Tanzania kuanza kuzalisha kompyuta – MICHUZI BLOG

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TANZANIA iko mbioni kuwa na kiwanda kikubwa cha kutengeneza kompyuta mpakato (Laptop) kitakachozalisha kompyuta aina ya Tanzanite.

Aidha, nyingi ya komyuta hizo zitaelekezwa katika kukuza sekta ya TEHAMA kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Hayo yalibainika Bungeni jijini Dodoma jana wakati Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alipofanya wasilisho juu ya tume yake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, chini ya Mwenyekiti wake, Moshi Kakoso.

Mwasaga alisema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali kupitia Tume ya TEHAMA katika kuvutia uwekezaji na ujenzi wa vifaa vya TEHAMA nchini.

“Tuko pazuri. Tume imeshaitembelea kampuni ya QuadGen Wireless Solutions Pvt. Ltd ya Bangalore, India ili kujionea uwezo wao baada ya kampuni hiyo kuonesha utayari wa kuwekeza kiwanda kitakachotengeneza kompyuka mpakato na mfumo wa ubao janja kwa ajili ya kufundishia shule. 

“Tume inaendelea na mazungumzo na kampuni hii ili kuwezesha uwekezaji wa ubia  wa viwanda vya viwango vya SKD (kiwanda cha kuunda) na CKD (kiwanda cha kutengeneza) nchini Tanzania. Hii inaendana na shabaha iliyowekwa na Umoja wa Afrika kwa bara letu kuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa za TEHAMA,” alisema Dkt. Mwasaga.

 Hatua hiyo ilipongezwa na Kamati na kuisihi Tume ya TEHAMA kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa kama nchi, macho yote kwa sasa yapo katika mwelekeo wa kuujenga uchumi wa kidigitali kupitia kundi kubwa la vijana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Mhe. Moshi Kakoso alipongeza na kusisitiza kuwa, fursa kama hizo hazipaswi kuachiwa, bali zifanyiwe kazi ziweze kunufaisha nchi.

Alisema makosa kadhaa yalifanyika miaka ya nyuma baada ya wawekezaji kutaka kuzalisha bidhaa nchini, lakini wakaishia kuhamia nchi jirani.

Related Posts