Na Dulla Uwezo
Imeelezwa kuwa changamoto zilizokuwepo katika Mradi wa Maji wa Kemondo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, sasa huenda zikatatuliwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuletwa fedha nyingi katika mradi huo, na kwamba mkandarasi kwa sasa anafanya kazi kwa juhudi kubwa.
Hayo yamebainika katika Ziara ya Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Mathew Kundo aliyefika Mkoani Kagera Januari 23, 2025 katika eneo la Mradi huo na kujionea hali ya mradi, ikiwa ni takribani Miezi kadhaa imepita tangu afike eneo hilo la mradi na kuacha maelekezo.
Naibu Waziri Mathew amesema kuwa mpaka sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari kaleta Shilingi Bilioni 9 kati ya Bilioni 15.8 zilizopangwa kutekeleza mradi huo, na kwamba fedha hizo ndizo zimefanya mradi huo kufikia hatua ulipofikia na kikwazo kikubwa ni hali ya hewa na changamoto ndogo za mkandarasi ambazo tayari zimeshaanza kutatuliwa, hivyo Wananchi wa Wilaya ya Bukoba Wataendelea kupata Maji safi na Salama chini ya Wakala wa Maji Mjini na Vijijini Ruwasa.
Kwa sasa hali ya upatikanaji wa Maji Wilayani humo ni 74% huku Mradi wa Maji Kemondo ambao chanzo chake ni Ziwa Viktoria, endapo utakamilika utahudumia zaidi ya Watumia Maji Laki Moja, Umeanza kutekelezwa tangu Mwaka wa Fedha wa 2021/22 na Ukitekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya Kwanza ukiwa umefikia 96% na Awamu ya Pili ya kulaza na kusambaza mabomba ikiwa imefikia 75% na huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba Mwaka huu.