Singida. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema moja ya majukumu makuu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ni kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wale wasiojiweza. Amesisitiza kuwa mfuko huo unalenga kutatua changamoto zinazohusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi, kama vile kuboresha miundombinu ya barabara na vivuko ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23, 2025, baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kupitia mfuko huo mkoani Singida.
Amesema Serikali inalenga kupunguza umasikini kwa kuwasaidia kifedha wananchi wasiojiweza na kushughulikia changamoto za msingi zinazowakabili katika maeneo yao wanayoishi.
“Serikali ya CCM inalenga kuondoa umasikini kwa wananchi wake, hasa wale wasiojiweza kabisa kwa kuwasaidia kifedha. Vilevile, inatumia mfuko huu kuboresha maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kushughulikia changamoto kama za miundombinu ya barabara na nyinginezo,” amesema Simbachawene.
Aidha, amesema serikali kupitia Tasaf inajenga pia vituo vya afya maeneo ambayo hayakidhi kujengwa zahanati ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana, jambo ambalo ni sehemu ya mkakati wa kupambana na umasikini.
Waziri huyo amesema Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao unalenga kuwasaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, unatoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Amesema mpango huo unalenga kuboresha hali za maisha ya makundi hayo na kupunguza umasikini.
“Tuna mpango wa kutoa mikopo kwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu, kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ili kuwawezesha kiuchumi,” amesema.
Simbachawene ametaja pia mipango mingine ya serikali inayolenga kuwawezesha wananchi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa ruzuku ya pembejeo za kilimo, mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa shule za sekondari kila kata, shule za msingi kila kijiji, na huduma za matibabu bure kwa wazee.
Kauli ya Simbachawene imekuja kama majibu kwa kauli iliyotolewa Januari 21 na Freeman Mbowe, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye alionekana kubeza manufaa ya mfuko huo.