Vigogo wamimina kongole uendeshaji uchaguzi Chadema

Dar es Salaam. Wadau wa demokrasia nchini, wamekipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuendesha uchaguzi wake kwa uhuru, haki na uwazi na hatua ya Freeman Mbowe kukubali matokeo akivitaka vyama vingine kuiga mfumo huo kuonyesha ukomavu. 

Licha ya kuonyesha doa la uchaguzi huo kuchukua muda mrefu hadi kupatikana mshindi, wamesema mchakato mzima umeonyesha mfano wa demokrasia na unaakisi kile wanacholalamikia kwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi wa Taifa katika kutenda haki. 

Mkutano Mkuu wa Chadema, ulianza Janauri 21, 2025 na kumalizika mchana wa Januari 22 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Mbowe aliyeshindwa na Tundu Lissu kwenye nafasi ya mwenyekiti, alikubali matokeo na kumtakia heri Lissu na timu yake nzima kukiendeleza chama hicho.

Makamu mwenyekiti Bara aliyechaguliwa ni John Heche, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Mzee. Lissu alimpendekeza John Mnyika kwa Baraza Kuu nalo likaridhia aendelee kuwa katibu mkuu.

Leo Alhamisi, Januari 23, 2025, Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali waliouangazia uchaguzi huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Balozi Ami Mpungwe, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi-Bara, Joseph Selasini na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere (MNF), Joseph Butiku ambao wamekuwa na mitizamo inayofanana juu ya kile walichokishuhudia.

Sumaye ambaye mwaka 2015 alihamia Chadema na 2020 akarudi CCM, amesema licha ya kwamba hakuwa kwenye uchaguzi huo, lakini aliufuatilia kupitia runinga na ulikwenda vizuri. 

“Uchaguzi ulikwenda vizuri, ulikuwa wa kidemokrasia na walioshinda na walioshindwa wameondoka kwa upendo, wamekumbatiana, kwa ufupi ni uchaguzi mzuri,” amesema Sumaye. 

Maoni ya Sumaye yanashabihiana na ya Butiku aliyesema uchaguzi wao uliendeshwa vizuri, walishindana, mmoja akamshinda mwenzake na aliyeshindwa amekuwa mstaarabu. 

“Hawakupigana ila walipongezana. Mbowe ametoka, ametoa maneno mazuri, ndivyo tunatamani inchi iwe, ni mfano mzuri, ilitendeka demokrasia. Walibishana muda mrefu hakuna aliyesema huyu asigombee lakini aliyekaa muda mrefu ameshindwa na amekubali,” amesema Butiku.

Butiku aliyekuwa katibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere amesema vijana wanapaswa kujifunza utamaduni huo, siku wakiwa kwenye nafasi ya uenyekiti kwa chama chochote na wanashindana wakishindwa wakubali, hiyo ndio maana ya demokrasia. 

“Tuwapongeze hawa watu kwa kuendesha uchaguzi wa haki, sijasikia kama kuna maneno, uchaguzi ulikuwa wa amani na wanasisitiza umoja na wanasema nchi yetu ibaki na amani kwa kuwa nchi ni kubwa kuliko vyama,” amesema. 

Butiku amesema kwa kuwa wamepata ushindi na malengo yao ni kuchukua dola, ni muhimu wajue mahitaji ya wananchi, wanataka jambo gani na wana hali gani. 

“Nitoe rai kwa vyama vingine kuzingatia demokrasia kama Chadema walivyofanya kuhakikisha chaguzi wanazofanya amani inatawala, wakubali kutofautiana kama anavyosema Mbowe, uchaguzi si vita,” amesema.

Amesema uchaguzi ni njia ya kuamua katika hali ya sasa na muda wa miaka mitano ijayo, yupi anafaa kuwaongoza na wapigakura wanapaswa kupewa nafasi ya kuamua. 

“Wapigakura wakiamua tuheshimu hilo, tuache ubishi, basi na tuzingatie maadili ingawaje sijasikia nchi yetu ina matatizo ya kimaadili,” amesema Butiku.

Kwa upande wake Balozi Ami Mpungwe amepongeza hatua hiyo ya Chadema akisema ni muhimu michakato ya kidemokrasia ikawa wazi kuliko kuificha. 

“Kuwa na michakato ya wazi ya kidemokrasia itawaimarisha badala ya kuwagawa, si jambo la Chadema pekee lakini linavutia nchi nzima pale unapoona vyama vya siasa vinajiimarisha, inakuwa afya kwa nchi,” amesema Mpungwe 

Mpungwe aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, amesema ni matarajio yake mchakato huo utakuwa somo na kuambukizwa kwa vyama vingine, ingawa wanaweza kuona kuvurugika kwa chama.

“Kama unataka kujenga jamii yenye nguvu na utamaduni wa demokrasia safi ni vyema kuwa na mifumo ya wazi, tukifanya hivyo tunaweza kupeleka mambo yetu vizuri kama nchi,” amesema. 

Amesema siasa inabadilika ni muhimu ikajengwa kwa sababu bado Tanzania uchumi wake si mkubwa, lazima watu wawe huru kutoa fursa ya watu kushiriki moja kwa moja katika kukuza uchumi wao. 

“Demokrasia kwangu si siasa tu, tunahitaji kupambana na uhuru wa hali yetu na huwezi kufanya hivyo kama umefungwa mikono. Kama tunataka kufanikiwa eneo zuri ni kuimarisha taasisi za kisiasa na michakato yake,” amesema.

Akijadili uchaguzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kwa namna ulivyoendeshwa, unaakisi kile walichokuwa wanalalamikia kwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi wa Taifa juu ya kutenda haki. 

“Chadema imejitahidi yenyewe kuonyesha ni namna gani inaweza kuusimamia uchaguzi kwa ufanisi na kutafsirika uchaguzi huru na haki, kuanzia kuhakiki uhalali wa wapiga kura na mchakato mzima kufanyika kwa uwazi,” amesema.

Amesema uchaguzi huo unaangaliwa kama wa mfano na wa kihistoria kwa kuwa Chadema hawajawahi kufanya uchaguzi wa aina hiyo, ni wa kwanza na ulikuwa na ushindani mkubwa. 

“Kampeni za uchaguzi zilianza vibaya kwa kutuhumiana kwa wazi na kurushiana makombora, ambayo baadhi ya watu walikuwa wanadhani yanaweza kukibomoa chama,” amesema. 

Amesema baada ya hayo yote na mshindi kupatikana, mazungumzo yalibadilika na kujikita kwenye maridhiano na kutaka kila upande kama matokeo hayako upande wao waunge mkono wengine.

“Kitendo cha kumbakiza John Mnyika ni dalili njema kwa Lissu, si kwamba anataka kufanya mabadiliko katika eneo la utendaji, anadhani ni sahihi abakie na kuwaingiza wengine na anajua anachokitaka kwa kukipeleka chama,” amesema. 

Dk Mbunda amesema kwa namna uchaguzi huo ulivyoendeshwa na kufanyika unaweza kubadili taswira ya uchaguzi mkuu unaokuja baadaye mwaka huu, kwa kuwa kuna waliodhani Chadema wamevurugana na hawatakuwa na nguvu. 

“Kilichotokea kama wameuwasha moto na utaendelea kusambaa kuelekea uchaguzi mkuu na watu wanaweza kuanza kupata matumaini, hasa kwa sababu Lissu ni mtu anayejua kujenga hoja na haogopi kuanika mabaya yanayofanywa na wapinzani wake,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi-Bara, Joseph Selasini amesema uchaguzi huo mwisho wake ulikuwa mzuri lakini kabla ya hapo alishuhudia vituko ambavyo havina afya kisiasa. 

“Tangu mwanzo nilisema ni makosa makubwa kumshindanisha makamu na mwenyekiti wake, wote walikuwa kwenye uongozi kipindi kimoja, kwa sababu wapiga kura wanapima uongozi uliopo ulifanya nini na kama wanaomba kurudi watafanya nini,” amesema Selasini aliyewahi kuwa mbunge wa Chadema. 

Amesema kuwashindanisha wawili hao lazima kutaibuka makundi yanayopingana na katika mchakato yalijitokeza mengi, ambayo ni neema za Mungu awajalie warudi kuwa kitu kimoja. 

Wakili Alute Mghwai, kaka wa Tundu Lissu, amesema mchakato wa uchaguzi huo uliendeshwa kwa uhuru na haki na hatimaye mshindi akapatikana kwa njia ya kidemokrasia. 

“Chadema wameonyesha mfano unapaswa kufuatwa na vyama vingine vya kisiasa nchini pamoja na CCM, juu ya namna ya kuongoza na kuendesha chaguzi zake za ndani kwa njia ya demokrasia,” amesema 

Wakili Alute amesema fundisho lingine Chadema wamepata wagombea waliokuwa wanawataka, si viongozi waliosimikwa na mamlaka za juu ya chama hicho. 

“Pamoja na changamoto zake, kwenye mchakato huo wameweza wamebaki wamoja hawajavurugana, naamini chama kitakuwa nguvu za pamoja kwa sababu vyama vya upinzani vikiwa na nguvu vitafanya chama dola kuwa na nguvu vilevile,” amesema. 

Amesema vyama vya upinzani vikiwa na nguvu vinaisimamia Serikali na watumishi wake kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa huku akieleza alizungumza na Lissu kumpongeza na Katibu Mkuu, John Mnyika kwa namna walivyoendesha uchaguzi. 

“Natafuta mawasiliano ya Mbowe vilevile niweze kumpigia simu kumpongeza kwa kuongoza uchaguzi vizuri na kuhakikisha chama kinabaki kimoja,” amesema. 

Wakili Alute amemshauri Lissu wakati mwingine watenge muda wa kutosha, wasichanganye na ajenda nyingine, ili uchaguzi umalizike mapema siku hiyo hiyo. 

“Tunataka uchaguzi uanze mapema na umalizike siku hiyohiyo, si vizuri uchaguzi kuchukua siku mbili kama juzi, walianza mchana na kuja kumaliza uchaguzi siku ya pili na watu hawakuwa wengi,” amesema. 

Alitolea mfano uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika uliofanyika Dodoma Agosti 2024 wapiga kura walikuwa zaidi ya 2000, shughuli ilianza mapema hadi saa tatu usiku ulikuwa umeisha. 

“Sasa Chadema walikuwa wapiga kura wachache inakuwaje wanatumia siku mbili, jambo hilo linapaswa kutazamwa upya lakini pia waboreshe namna ya kushughulikia malalamiko ya wagombea kwa kuongeza muda ili kutenda haki,” alisema. 

Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa, Richard Kasesela amewapongeza Chadema kwa kuendesha uchaguzi vizuri na kujitahidi kuchaguana bila kutifuana na hatimaye Mbowe ameachia.

“Natoa angalizo CCM, tunasimama na 4R, na tunapenda na wao wangesimama kwa minajiri hiyohiyo, sasa ukiangalia waliochaguliwa kwa asilimia kubwa wote ni wanaharakati kinakuwa chama cha harakati,” amesema. 

Kasesela anasema hofu yake kwa kuwa jopo nzima linaundwa na wanaharakati muda mwingi wanaweza kutumia mfumo wa harakati kudai mambo.

“Kama kutakuwa na jambo njoo tukae tu, Watanzania ni watu tunaokaa pamoja kuzungumza kukiwa na jambo kulijadili, nategemea hayo ingawaje naona kamati kuu yao iliyoundwa wote ni wanaharakati, mwenyekiti, makamu wote ni walewale,” amesema.

Kasesela amesema kwa sura hizo anaamini kabisa watajipanga kiharakati kwa kila jambo kama nchi imeshapiga hatua na limejikita kimaendeleo zaidi kuliko kubishania mambo ya kiharakati.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa pongezi kwa Chadema na wanachama wake kwa kufanya uchaguzi kwa uwazi, utulivu na weledi wa hali ya juu. 

“Tunavisihi vyama vingine vya upinzani nchini viige kilichofanywa na Chadema kuweka uhalali wa viongozi wa vyama hivi ambavyo vingine vina viongozi wa kudumu,” imeeleza TEF kupitia taarifa yake kwa umma iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Deodatus Balile.

Balile amesema wanawapongeza viongozi wa chama hicho kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa aliouonyesha Mbowe, aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21 kwa kukubali kushindwa.

“Tunafahamu ulikuwapo msuguano mkubwa wakati wa kampeni na joto lilipanda hadi polisi wakaimarisha ulinzi kwa kiwango ambacho hakijapata kushuhudiwa,” amesema.

Related Posts