BADO Klabu ya Pamba Jiji inaumiza kichwa namna ya kumalizana na mshambuliaji, Mghana Erick Okutu ambaye mwanzo ilielezwa angejiunga na KenGold dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu, lakini imeshindikana.
Wakati ishu ya Okutu ikiwa pasua kichwa, klabu hiyo imeachana na nyota sita kipindi cha dirisha dogo.
Awali, Mwanaspoti liliripoti kambi ya Okutu haikukubaliana na uamuzi wa mteja wao kutolewa kwa mkopo, isipokuwa kwa sharti moja la kuuvunja mkataba uliobaki wa miezi sita.
Okutu alinukuliwa akisema hana taarifa za kutolewa kwa mkopo kwani anachokifahamu bado ana mkataba wa miezi sita na kikosi hicho, huku akiweka wazi hana dhamira yoyote ya kuondoka labda itokee ofa kwa timu nyingine kutoka nje.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Ezekiel Ntibikeha, alisema klabu hiyo imekubali kukaa mezani na mchezaji huyo ili kupata muafaka wa namna ya kuvunja mkataba wake baada ya maingizo mapya dirisha dogo.
“Okutu tulikuwa na mpango wa kumpeleka kwa mkopo KenGold lakini mwishoni kabisa wenzetu wakaukataa ule uhamisho, tumeamua kukaa naye mezani tupate mwafaka lakini tutakuwa kwenye mazingira mazuri ya kumalizana naye,” alisema Ntibikeha.
Ntibikeha ambaye pia ni meneja wa Pamba Jiji, alisema kuwa katika dirisha dogo wamesajili wachezaji tisa na kuacha sita wakiwemo watatu waliopelekwa timu nyingine kwa mkopo akiwemo George Mpole aliyetimkia Kagera Sugar.
Aliwataja walioachwa ni John Mtobesya, Emmanuel Boateng (Ghana), Robert Kouyala (Togo) na Salim Kipemba.
“Tumemalizana nao kabisa baada ya kuona mwalimu ametoa mapendekezo yake na sisi tumejiridhisha ni kweli hawajapata nafasi kwa mechi 16 zilizopita, tukaona yawezekana kwa mechi hizi zinazofuata hatuwezi kuwatumia kwahiyo tulikaa nao mezani na kumalizana,” alisema Ntibikeha.