Walioandika matusi kidato cha nne kuadhibiwa na wazazi wao

Dar es Salaam. Wanafunzi watano walioandika lugha za matusi kwenye kwenye mitihani ya kidato cha nne wataadhibiwa na wazazi wao.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Januari 23, 2025 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Said Mohammed wakati akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024.

Wanafunzi hao watano ni kati ya watahiniwa 72 waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne.

Dk Mohammed amesema mbali na kufuta matokeo ya wanafunzi hao, pia wameziandikia barua shule walizosoma ili kutoa taarifa kwa wazazi wao wawachukulie hatua za kimaadili kwa kuandika matusi.

“Kuandika matusi kunaendana na suala la maadili si kwenye mitihani tu, hadi kwingineko na matusi hayakubaliki kila mahali.

“Mwaka huu wametokea watano walioandika matusi kwenye matokeo ya kidato cha nne, katika matokeo ya kidato cha pili pia walitokea watano na mwaka 2023 kwenye matokeo ya kidato cha nne walitokea watano,” amesema.

Amesema kuandika matusi si jambo ka kimaadili na jamii inahitajika kuendelea kukemea.

Aidha, katika matokeo hayo ufaulu umeongezeka kwa asilimia tatu ikilinganishwa na ya mwaka 2023.

“Asilimia 92.32 ya watahiniwa wamefaulu kwa kupata darala la kwanza hadi la nne mwaka 2024 kulinganisha na asilimia 89.36 waliofaulu kwa madaraja kama hayo mwaka 2023,” amesema Dk Mohammed.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi kuhusu matokeo

Related Posts