Mbeya. Zaidi ya wananchi 1,500 katika Kijiji cha Mashese kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wameondokana na gharama za matibabu baada ya serikali ya kijiji hicho kuwapatia bima.
Bima hizo zinatokana na mapato ya ndani ambapo mbali na wananchi wa kawaida, pia, wanafunzi watanufaika na katika mpango huo unaolenga kuhakikisha jamii hiyo inakuwa salama kiafya ili kuchochea maendeleo.
Akizungumza na Mwananchi Januari 22, 2025, mwenyekiti wa kijiji hicho, Osia Mwakalila amesema lengo lao ni kuona wananchi wake wanapata huduma hiyo ili kuondoa changamoto na kupunguza gharama za matibabu.
Amesema hatua hiyo ni baada ya vikao vya mara kwa mara na wananchi kuazimia kutumia mapato ya ndani kusaidia upatikanaji wa bima hizo na wengi vipato vyao kuwa vya chini.
“Tunachoomba serikali na wadau watusaidie kupata vifaa vya maabara katika zahanati yetu ya Ilungu ili kusaidia upatikanaji huduma, lengo letu ni kuona wananchi wote wanapata bima,” amesema Mwakalila.
Mmoja wa wananchi wanufaika na huduma hiyo, Mariam Mathayo ameishukuru serikali ya kijiji kwa mpango huo ambao umetekelezwa kupitia rasilimali za kijiji na kuhakikisha kwamba manufaa yanarudi kwa wananchi wenyewe.
“Hii ni njia nzuri ya kujali afya na maisha ya wananchi, tuipongeze na kuishukuru serikali kwa hatua hii, tunaanza kuwa na uhakika wa huduma muda wote na sehemu yoyote,” amesema Mariam.
Kwa upande wake, mganga mkuu wa zahanati hiyo, Dk Jafari Edward amesema uwepo wa bima za CHF kwa wananchi ni hatua muhimu kwa ustawi wa Jamii na amekanusha taarifa za wenye bima kutothaminiwa.
“Bima ya CHF iliyokatwa ni kwa ajili ya familia au kundi la watu sita kwa Sh30,000, lakini si kweli kwamba wenye bima hawathaminiwi hospitalini, niwapongeze kwa hatua hii kubwa,” amesema Dk Edward.
Naye mratibu wa bima hizo, Wilaya ya Mbeya, Francisco Nguvila amesema kilichofanywa na serikali ya kijiji hicho ni cha kuigwa katika maeneo mengine ili kuhakikisha jamii inakuwa na uhakika wa kupata huduma za afya na kuchochea maendeleo.
“Hiki kilichofanyika ni cha kuigwa hata maeneo mengine kwa kuwa wananchi wanaenda kuwa na uhakika wa huduma na kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja,” amesema Nguvila.