wa shtaka linalomkabili.

Katika shauri hilo la maombi ya jinai namba 1637/2025, linalohusiana na hatima ya dhamana yake, Dk Slaa anapinga uamuzi wa Hakimu Nyaki kutokumpa dhamana kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya Jamhuri ya kupinga dhamana yake.

Kwa mujibu wa hati ya maombi anaiomba mahakama iitishe kwa mwenendo wa shauri la maombi madogo yaliyowasilishwa na Jamhuri katika Mahakama ya Kisutu, maombi namba 1015/2025 ya kupinga dhamana ya Dk Slaa kwa ukaguzi na marejeo.

Pia anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa Hakimu Nyaki hastahili kuendelea na kesi hiyo, kwamba amewekwa katika mahabusu ya Gereza la Keko kwa amri ya Mahakama isivyo halali.

Vilevile anaiomba mahakama itamke kuwa mwenendo wote wa shauri hilo tangu siku ya kwanza mpaka ulipoishia umegubikwa na nia ovu, uzembe, na upendeleo ambo huathiri haki ya uhuru wa mteja wao moja kwa moja.

Kisha anaiomba mahakama hiyo itoe maelekezo kwa Hakimu Nyaki kuwa maombi ya mshtakiwa yeyote kuhusiana na uhuru wake yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanagusa haki ya msingi, haki ya kwenda popte na haki ya kufanya kazi.

Shauri hilo limesikilizwa leo mbele ya Jaji Anold Kirekiano ambapo mawakili wa mwombaji umefafanua kile wanachokiita kasoro katika mwenendo wa shauri la maombi ya kupinga dhamana katika Mahakama ya Kisutu.

Pamoja na mambo mengine mawakili hao Hekima Mwasipu, Peter Madeleka, Edison Kilatu na Paul Kisabo wamsmedai kuwa Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki anayesikiliza kesi ya msingi inayomkabili Dk Slaa aliiendesha kwa hila na kwa ukiukwaji wa haki za msingi kinyume na Sheria na Katiba.

Wamedai ingawa shtaka lake linadhaminika lakini baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa umewasilisha maombi ya kupinga dhamana, Hakimu Nyaki hata bila kujiridhisha kama kweli shauri hilo liko katika mfumo wa Mahakama aliamuru mteja wao amepelekwe mahabusu.

Januari 13 siku ambapo shauri la Jamhuri lilikuwa limepangwa kusikilizwa mawakili wa Dk Slaa nao wakiibua pingamizi wakihoji uhalali wa mashtaka hayo, hivyo Hakimu Nyaki akaahirisha shauri hilo na kupanga kusikiliza pingamizi la Dk Slaa pamoja na shahidi la Serikali kupinga dhamana Januari 17.

Januari 17 baada ya kusikiliza pingamizi la Dk Slaa na kupanga Hakimu akaipanga kulitolea uamuzi Januari 23, upande wa mashtaka ulipendekeza usikilizwaji wa shauri lake la kupinga dhamana ufanyika baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa pingamizi la Dk Slaa kuhusu uhalali wa kesi (hati ya mashtaka).

Ingawa mawakili wa Dk Slaa alipinga wakisisitiza na shauri la Jamhuri lisikilizwe siku hiyohiyo Ili uamuzi utolewe pamoja kuokoa muda lakini Hakimu Nyaki alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka akamuru kuwa usikilizwaji wa shauri la kupinga dhamana utafanyika baada ya uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi.

“Kwa hiyo tunaialika mahakama yako iangalie amri hizo za uahirishwaji wa shauri hilo kama ulikuwa halali na sawa.Tunaomba mahakama irejewe Mwenendo huo na ikiona kasoro hizo tunazosema aachiwe huru kwa dhamana wakati kesi ya msingi inaendelea,” amesema Wakili Mwasipu baada ya kuelezea mtiririko wa matukio hayo.

Kwa upande wake Wakili Peter Madeleka amedai kuwawa kwa kuwa mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa linalodhaminika ilikuwa ni makosa Hakimu kumnyima dhamana kwa sababu nyinginezo zozote.

Amedai hata amri za kuahirishwa kwa shauri hilo zilizokuwa zinazotolewa na Hakimu Nyaki zilikuwa ni za kumnyima haki na kumkomoa.

Wakili Edson Kilatu amedai kuwa dhamana ni haki ya msingi ambayo haiwezi kukatishwa kwa namna yoyote ile isipokuwa kwa mujibu wa Sheria na katiba ya Nchi.

Amedai kilichofanywa na Mahakama ya Kisutu ni ukiukwaji wa iba13 (6) usikilizwaji sawa, kwa kusikiliza upande mmoja tu wa Jamhuri na kuamuru mteeja wao apelekwe mahabusu.

Wakili Paul Kisabo amedai kuwa kwa kuwa mteja wao anakabiliwa na shtaka linalodhanika alipaswa aachiliwe kwanza kwa dhamana ndipo Mahakama ingesikiliza hayo maombi ya kuzuia dhamana.

Akijibu hoja hizo Wakili Katuga pamoja na mambo mengine amsmedai kuwa kilichowasilishwa na mwombaji hatika hati za maombi yake na kilichozungumzwa na mawakili mahakamani ni mambo mawili tofauti.

Pia amedai kuwa hakuna ukiukwaji uliofanywa na Mahakama ya Kisutu na kwamba amri za kuahirishwa kwa shauri hilo zilikuwa zinatewa kwa mujibu wa Sheria.

Hata hivyo Katuga amedai kuwa hata wai hawafurahii kuona mtu anauestahili kupata dhamana anaendelea kukaa mahabusu huku wamewarishia mpira mawakili wa utetezi kuwa wao ndio wamesabisha mteja wao aendelee kukaa mahabusu.

Amedai kuwa mawakili hao walisilisha pingamizi kuhoji uhalali wa kesi ya msingi na kwamba kiutaratinu ilibidi shauri lao la kupinga dhamana lisimamie Ili kwanza lisikilizwe pingamizi lao na kwamba kabla ya kuamuriwa wakafungua maombi mengine Mahakama Kuu.

Na pale pingamizi linapoibuka ni utaratibu wa kawaida kusikiliza kwanza pingamizi.

“Pingamizi hilo pekee pengine lingeweza kutosha kulimaliza shauri na uamuzi wa pingamizi hilo ulikuwa umepangwa kutolewa leo, kuonesha kuwa uchelewaji unatokana na wao wenyewe,” amedai Katuga.

Hata hivyo, Wakili Madeleka amepinga vikali madai ya kuchelewesha hatima.ya dhamana ya mteja wao akidai kuwa sio wao walioweka pingamizi la kuzuia dhamana.

“Kwa hiyo siyo sisi tunaokwamisha bali wao ndio wanaokwamisha kinyume na sheria,” amesema Madeleka.

Jaji Kirekiano baada ya kusikiliza hoja za pande zote zmepanga kutoa uamuzi wake Jumatatu ya Januari 27, 2025 sa 4:00 asubuhi.

Related Posts