Samia aagiza fidia wanaopisha mradi Monduli kabla ya Februari

Monduli. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza fidia iliyotengwa kwa wananchi wa vijiji vinne waliopisha mradi wa magadi soda wilayani Monduli, mkoani Arusha, iwe imelipwa ifikapo Februari 15, 2025.

Serikali imetenga Sh14.48 bilioni kwa ajili ya ulipaji fidia hiyo na jumla ya wananchi 595 kutoka vijiji hivyo wananufaika.

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi Januari 23, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, kwa niaba ya Rais Samia, wakati wa uzinduzi wa ulipaji fidia uliofanyika katika Kijiji cha Engaruka, wilayani Monduli.

Vijiji vinavyohusika ni Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni.

Dk Jafo amesema, “Wananchi wote wanaoguswa na fidia wanapaswa kupewa haki yao ifikapo Februari 15, 2025. Malalamiko yoyote yahakikishe yanashughulikiwa kwa wakati, ili kila mmoja apate haki yake bila kudhulumiwa.”

Waziri Jafo amesema Rais Samia amesema lengo ni kuhakikisha mradi huo unatekelezwa huku haki za wananchi zikizingatiwa.

Waziri Jafo amesema awali, mradi huo haukutekelezwa kati ya mwaka 2004 na 2006 katika Ziwa Natron kutokana na changamoto za kimazingira.

Hata hivyo, Serikali imefanya tafiti za kina na kubaini kuwa eneo la Engaruka linafaa kwa utekelezaji bila kuathiri mazingira.

Amesema mradi huo unatarajiwa kupunguza gharama za uagizaji wa magadi soda kutoka nje ya nchi, huku ukitoa ajira kwa wananchi wa wilayani humo.

“Madini haya yatatumika katika sekta mbalimbali za viwandani, ikiwemo sabuni, nguo, na bidhaa za madini. Awamu ya kwanza ya mradi itahusisha viwanda viwili na tutaendelea kuchochea viwanda vingine,” amesema Waziri Jafo.

Amesema sekta ya viwanda na biashara kwa sasa inachangia asilimia 8 ya pato la Taifa, lengo ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 kupitia uwekezaji huo na miradi mingine ya viwanda.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, Geofrey Pinda amesema wizara yake itatekeleza mpango maalum wa upimaji wa vijiji hivyo na kuhakikisha matumizi bora ya ardhi, ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

“Nimemuelekeza Katibu Mkuu kuhakikisha Wilaya za Monduli na Longido zinaingizwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi,” amesema Naibu Waziri Pinda.

Pia, amesema wizara itashirikiana na wananchi ili kuhakikisha maeneo yao yatambuliwe sambamba na kuunda kamati za vijiji ambazo zitayatambua maeneo hayo.

“Hivyo zoezi la kwanza ni mipaka ya vijiji ili kazi iende kwa malengo ya serikali,”amesema.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema mali ghafi hiyo itakayozalishwa katika eneo hilo, inakwenda kunufaisha sekta mbalimbali.

Hivyo amewataka wananchi kutunza na kulinda amani ya mkoa huo na kuwatia moyo viongozi ili kuhakikisha wanaleta mabadiliko ya maendeleo.

Akizungumzia ajira, Makonda amesema Mkoa wa Arusha una tatizo la ajira lakini anaamini kupitia mradi huo, vijana wengi wazawa watapata ajira.

“Kumekuwa na tatizo la ajira kwa vijana wengi,naamini kupitia mradi huu wazawa watapata ajira na kunufaika na mradi,hicho ni moja ya  kipaumbele,wana uadilifu, uaminifu na uwezo wa kufanya kazi upo,” amesema Makonda.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dk Nicolaus Shombe amesema walifanya utafiti katika eneo hilo kati ya mwaka 2010/2013 na kubaini kiasi cha magadi soda yakiwa na mita za ujazo bilioni 3.8 sawa na tani milioni 787.

Hata hivyo, amesema mahitaji ya soko kipindi hicho yalikuwa ni tani milioni moja. Amesema  eneo hilo lina ukubwa wa hekari zaidi ya 60,000.

Hivyo, Dk Shombe amesema mradi huo ni zaidi ya mradi wa kimkakati na ni wa kielelezo ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa viwanda vinavyozalisha vinywaji, vioo, sabuni na nguo.

Related Posts