Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) iweke kipaumbele cha kuboresha mtandao wa uangazi wa taarifa za hali ya hewa katika maeneo madogo madogo ambayo bado hayajafikiwa na Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF)
Agizo lingine alilolitoa kwa mamlaka hiyo ni pamoja na kuendelea na kuimarisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa zitakazosaidia kutoa huduma na kuboresha zaidi shughuli za kijamii na kiuchumi zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Maagizo hayo ameyatoa Alhamisi Januari 21, 2025 jijini Dodoma alipokuwa akizindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF) – Project”.
Amesema Serikali imefanya maboresho na uwekezaji TMA ikiwemo upande wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kujenga uwezo wa wafanyakazi.
“Watumishi watakaopata fursa ya kufanya kazi katika mradi wahakikishe wanafanya kazi kwa uadilifu na weledi ili utekelezaji wa mradi huo uwe na tija inayokusudia kwa Taifa letu. Waratibu wa mradi wahakikishe wanazingatia mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati na kwa ufanisi uanotarajiwa,” amesema Majaliwa.
Amesema miongoni mwa uwekezaji huo ni ununuzi wa rada saba za hali ya hewa, upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa kwa kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Minamata.
“Lengo la uwekezaji huo na maboresho ni kuwezesha utoaji wa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa,” amesema Majaliwa.
Katika kuunga mkono utekelezaji wa mradi wa SOFF, waziri mkuu amesema Serikali imetenga fedha za kununua Vituo 11 vya Hali ya Hewa, vituo hivyo vinavyojiendesha vyenyewe vitachangia data katika Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi.
Pia, amesema Serikali inaunga mkono kwa kutoa mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni nne ambazo ni thamani ya mchango kwa njia ya huduma zisizo za kifedha (In-Kind contribution).
“Jitihada zote hizo, zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa,” amesema.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mradi wa SOFF “SOFF – Investment Phase Project”, Majaliwa amesema mradi huo una umuhimu mkubwa siyo tu kwa kukidhi mahitaji ya data za hali ya hewa na tabianchi kwa ajili ya utabiri wa hali ya hewa duniani, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na ubadilishanaji data za hali ya hewa kimataifa, hivyo kuimarisha huduma za hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
“Mafanikio katika utekelezaji wa SOFF yatachangia sana kuimarisha ustahimilivu wa matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maendeleo endelevu nchini,” amesema.
Amesema uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea unategemea sekta zinazohusiana moja kwa moja na hali ya hewa, ambazo ni kilimo, lakini pia, ufugaji, nishati, maji, afya, madini na usafirishaji.
Naibu Waziri, Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile amesema kwa sasa imani ya wananchi kuhusu masuala ya utabiri wa hali ya hewa imeongezeka na wanafuatilia taarifa za utabiri hali ambayo imesaidia kupunguza majanga kwa kiasi kikubwa.
“Mradi wa SOFF utasaidia kuboresha miundombinu ya uangavu wa hali ya hewa, hivyo kuiwezesha nchi kufikia viwango vinavyohitajika katika utoa wa taarifa za hali ya hewa, ambapo utarahisisha uoakoaji wa watu na mali zao. Wizara itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha shughuli za TMA ili kufikia lengo lililokusudiwa,”amesema .
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a ametaja faida za mradi huo unaogharimu Dola za Marekani zaidi milioni 13 kuwa ni pamoja na kuchangia kuongeza uwezo wa TMA katika utoaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini na duniani kwa ujumla.
“Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa mbalimbali, ambayo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa nchini kupitia ununuzi wa vituo vipya tisa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe, vituo vitatu vya uangazi wa anga za juu na maboresho ya vituo saba vya uangazi vinavyojiendesha vyenyewe na kituo kimoja cha uangazi wa anga za juu.”
Pia, Dk Chang’a amesema manufaa mengine uboreshaji wa huduma za tahadhari zitakazosaidia shughuli za kiuchumi na kupunguza hatari za majanga pamoja na kukidhi matakwa na mahitaji ya kimataifa kama Mtandao wa Uangazi wa Msingi wa Kimataifa.
Amesema TMA ni miongoni mwa taasisi bora za Hali ya Hewa barani Afrika zinazoaminika na kutumiwa na WMO kutoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine barani Afrika ikiwa ni pamoja na katika Mfumo wa Kusimamia Ubora (QMS), Mpango wa Pamoja wa Kutoa Tahadhari (CAP) na Utabiri wa Hali ya Hewa kwa njia ya Modeli za Kompyuta (NWP).
Awali, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya SOFF, Markus Repnik aliipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa iliyoufanya kwa TMA na kwamba wataendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha harakati za kuimarisha uangazi wa hali ya hewa zinafikiwa.