“Nguvu zaidi zinahitajika ulinzi Ghuba ya Chwaka”

Unguja. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema umefika wakati sasa kuongeza nguvu ya ulinzi katika Ghuba ya Chwaka kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wavuvi kuendelea na uharibifu wa hifadhi za bahari na rasilimali zake.

Ameyasema hayo Januari 23, 2025 Marumbi wakati wa uzinduzi na kukabidhi boti ya doria kwa ajili ya kamati ya usimamizi wa doria ya Ghuba ya Chwaka.

Ayoub amesema Serikali imefanya uamuzi wa kuzuia eneo hilo lisitumike kwa uvuvi wa nyavu na matumizi mengine ya uvuvi kutokana na jiografia ilivyo katika ghuba hiyo.         

Hata hivyo, amesema kutokana na ukubwa wa historia ya hifadhi ya Ghuba ya Chwaka chimbuko lake ni changamoto za kiuvuvi na upatikanaji wa mazao ya bahari katika ukanda huo, hivyo limekuwa jicho la serikali.

“Sisi tutatimiza wajibu wetu ndani ya wiki hii, hakuna mtu aliyeruhusiwa kuvua uvuvi haramu au eneo la hifadhi la Serikali hii mpaka sasa, kwa hiyo tutakuwa makini na wakali kulinda,” amesema.

Ameeleza Serikali ina azma ya kutatua changamoto za wavuvi wadogowadogo na ndio maana zinatolewa boti za kisasa katika uvuvi ambapo kwa ukanda wa kusini wamepewa boti 100 ili kuepusha uvuvi haramu.

“Kutokana na umuhimu wa kuhifadhi bahari, ni jambo la kisheria, hivyo wadau hao kutoa boti hiyo ni kuiunga mkono Serikali kupitia ushirikiano uliopo na ni chachu ya mafanikio kwa serikali kwani mashirikiano hayo ya wadau yanasaidia kubadili baadhi ya wananchi fikra na mienendo yao,” amesema.

Wakati huohuo, ametoa agizo kwa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi kukamilisha taratibu za eneo la Chamakangu kufungiwa kwa shughuli za uvuvi na kutumika kwa shughuli za utalii kwa ajili ya maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Bahari, Dk Makame Omar Makame amesema kwa kiasi kikubwa kamati ya usimamizi wa pamoja ya Ghuba Chwaka (CMG) imesaidia kuimarika kwa rasilimali za bahari, jambo ambalo limesaidia kuinua uchumi wa buluu kupitia sekta ya uvuvi na utalii kutokana na kuwepo kwa vivutio kwa wageni wanaofika katika huba hiyo.

“Kamati hiyo ni muhimu sana katika kufikia malengo ya serikali, kunahitaji kamati kushirikiana na kupata fursa ya kukaa pamoja na kujadiliana namna bora ya kutumia bahari ipasavyo,” amesema.

Vilevile, alitoa shukurani kwa kamati pamoja na Taasisi ya Mwambao (MCCC) kwa kuiunga mkono Serikali katika kuchangia kwa kiasi kikubwa katika masuala ya uhifadhi wa bahari na rasilimali zilizomo.

Amesema Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imepewa jukumu la kusimamia uvuvi na kuimarisha mazingira ya bahari kwa ajili ya maslahi ya wavuvi na watalii wanaoingia katika ghuba hiyo.

“Ili tuwe na uchumi wa buluu, lazima tuwe na usimamizi madhubuti wa kulinda rasilimali za bahari na uvuvi endelevu wenye kufuata sheria na kanuni za uvuvi za hapa nchini,” amesema.

Ametoa wito kwa kamati ya usimamizi baada ya makabidhiano ya boti hiyo kushirikiana na wananchi kupitia kamati za uvuvi, wadau wa maendeleo na vyombo vya ulinzi na usalama ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali.

“Boti hii ni chachu ya maendeleo kwa mkoa wa kusini endapo, itafanyiwa kazi kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa MCCC, Dk Said Khalid amesema MCCC kwa kushirikiana na idara ya maendeleo ya uvuvi pamoja na wanajamii wanafanya tathmini ya maeneo yaliyozunguka jamii husika kwa lengo la kuweka utaratibu wa matumizi mazuri katika hifadhi za bahari.

Dk Said amesema elimu zaidi itaendelea kutolewa kwa wanajamii ili kuleta faida kwa wavuvi katika kujiongezea kipato kupitia uhifadhi wa bahari.

Amesema vikundi 15 tayari vimepatiwa mafunzo ya uhifadhi wa bahari.

Ameitaka kamati ya usimamizi kuitunza na kuitumia vizuri boti hiyo kutokana na kuthibitika kwamba boti hiyo ina uwezo wa kuishi kwa muda wa miaka 20 bila ya kupata tatizo lolote.

Akizungumza kwa niaba ya wanakamati wa CMG, mwenyekiti katika Ghuba ya Chwaka, Muhsini Mohamed ameziomba taasisi husika kuwapatia bajeti ya kutosha ili wafanye kazi ya doria kwa ajili ya kupambana na wavuvi wanaokiuka utaratibu uliowekwa na serikali, jambo linalorudisha nyuma maendeleo katika ghuba hiyo.

Vilevile, amesema kupitia kamati ya CMG, imeziweka pamoja kamati za uvuvi za Ghuba ya Chwaka kwa lengo la kushirikiana na wavuvi katika utoaji wa elimu juu ya madhara yanayotokana na uvuvi haramu katika hifadhi za bahari.

Related Posts