Dodoma. Tanzania iko mbioni kuwa na kiwanda kikubwa cha kutengeneza kompyuta mpakato (Laptop) kitakachozalisha kompyuta aina ya Tanzanite.
Aidha, nyingi ya komyuta hizo zitaelekezwa katika kukuza sekta ya Tehama kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Hayo yalibainika Bungeni jijini Dodoma jana Jumatano, Januari 22, 2025 wakati Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga alipofanya wasilisho juu ya tume yake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, chini ya Mwenyekiti wake, Moshi Kakoso.
Mwasaga amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali kupitia Tume ya Tehama katika kuvutia uwekezaji na ujenzi wa vifaa vya Tehama nchini.
“Tuko pazuri. Tume imeshaitembelea kampuni ya QuadGen Wireless Solutions Pvt. Ltd ya Bangalore, India ili kujionea uwezo wao baada ya kampuni hiyo kuonesha utayari wa kuwekeza kiwanda kitakachotengeneza kompyuka mpakato na mfumo wa ubao janja kwa ajili ya kufundishia shule.
“Tume inaendelea na mazungumzo na kampuni hii ili kuwezesha uwekezaji wa ubia wa viwanda vya viwango vya SKD (kiwanda cha kuunda) na CKD (kiwanda cha kutengeneza) nchini Tanzania. Hii inaendana na shabaha iliyowekwa na Umoja wa Afrika kwa bara letu kuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa za Tehama,” amesema Dk Mwasaga.
Hatua hiyo ilipongezwa na Kamati na kuisihi Tume ya Tehama kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa kama nchi, macho yote kwa sasa yapo katika mwelekeo wa kuujenga uchumi wa kidigitali kupitia kundi kubwa la vijana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Moshi Kakoso alipongeza na kusisitiza fursa kama hizo hazipaswi kuachiwa, bali zifanyiwe kazi ziweze kunufaisha nchi.
Amesema makosa kadhaa yalifanyika miaka ya nyuma baada ya wawekezaji kutaka kuzalisha bidhaa nchini, lakini wakaishia kuhamia nchi jirani.
Mitaala 21 ya TEHAMA vyuoni yahakikiwa
Katika hatua nyingine, Tume ya Tehama nchini imehakiki mitaala 21 katika vyuo mbalimbali nchini.
Uhakiki huo, kwa mujibu wa Dk Mwasaga, unaangalia kama mitaala hiyo imetatua ombwe lililokuwepo kwa kutokuwepo kwa wataalamu wa teknolojia ibukizi kwenye soko la ajira nchini.
Amesema uhakiki huo na juhudi nyingine zinazofanywa na Serikali kupitia Tume ya Tehama, zinalenga katika kutoa elimu ya uhakika kwa Watanzania, hususani vijana ambao ndio walaji wakubwa wa sekta hiyo inayokua kwa kasi duniani.
Sambamba na hilo, amesema uelewa wa vijana kuhusu umuhimu wa Tehama unaongezeka kwa kasi na kwa sasa Tume ya Tehama imesajili wataalamu wa Tehama 1,600 kwenye kanzi data ya taifa ya wataalamu.
“Hii inawezesha kuwajengea uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya Tehama,” amesema Mwasaga na kuongeza, katika eneo hilo ya kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa Tehama, tume ipo kwenye mazungumzo na shule na vyuo vya elimu ya uchumi Urusi ili kuweza kujengeana uwezo kwenye mafunzo ya maeneo mbalimbali ya ujuzi wa Tehama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Moshi Kakoso alionesha kuguswa na mkakati huo huku akihimiza kuhakikisha sekta ya Tehama inakuwa na ubora unaotakiwa.
“Dunia sasa hivi imeshabadilika. Tunahitaji wataalamu wengi. Mna Mawazo mazuri sana, lakini tunashauri ongezeko kasi katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kukuza Maendeleo ya Teknolojia ya sasa ni ya hali ya juu,” amesema.
“Hawa vijana bado hatujawapa nafasi ya kutosha. Wakipewa ujuzi, wana mengi ya kufanya katika kuchangia mapinduzi ya kiteknolojia na kushiriki katika kuujenga uchumi wa kidigitali. Tuwaige Wachina, walipeleka vijana wengi sana nje ya nchi yao Kwenda kujifunza ujuzi kutoka kwa Marekani. Sasa hivi Wachina wako mbali mno na teknolojia inawalipa kwa sababu wamewekeza katika teknolojia,” amesema Kakoso.