Wazee Japan walipia Sh400,000 ili wafungwe gerezani, sababu yatajwa

Tokyo. Wakati baadhi ya watu nchini wakiogopa kufungwa gerezani hata kama wametenda makosa, hali ni tofauti nchini Japan ambako wazee wanalazimika kulipia fedha ili wafungwe gerezani.

Kwa mujibu wa tovuti ya CNN, nchini Japan wazee wanalazimika kulipia kati ya Yuan 20,000 hadi 30,000 (wastani wa Sh400,000) kila mwezi kwa ajili ya kuishi katika magereza yaliyopo nchini humo.

CNN imeripoti kuwa ukitembelea kwenye magereza ya nchi hiyo, utakuta vyumba vingi vimefungwa ishara ya kuwa kuna watu wanaoendelea kutumikia adhabu zao, la hasha! Wengi wao ni wazee waliokacha makazi yao na kukimbilia maisha ndani ya magereza hayo.

Imeripoti kwamba ukibahatika kukaa ndani yake kwa muda mrefu, utakutana na wazee wakitembea kwenye korido, wengine wakitumia vifaa vya kuwasaidia kutembea ‘Walkers’.

Japo siyo makao ya wazee, lakini aina hiyo ya wateja gerezani hujitokeza kwa wingi kutokana na upatikanaji wa huduma wanazokosa wakiwa kwenye familia zao ikiwemo kuogeshwa na wafanyakazi wa magereza hayo, kusaidiwa kufanya mazoezi na kukumbushwa kumeza dawa za maradhi yanayowatesa.

Ofisa wa Polisi katika Gereza la Tochigi nchini Japan, Takayoshi Shiranaga aliieleza CNN kuwa ‘Upweke’ ni sababu nyingine inayosababisha wazee hao ‘kutoboka mifuko’ ili kuishi katika magereza hayo hususan ni wanaohofia kuishi wenyewe nyumbani.

“Pia kuna watu ambao wanalipia hadi Yen kati ya 20,000 au 30,000 (Dola za Marekani 130-190) kila mwezi ili waishi milele ndani ya gereza,” anasema Shiranaga katika mahojiano ya CNN ilipotembelea gereza hilo Septemba mwaka 2024.

Ndani ya gereza hilo, kumenakshiwa kwa rangi ya ‘pink’ na kuta zenye michoro mbalimbali, kwa mbali anaonekana, Akiyo ambaye ni mfungwa wa kike mwenye umri wa miaka 81. Akiyo anaonekana akipatiwa chakula ndani ya gereza hilo.

“Kuna watu wazuri sana ndani ya gereza hili,” alisema Akiyo, ambaye siyo jina lake halisi kwa sababu za kuheshimu faragha yake huku akiongeza kuwa: “Kwa kweli hakuna maisha mazuri na ya amani kwangu kama nikiwa humu.”

Wafungwa ndani ya gereza la wanawake la Tochigi nchini humo huishi huku wakitakiwa kufanya shughuli mbalimbali kwenye viwanda, hata hivyo maisha hayo yanaonekana kuwafurahisha na kuwavutia wazee nchini humo.

Yoko (51) aliieleza CNN kuwa ndani ya gereza hilo wanapatiwa chakula, huduma ya afya bila malipo na uangalizi wa msingi kwa wazee, huduma ambazo anadai hazipatikani wanapokuwa katika jamii na familia yao.

Yoko, (siyo jina halisi) alisema hata kabla ya kurejea na kuomba kufungwa ndani ya gereza hilo kwa gharama zake, anasema aliwahi kushtakiwa kwa makosa ya dawa za kulevya kwa zaidi ya miaka 25.

Alisema kadri anavyozidi kukaa ndani ya gereza hilo, idadi ya wafungwa inaongezeka hususan ni wenye umri mkubwa na vikongwe.

“Ndani ya gereza humu tuna watu ambao wakati mwingine wanafanya matendo mabaya huko nje ili tu wafungwe katika gereza hili hususan ni wale ambao wanaishiwa pesa ya kulipia gharama za kufungwa humu,” alisema Yoko.

Akiyo anadai kupitia wakati mgumu kutokana na kutengwa na familia yake na uchumi hafifu. Anasema ni mara yake ya pili kuishi gerezani huku kumbukumbu yake ikiwa kifungo alichopewa miaka ya 1960 kwa kosa la kuiba chakula.

“Kama ningekuwa na kipato cha kutosha ama familia ingekuwa inanijali, ninaamini ningeishi maisha mazuri na yenye furaha, lakini ndiyo hivyo, havipo ndiyo maana niliiba chakula na kufungwa humu,” alisema.

Akiyo alisema kabla kufungwa anakumbuka alitamkiwa na mtoto wake wa kiume (43) kuwa anatamani aondoke na kutokomea ili asiendelee kutumia muda mwingi kumhudumia.

“Nilijihisi kama sina nilichobakisha duniani, niliona hakuna sababu tena ya mimi kuishi na nilitamani kufa, lakini nashukuru matumaini ya kuishi yamerejea nikiwa gerezani,” alisema.

Miongoni mwa mbinu inayotumiwa na wazee nchini Japan ili kupata fursa ya kufungwa magerezani ni pamoja na wizi, wengi wao ni wanawake. Mwaka 2022, zaidi ya asilimia 80 ya wafungwa wanawake (wazee) nchini humo walifungwa kwa makosa ya wizi.

Asilimia 20 kati yao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa lengo la kumudu maisha. Asilimia 20 ya raia wa Japan wana umri zaidi ya miaka 65 na wanapitia changamoto ya umaskini.

Kwa mujibu wa CNN, wengine hutenda makosa hayo pindi wanapobaini kuwa wamebakiwa na akiba kiduchu ya fedha ikilinganishwa na mahitaji yao wakiwa uraiani.

“Kuna watu ambao wanakuja kufungwa humu kwa sababu nje kuna baridi kali ama kwa sababu wanakabiliwa na njaa kali,” alisema mmoja wa walinzi katika gereza hilo, Shiranaga.

Kwa mujibu wa Shiranaga, wafungwa ambao wanaugua wakiwa ndani ya gereza hilo hupatiwa matibabu na huduma za msingi bure, ila wanapokuwa nje wanatakiwa kulipia gharama hizo endapo wataugua.

Kwa mujibu wa mwandishi wa CNN alipokuwa akikatiza kwenye Korido za Gereza hilo lililopo Tochigi, alibaini kuwa mfungwa mmoja kati ya watano ni mzee.

Nchini Japan, idadi ya raia wenye umri wa kuanzia miaka 65 iliongezeka mara tatu mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2003, na ongezeko hilo limeathiri idadi ya wafungwa magerezani.

“Sasa hivi tunawajibika hata kuwabadilishia ‘pampas’ (diapers), tunawasaidia kwa kuwaogesha na kuwapatia chakula. Tunapofanya hivyo tunajiona kama tunahudumia wazee,” alisema Megumi ambaye naye ni mlinzi katika gereza hilo.

Mamlaka nchini humo zilibaini uwepo wa ongezeko la wazee wanaokimbilia magerezani hususan mwaka 2021, ambapo idadi ya wazee waliorudia makosa ili kurejeshwa gerezani iliongezeka.

Wizara ya Sheria nchini Japan pia imeanzisha programu maalumu kwa ajili kuboresha huduma kwa wazee wanaokimbilia magerezani kupata huduma, kuwasaidia kuondokana na uraibu wa dawa za kulevya na kuwarejeshea upendo kwenye familia zao.

Serikali pia imeanzisha mpango maalumu kwa ajili ya kutoa makazi ya bure kwa wazee kwenye manispaa 10 nchini humo ili kutoa malazi kwa wazee nchini humo hususan wasio na familia na wanaokataliwa na ndugu zao.

Takwimu nchini humo zinaonyesha Japan itahitaji wataalamu wa kuhudumia wazee (caretaker) milioni 2 ifikapo 2040 ili kutosheleza mahitaji ya huduma kwa wazee nchini humo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Statista, idadi ya watu nchini Japan mwaka 2025, inakadiriwa kufikia milioni 123 huku idadi hiyo ikitarajiwa kupungua hadi milioni 120 ifikapo 2029 kutokana na taifa hilo kuwa na idadi kubwa ya wazee na vijana wengi wakikwepa kuzaa watoto kwa hofu ya ugumu wa maisha.

Related Posts