Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema wataendelea kukusanya kodi kwa manufaa ya Taifa bila kuingia migogoro na walipakodi.
Katika kufanikisha hilo amesema kama mamlaka wanaendelea kuimarisha mazingira ya ulipaji kodi kwa kujenga uhusiano na walipakodi nchini pamoja na kuboresha mazingira ya mfumo wa ulipaji kodi.
Mwenda ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 23, 2025 kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa walipa kodi bora wa mwaka 2023/2024 ya Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayofanyikia katika ukumbi wa The Super Dom Masaki jijini Dar es Salaam.
“Tutajitahidi kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa bila migogoro na walipaji, kusimamia maadili kwa watumishi wa TRA, kutatua migogoro na kusimamia ulipakodi wa hiyari, kupunguza cash economy (uchumi wa fedha taslimu) kwenye nchi yetu,” amesema Mwenda.
Amesema kwa sasa kuna mapinduzi makubwa katika shughuli za usimamizi wa kodi, uboreshwaji wa mazingira na mifumo ya usimamizi wa kodi, kusimamia ustawi wa walipakodi kwa kupambana na wachache wanaokwepa kodi.
Katika hatua nyingine ili kuhamasisha ulipaji kodi nchini, Mwenda ametaja vigezo kwa washindi wa tuzo za walipakodi bora amesema ni wale walioweka rekodi ya utunzaji wa kodi, anayelipa kodi kwa hiyari na wakati, anayefanya matumizi ya mashine za EFD na matumizi ya stempu za kielektroniki pamoja na anayelipa kiasi kikubwa cha kodi na anayetoa ushirikiano mzuri kwa TRA.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema mapato yanaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa kodi pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.