MKONGO WA TAIFA KUINUA TEKNOLOJIA NA BIASHARA TANZANIA NA NCHI JIRANI

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia, na Habari imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua inayolenga kuboresha mawasiliano ya ndani na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi jirani, ikiwemo Kenya.

Akizungumza Januari 23, 2025, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia, na Habari, Jerry Silaa, alisema mkongo huo unajumuisha nyaya za mawasiliano zinazounganisha Tanzania na Kenya kupitia Horohoro hadi Mombasa, pamoja na kuunganishwa na mikongo ya chini ya bahari kupitia Dar es Salaam.

“Tunayo kilomita 13,991 za mkongo zilizokamilika, na tunalenga kufikisha kilomita 15,000 ifikapo Juni mwaka huu. Hii inawezekana kutokana na juhudi za serikali kuhakikisha TTCL inaimarisha huduma zake,” alisema Waziri Silaa.

Waziri Silaa alibainisha kuwa mradi huo umeweza kuunganisha wilaya 109 kati ya wilaya 139 za Tanzania, huku zabuni za kuunganisha wilaya zilizobaki zikiwa tayari zimetangazwa. Pia, alisema mkongo huo unaongeza uwezo wa mawasiliano ya kidigitali na kuboresha huduma za kiteknolojia nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema kuwa mkongo huo umewezesha Tanzania kuunganishwa na nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, na Malawi, hatua inayopanua fursa za biashara na mawasiliano.

“Mkongo huu utaimarisha mawasiliano ya kibiashara. Kupitia Mombasa, tutakuwa na njia mbadala za mikongo ya Dar es Salaam, hivyo kuongeza ufanisi wa mawasiliano,” alisema Marwa.

Marwa aliongeza kuwa mradi huu pia unapanua uwezo wa kusafirisha data, jambo linalosaidia maendeleo ya sekta za teknolojia, biashara, na uchumi kwa ujumla. Mradi huo unatarajiwa kuanza kazi rasmi Februari 1, 2025.

Kwa mafanikio haya, Tanzania inajiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Related Posts