TMA yatabiri mafuriko, maporomoko mikoa 14, Dar ipo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema maeneo yanayopata mvua za chini ya wastani hadi juu ya wastani yanatarajiwa kuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

TMA imesema vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, yanayoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, mlipuko wa magonjwa pamoja na upotevu wa mali na maisha.

Maeneo yanayotarajiwa kunyesha mvua za chini ya wastani hadi wastani ni mikoa ya  Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.

Mikoa inayopata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni mashariki mwa mikoa ya Simiyu na Mara.

Hata hivyo, Mwananchi imemtafuta Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali, Hosea Ndagala kujua walivyojipanga iwapo hali hiyo itajitokeza.

“Tunafuatilia taarifa ya utabiri uliotolewa na TMA kisha tutaeleza tulivyojipanga,”amesema Ndagala.

Leo Alhamisi, Januari 23, 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amekutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa masika unaotarajia kuanza Machi hadi Mei 2025.

Amesema hali mbaya ya hewa imesababishwa na ongezeko la joto duniani ambapo imefikia nyuzi joto 1.55, huku upande wa Tanzania ni nyuzi joto 0.7 kwa mwaka 2024.

Dk Chang’a amesema ongezeko la joto hilo linasababisha kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vimbunga vinavyoweza kujitokeza kwa ukubwa.

Kutokana na hali hiyo, Dk Chang’a amezitaka mamlaka za maafa nchini kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za masika.

Dk Chang’a amesema menejimenti ya maafa inatakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

“Ongezeko la mvua kubwa linatarajiwa Aprili 2025 kutakuwa na vipindi vya unyevu wa kuzidi pamoja na mafuriko vinavyoweza kuathiri ukuaji wa mazao na magonjwa ya milipuko yanaweza kutokea kutokana na uchafuzi wa maji,” amesema Dk Chang’a.

“Kwa upande wa wakulima wanashauri kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maofisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi.”

Amezungumzia sekta ya usafiri na usafirishaji wanashauriwa kuchukua hatua katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali Ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wa nishati na madini amesema upungufu wa maji unaweza kusababisha ongezeko la gharama za kutibu maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na endelevu ya rasilimali maji, ikiwemo uzalishaji wa umeme wa maji.

Dk Chang’a amesema kwa upande wa mamlaka za miji na wilaya zinashauriwa kutoa elimu ya uelewa kwa timu mbalimbali za usimamizi katika halmashauri kuhusu hali ya hewa inayotarajiwa msimu huo.

Related Posts