Vivuko vipya kupunguza machungu Kigamboni

Dar es Salaam. Milango ya ushirikiano kati ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na sekta binafsi, imeanza kufungukia kwa huduma za vivuko katika eneo la Magogoni-Kivukoni.

Hilo ni baada ya wakala huyo kushirikiana na Azam Marine Ltd katika utoaji huduma hiyo na tayari vivuko viwili vya kasi vimezinduliwa kuanza huduma katika eneo hilo.

Milango hiyo inafunguka mwezi mmoja tangu wakala huyo utoe wito kwa wazabuni wa sekta binafsi kushirikiana katika huduma zake mbalimbali, zikiwepo za vivuko.

Mzizi wa wito kwa sekta binafsi ni ripoti maalumu ya Gazeti la Mwananchi iliyochapishwa miezi minane iliyopita, ikionyesha namna mifumo ya Temesa inavyoweka ugumu kwa sekta binafsi kuwekeza katika huduma za vivuko.

Katika ripoti hiyo ya uchunguzi wa takriban miezi mitatu ndani ya wakala huo, Mwananchi lilieleza kutobadilishwa kwa viwango vya nauli, jambo linaloiogopesha sekta binafsi kuwekeza.

Temesa inatoza nauli ya Sh200 kwa kila abiria anayepanda vivuko, kiwango kinachotajwa kutoendana na uhalisia wa gharama za uendeshaji wa vivuko, hivyo wawekezaji walitoa sharti ili wawekeza lazima nauli iongezwe kutoka Sh200 hadi angalau Sh500 kwa kila abiria.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango hicho cha nauli kinazua hofu kwa wawekezaji kuwekeza, wakihisi watapata hasara.

Kukosekana kwa sekta binafsi, kulisababisha uhaba wa vivuko katika eneo la Magogoni-Kivukoni na hivyo abiria alilazimika kutumia dakika 45 hadi saa moja kusubiri kuvushwa.

Akizungumza katika uzinduzi wa ushirikiano huo, leo Alhamisi Januari 23, 2025, Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala amesema mkataba huo wa ushirikiano unagharimu Sh5.98 bilioni.

Mkataba huo wa miaka minane, amesema unahusisha ujenzi wa majengo ya kupokea na kupumzikia abiria na ofisi.

Kadhalika, amesema utahusisha usimikaji mageti na mfumo wa ukusanyaji nauli, sambamba na vivuko vya kasi vitatu.

Ameeleza mkataba huo utadumu kwa miaka minane na utafanyiwa mapitio kila baada ya miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Kilahala, katika vivuko hivyo vya Azam Marine Ltd, abiria atatozwa Sh500 kwa safari moja.

Kuwepo kwa vivuko hivyo, amesema kutapunguza muda wa takriban dakika 45 ambazo abiria alikuwa akisubiri huduma, lakini sasa utakuwa chini ya dakika tano.

“Kwa sasa wakazi wa Kigamboni watakuwa na uhuru wa kuchagua kivuko ambacho wangependa kupanda kuvuka,” amesema.

Amesema Temesa inaendelea na utekelezaji wa ukarabati wa vivuko vya MV Kigamboni kilichofikia asilimia 10 na MV Magogoni kilichofikia asilimia 55.

Matengenezo hayo kwa ujumla, amesema yanagharimu Sh23.04 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine Ltd, Aboubakar Aziz amesema kati ya vivuko hivyo viwili, kila kimoja kitabeba abiria 250 kwa wakati mmoja.

Vivuko hivyo, amesema vitaanza kutoa huduma saa 11:00 alfajiri hadi saa 5:00 usiku na vinakadiriwa kwa saa vitahudumia takriban abiria 5,000.

Sambamba na vivuko hivyo viwili, Aziz amesema vingine vinne vinaendelea kujengwa na kabla ya Mei mwaka huu vitaanza kutoa huduma.

“Vivuko hivi vimejengwa kwa aluminiam maalumu kwa shughuli ya uvushaji wa abiria na vimejengwa katika karakana ya meli ya Songoro Marine, Dar es Salaam,” amesema.

Kwa mujibu wa Aziz, kila kivuko kina injini mbili na vimekidhi viwango vya usalama vya Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC).

Katika uwekezaji huo, amesema wamejenga majengo mapya ya kupokea na kusubiri abiria watakaotumiwa na vivuko hivyo.

Amesema Azam Marine Ltd kwa ujumla imetoa ajira za moja kwa moja 470 nchini na inahudumia abiria milioni mbili kwa mwaka Tanzania Bara na Zanzibar.

Ameeleza kwa siku wanahudumia wastani wa abiria 5,000 na kwa idadi ya vyombo walivyonavyo wanaweza kuhudumia abiria 12,000.

Aziz ameeleza Sh250 bilioni zimewekezwa kati ya mwaka 2010 hadi 2014 katika uwekezaji wa huduma majini.

Amesema wanatarajia kuongeza chelezo kwa pande zote mbili ili kuwezeshe vivuko vitatu vihudumie kwa pamoja na sio kusubiriana.

Ameeleza baada ya uwekezaji huo, huduma ya kivuko itapatikana chini ya dakika tano.

“Tunaamini tutapunguza adha na kuwarahisishia wananchi usafiri wanapoelekea kwenye shughuli zao,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema kuwepo kwa vivuko hivyo vya sekta binafsi, hakuondoi vivuko vya Serikali, bali abiria atakuwa na nafasi ya kuchagua.

“Isiwe kivuko kikawa kikwazo cha watu kufanya biashara zao, au wanakwenda hospitalini na kutoa huduma mbalimbali wakashindwa kufanya hivyo kwa wakati eti sababu tu, kivuko kipo upande mwingine,” amesema.

Amesema vivuko vilivyopo vinapaswa kukaguliwa kila wakati na ndio maana vikifikia muda wa matengenezo vinakwenda kukarabatiwa.

“Niwahakikishie kwamba vivuko vile vitakapokuwa tayari vitarejea hapa na vitafanya kazi kwa ushindani na hiyo itatufanya tusibweteke na tuwe wabunifu na itafanya tuwe wabunifu,” amesema Ulega.

Amesema kivuko cha Azam Marine kitavusha abiria kati ya dakika tano hadi sita kutoka eneo moja kwenda lingine.

Waziri Ulega amesema kiu ya Serikali ni kuhakikisha watu wanaovushwa katika eneo hilo wanafikia 70,000 kutoka 60,000 wa sasa.

Ulega ameishawishi Azam Marine Ltd kuangalia uwezekano wa kwenda kuwekeza huduma za vivuko katika maziwa yote nchini.

“Nawaomba kwa dhati Azam Marine wakawekeze na wakati wa kufanya hivyo ni sasa,” amesema waziri huyo na kuwataka wavuvi katika eneo hilo, kufanya shughuli zao bila kuathiri uvushaji wa wananchi.

Amezitaka pia mamlaka zinazofanya ukaguzi ziwe zinakagua mara kwa mara ili kuweka mazingira safi na ulinzi dhidi ya vitu vinavyoharibu vivuko, zikiwemo nyavu za wavuvi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso ameisihi Serikali kutoa nafasi kwa wataalamu wa ndani katika matengenezo ya vivuko.

“Tunaiomba Serikali iwekeze zaidi tuwape fursa wawekezaji wa ndani ili wakuze uchumi,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uwekezaji huo, utakomesha changamoto ya abiria kuchelewa kwenda kwenye shughuli zao.

Related Posts