Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia Bangros Sikaluzwe (37), mkazi wa Ilolo, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kwa tuhuma za kujifanya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 22, 2025 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shaaban, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 22, 2025, saa 7:45 usiku katika msako uliofanyika Mtaa wa Majengo, mjini Tunduma, Wilaya ya Momba.
Akama amesema mtuhumiwa alikamatwa akiwa anafanya kazi za usalama barabarani katika barabara ya Tunduma-Sumbawanga kwa kuyapanga malori yanayovuka mpaka wa Tunduma kuelekea Zambia na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.
Ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa amevaa sare za polisi, pia, akiwa na vifaa vingine vya jeshi hilo kama pingu alizokuwa amezining’iniza kiunoni, kisu cha kukunja pamoja na tochi aliyokuwa ameshika mkononi.
Taarifa hiyo ya Kaimu Kamanda Akama imeeleza kuwa uchunguzi wa haraka ulibaini kuwa Bangros si askari polisi halali, bali ni mgambo aliyekuwa akijifanya askari kwa malengo ambayo bado hayajathibitishwa.
Katika tukio jingine, watu watatu wameuawa na watu wenye hasira kali wilayani Mbozi kwa tuhuma za wizi wa bajaji. Waliouawa kwa kuchomwa moto ni Steward Mwashiuya (28) na Musa Silumba (32) ambao walishambuliwa Januari 18, 2025 saa 7 mchana katika Mtaa wa BRN mnada wa zamani uliopo kata ya Ilolo, waliuawa.
Akama amesema marehemu mwingine ni Ombeni kayuni (22) ambaye katika Kijiji cha Old Vwawa, alishambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa kupigwa na wananchi kwa kutumia silaha za jadi na kupelekea kifo chake.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha tukio ni kwamba marehemu alikuwa anatuhumiwa kuiba bajaji maeneo ya Ilembo wilayani Mbozi na kukamatwa katika Kijiji cha Ikumbilo wilayani Ileje, akiwa na bajaji hiyo.
“Walipokuwa wanaelekea Kituo cha Polisi Vwawa, walipofika maeneo ya Old Vwawa, walimshambulia kwa kumpiga na kusababisha kifo chake,” amesema Kaimu Kamanda Akama katika taarifa yake.